Ticker

6/recent/ticker-posts

Kipindi cha Maswali na Majibu kuhusu Utoaji kinaendelea (Swali la 3 na 4)


Kipindi cha Maswali na Majibu kuhusu Utoaji kinaendelea (nimejibu swali namba 1 na 2 katika Makala zilizopita. Sasa ni swali namba 3 na 4)

Swali la 3. Kama nimetumia laki 1 kununua mfugo halafu akakua na nikamuuza kwa laki 3, natoa zaka shilingi ngapi?

Hatukuagizwa kutoa zaka ya mti bali ya matunda. Mambo ya Walawi 27:30 “Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana.” Kwa hiyo unatakiwa kutoa zaka ya shilingi laki 2 ambayo ni shilingi elfu 20. Hata hivyo tunatarajia kwamba una tabia ya kutoa zaka. Hivyo, pesa uliyotumia kununulia mfugo wako ilibaki baada ya kutoa zaka au pengine ni mkopo. Mkopo sio mali yako. Lakini pia zaka ni kiwango cha chini (minimum). Unaweza kutoa zaka ya shilingi laki 3 unapojisikia kumuamini Mungu. Ukipiga mahesabu ya sadaka walizotoa Waisraeli katika kipindi cha Biblia zilifikia takriban asilimia 70 ya kipato chao na bado hawakupungukiwa. Walipumzisha mashamba mwaka wa saba na bado hawakuwa ombaomba. Hivyo tusitoe zaka kama sheria. Kuna mwaka fulani muumini wa Kanisa ninalochunga alipata msukumo wa kutoa asilimia 20 badala ya asilimia 10 kama zaka kwa Bwana. Baraka zetu hazipo katika uwingi wa mali bali katika utii na upendo kwa Mungu wetu anayetulinda na kutuepusha na majanga mengi ya maisha.  

Swali la 4. Nikiokoka natakiwa kutoa zaka ya mali nilizokuwa nazo kabla sijaokoka?

Ni kweli tunatakiwa kutoa zaka ya vitu vyote. Kuna watu wanadhani wanatakiwa kutoa zaka ya pesa peke yake. Wakipewa zawadi za vitu kama nguo au vyakula hawatoi zaka yake. Vitu vinatolewa zaka kwa kujua thamani yake na kisha kutoa asilimia 10. Kama vitu hivyo viko kumi ni rahisi kutoa kimoja kama zaka (sehemu ya kumi) na kama havigawanyiki unathaminisha na kutoa sehemu yake ya kumi (10%).

Hatudaiwi zaka kabla ya kuokoka. Kumbuka kabla ya kuokoka mtu anakuwa hajaandikwa au kusajiliwa jina lake katika Kitabu cha Uzima cha Mwanakondoo. Ila kama mtu ana vitu vya wizi anatakiwa kuviondoa nyumbani kwake. Ezekieli 22:26 “Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao.” Haiwezekani kuvitakasa vitu vichafu. Damu ya Yesu inatakasa vitu vilivyochafuka lakini haitakasi uchafu. Huwezi kutakasa kinyesi ila unaweza kutakasa chombo kilichochafuliwa. Mdo 19:19 “Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.”

Dr. Lawi Mshana, 0712924234; mshanalawi@gmail.com