Tumeanza mpango wetu wa kutambua
uhatarishi na majanga na kusaidia katika kutafuta ufumbuzi kwa kutumia mbinu shirikishi.
Leo tumekutana na watoto na vijana (adolescents and youth) wa umri wa miaka
10-24 kupitia programu yetu ya Kijana Nitatoboa. Napenda kukushirikisha kama
mdau ili uhusike katika kufanya sehemu yako. Huu sio wakati wa kulalamika au
kulaumu bali ni wa kufanya unaloweza ili kupunguza madhara na kumlinda mtoto na
kijana. Tuunge mkono juhudi za serikali kwa kufanyia kazi yale tunayoyaweza
kama jamii, wazazi, walimu, viongozi na wanafunzi pia.
Washiriki
wa mdahalo wa leo wametaja uhatarishi ulioko kwenye mashule kama ifuatavyo:
Tunachapwa kupitiliza
mpaka mwanafunzi anajisaidia muda huohuo wa adhabu, mwalimu anatunyima ruhusu
ya kwenda kujisaidia mpaka mwanafunzi anajikuta amejisaidia darasani, chumba
cha darasa kina ufa ambao ni hatarishi, monita anasingizia kwamba mwanafunzi amepiga
kelele kama hatampa rushwa ya sh 200, monita akiomba kalamu ukimnyima anakuandika
kwamba umepiga kelele hivyo unaadhibiwa bila kosa, unaporipoti ofisini kwamba
kuna mwanafunzi amekupiga unaambiwa, ‘Na wewe kampige!’, tunalazimishwa kununua
bidhaa ili tusiadhibiwe, mwanafunzi anapewa simu ili kuwasiliana kwa siri na
kuhakikishiwa kwamba hatafeli somo lake.
Kuna matumizi mabaya ya
vyoo (wanafunzi hawamwagi maji kuflashi vyoo hata kama yapo), ukosefu wa maji
vyooni unasababisha matumizi ya vitu vinavyoziba mfumo wa maji taka kwenye vyoo,
wanafunzi wanaandika matusi kwenye kuta za vyoo, taulo za kike zinatupwa kwenye
vyoo vya kuflashi na kusababisha vyoo kuziba kwa vile hakuna mahali maalum pa
kuzitupa na pa kuzichoma.
Tunapigwa na wanafunzi
wakubwa na kuonywa tusithubutu kusema na kama utamwambia mwalimu, mwanafunzi
huyo anakusubiri ukitoka shule ili akupige vizuri, baadhi ya wanafunzi wanaandikiana
barua na kukabidhiana kwa siri muda wa darasani. Mmojawapo anasema aliandikiwa
barua lakini hakujua hatua za kuchukua.
Nilipowauliza kama
wanajua simu za dharura wanapokutana na uhatarishi au majanga, niligundua
kwamba wanajua chache sana. Lakini pia inaonyesha kwamba hakuna sehemu maalum za
kupatiwa huduma ya kwanza wanapopata matatizo ingawa kinadharia wanajua kutaja
vifaa vyote muhimu kuwepo kwenye sanduku la huduma ya kwanza.
Mwisho
Tutumie tathmini hii
ndogo kuwalinda watoto, vijana na walimu dhidi ya uhatarishi ulioko shuleni.
Naamini tukipata nafasi ya kuwahoji walimu pia tutagundua kwamba wanakutana na
uhatarishi mwingi unaotakiwa pia kufanyiwa kazi. Msongo wa mawazo unaweza
kumfanya mtu afanye mambo mengi ambayo hayakutarajiwa katika jamii
iliyostaarabika.
Beyond Four Walls,
Korogwe, Tanga