Hesabu
gharama kabla ya utekelezaji wa mpango wako
Maono: Nimeona mtu akisema
afadhali kwa sasa apange nyumba kwenye eneo ambalo ni salama kwake na mali zake
na barabara zinapitika kuliko kujenga nyumba mbali ambapo hakuna usalama na
barabara haipitiki kwa gari lake.
Maono haya hayana maana ya
kukatisha tamaa watu kujenga. Ila yanatufundisha tu umuhimu wa kuhesabu gharama
kulingana na wakati na kazi anayoifanya mtu. Mtu anaweza kulipa gharama kubwa ya
pango lakini anaingizia kipato kikubwa kuliko akikaa nyumba ya bure aliyoijenga
mwenyewe mahali penye gharama kubwa za ziada kv usafiri, usalama nk.
Kuna watu wengi wanapenda
kusingizia ‘imani’ mahali ambapo panahitaji ‘mipango’ na ‘mikakati’. Wanasahau
kwamba ingawa Bwana Yesu anatutaka tuishi kwa imani kuna mahali ametufundisha
kwamba tuhesabu gharama ili tusije tukaaibika na kuchekwa.
Lk 14:28-31 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka
kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya
kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote
waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana
nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme
mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi
ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?”
Ili kukazia ujumbe wake, Bwana
Yesu aliamua atoe mifano ya aina mbili tofauti yenye maana moja ya
kututahadharisha kwamba TUSIKURUPUKE bali TUJITATHMINI KWANZA NA KUJIRIDHISHA
KWAMBA TUNAWEZA. Alitumia mfano wa UJENZI na mfano wa VITA. Tuache tabia ya
‘kukopa na kuahidi kwamba tutalipa kwa imani.’ Lazima tuwe na mkakati wa
ulipaji unaoeleweka. Tusijiingize kwenye miradi au vita ambazo iko wazi kwamba
adui ana nguvu au silaha za kisasa kuliko sisi. Tunashauriwa tutumie njia ya kidiplomasia
zaidi kuliko kujipanga kwa vita tusizoziweza.
Mfano hai: Katika semina ya
vijana niliwaomba tupige mahesabu ya kulinganisha kipato cha mfanyakazi wa
nyumbani (house girl/boy) na waajiriwa kwenye steshenari, ofisi nk. Tukagundua
kwamba wanalipwa kati ya sh 80,000 mpaka 150,000 kwa mwezi lakini wanajitegemea
malazi, umeme, maji, chakula, matibabu na pango. Na sio rahisi baada ya
matumizi hayo abaki na sh 50,000 kama faida. Tulipoondoa gharama za ziada kwa
msichana wa kazi tuligundua mtu anayejitegemea anaweza kumfikia kama atalipwa
mshahara usiopungua 250,000 kwa mwezi. Hata hivyo inategemea mfanyakazi wa
nyumbani anafanya kazi kwa nani. Maana kuna watu hawashindwi kumkata msichana
wa kazi posho yake anapohitaji Panadol. Hawana huruma kiasi kwamba wanathubutu
kumnyanyasa mtu anayewapikia. Hawaogopi kulishwa vitu vichafu. Lakini pia
wazazi wa wasichana wa kazi wengine wanawanyanyasa kwa kuchukua mshahara wote
bila huruma. Lakini huu unyanyasaji haupo kwao tu. Hata walioajiriwa pia
wanakutana na unyanyasaji katika sehemu za kazi.
Mambo kadhaa ya kujifunza
kuhusu utendaji wa Mungu tunayemuabudu
1.
Alipopanga kumuumba mwanadamu alishirikisha (kikao kilifanyika)
Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano
wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na
wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Hapa tunaona Mungu ambaye
angeweza kuumba tu mwenyewe anasema, “Na tumfanye mtu.” Lakini pia
akashirikisha huyo mtu awe na sifa zipi. 1. Awe na sura ya Mungu kv utashi.
Malaika hawana uwezo huo. Wao wanatumwa tu kutekeleza maagizo. 2. Awe mtawala
wa viumbe vingine na mazingira yake.
Mungu hakumtengenezea Adamu
barabara wala kumjengea nyumba bali alimpa akili na ubunifu wa kubadilisha
mazingira yake.
2.
Aliumba kwa utaratibu maalum
Mwa 1:12,13 “Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa
jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi
yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.”
Mungu hakushindwa kuumba vitu
vyote kwa sekunde moja. Lakini aliamua kutufundisha kuwa na ratiba na utaratibu
kwa kuzingatia nini kianze na kipi kifuate. Lakini pia alitathmini kwanza kazi
aliyoifanya ndipo akaumba nyingine – Mungu akaona kuwa ni vyema.
Watu wengi leo wamelemewa na
matatizo kwa sababu tu hawana VIPAUMBELE. Mfano, mtu hana nyumba ya kukaa
ananunua gari na kulipaki polisi. Mwingine badala ya kusoma kwanza anaamua aoe
na kujikuta masomo yanamshinda. Mwingine ananunua sofa ili ajionyeshe wenzake sebuleni
wakati hana kitanda chumbani. Mwingine anatumia pesa zote kwenye kusomesha kwa
gharama kubwa bila kuwekeza katika maisha yake binafsi. Matokeo yake anataka
kuwaalani watoto wakishindwa kumsaidia wanapopata kazi nk.
3.
Mungu hakumuumba mwanadamu mpaka alipomtengenezea mazingira
Mwa 1:27,28 “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa
mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia,
Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale
samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho
juu ya nchi.”
Kwa vile Mungu alijua
mwanadamu atahitaji hewa, mwanga, maji, chakula nk alihakikisha anatanguliza
vitu hivyo. Mara ngapi umenunua vitu ambavyo kwa sasa havina faida kwako.
Mfano, mtu anakushawishi ununue kifaa kinachotumia umeme mwingi na unakinunua
wakati nyumba yako sio tu kwamba haina umeme bali hukuwa na mpango wa kuweka
miundombinu ya umeme mkubwa.
Lazima tujifunze kufanya
upembuzi yakinifu (feasibility study) ili kujiridhisha kama kuna uwezekano wa
kufanikiwa katika mipango tunayoifanya. Unaweza kudhani ukihamia mji fulani
utafanikiwa kwa vile utalipwa mshahara mkubwa na kumbe gharama za maisha za
mahali hapo ziko juu sana.
Ndiyo sababu kila tunapotaka
kufanya kazi zetu za kiroho na kijamii tunaingia gharama kufanya tathmini. Hii
inatuepusha na maumivu mengi yasiyo na sababu.
4.
Mungu anatenda miujiza anapoona hakuna uwezekano kibinadamu
Yoshua 5:12 “Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake,
baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana
tena; lakini wakala katika viliwa vya nchi ya Kanaani mwaka huo.”
Mungu hatendi miujiza kama
mazingaumbwe. Anakuwa na sababu. Kwa mfano, wana wa Israeli walipewa mana
jangwani kwa vile hapakuwa na uwezekano wa kulima mazao wakiwa safarini. Lakini
Mungu alipoona wanaweza kujilimia na kuvuna, hakuwapa tena mana. Jifunze
kufanya yote unayoweza kufanya kwa nguvu zako na kumuachia Mungu kwa lile tu
ambalo liko juu ya uwezo wako aliokujalia.
Marko 6:47,48 “Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa
katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika
kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu
ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita.”
Bwana Yesu alitembea juu ya maji kwa vile wakati wanafunzi wakipambana na
dhoruba baharini Yeye alikuwa nchi kavu. Haikuwepo mashua nyingine ya
kumfikisha pale walipo. Hapo ndipo akatumia uwezo wake wa Kiungu ambao
hauhitaji mashua za kibinadamu.
Kuna watu wanaaibika kwa vile
wanasubiri miujiza hata kwa mambo ambayo Mungu amewapa uwezo wa kuyafanya.
Maombi
ya wiki hii:
1. Ee Mungu naomba unifundishe
jinsi ya kushirikisha maono yangu kwa watu sahihi ili nisikwame.
2. Ee Mungu naomba unifundishe
kuwa na mpangilio wa shughuli zangu nijue naanza na lipi na kumaliza na lipi
ili nisijilaumu wala kukulaumu ninaposhindwa.
3. Ee Mungu naomba uniwezeshe
kutambua wakati muafaka wa kufanya kila jambo ili nisipate hasara
zinazoepukika.
4. Ee Mungu naomba unisaidie
nijitambue ili nisikungoje kwa mambo ambayo ulishanipa uwezo wa kuyafanya.
Kumbuka ku-follow kurasa zetu na
kujiunga na makundi yetu ili uendelee kupata mafundisho ya kukua katika neema
ya Mungu na kushinda changamoto za maisha.
Lawi
Mshana, 0712-924234


