Ticker

6/recent/ticker-posts

BAADA YA KUMUOMBA MUNGU FANYA UNALOWEZA KIBINADAMU USIJE UKAAIBIKA (Jipatie Kitabu-pepe)

Mbinu za Kiroho na Kiuchumi za Kushinda Utegemezi na Umasikini (Ebook)

BAADA YA KUMUOMBA MUNGU FANYA UNALOWEZA KIBINADAMU USIJE UKAAIBIKA

Watu wengine wamemkufuru Mungu na wengine kufilisika kwa vile baada ya kumuomba Mungu waliamua kukunja mikono na kumuachia. Wanasahau kwamba mara nyingi Mungu hatufanyii mambo tunayoweza bali anatutia nguvu (anatupa uwezo wa kutenda). Fil 4:13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Mungu alikusudia Roho Mtakatifu atupe uwezo wa kutenda mambo tusiyoweza kibinadamu (divine empowerment) Luka 24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.” Pia Mungu anatenda kazi KWA KUSHIRIKIANA NASI. Mbele za Mungu sisi ni watendakazi wenza (co-workers). 1 Kor 3:9 “Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.”

1. Unapopata maono au unabii fanya maandalizi unayoyaweza kibinadamu.

Andiko: Mdo 11:27–30 “…27 Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia. 28 Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio. 29 Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi. 30 Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.”

Jambo la kujifunza:

Walipojulishwa kwamba njaa kubwa itatokea, hawakufunga na kuomba ili kukemea hali hiyo tu. Walijipanga na kuchukua hatua ya kuwasaidia ndugu zao na kuweka utaratibu wa namna ya kuwafikishia msaada walio katika uhatarishi zaidi (kukusanya, kutuma na kugawa).

Swali la kujiuliza: Mara ngapi ulipopata maono usiyoyapenda ulifanya maandalizi yoyote zaidi ya kuomba na kumuachia Mungu? Unadhani Mungu alipompa Yusufu maono ya kukimbilia Misri ili mtoto Yesu asiuawe, alishindwa kumuua Herode?

2. Muombe Mungu utambue jinsi ya kutumia raslimali zinazokuzunguka ili kutimiza mahitaji yako 

Nehemia 2:4,8Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni. …..nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu.”.

Jambo la kujifunza

Nehemia, mateka wa Kiyahudi huko Babeli, alikuwa amepandishwa cheo katika ikulu ya mfalme. Pamoja na kumuomba Mungu alitambua namna ya kupata raslimali kupitia kwa bosi wake kv kibali cha safari na kupata mbao za ujenzi wa ukuta.

Swali la kujiuliza: Mara ngapi ukimuomba Mungu anakufungua macho ujue nani wana funguo za maisha yako na kujua namna bora ya kuwashirikisha? Watu wangapi mnafahamiana au wanakuzunguka lakini hujajua nafasi yao katika kurahisisha au kuboresha maisha yako?

3. Punguza athari mbaya za maisha yako kwa kujali ubora na uimara wa msingi wa maisha yako

Mt 7:24-27 “24 Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; 25 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. 26 Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; 27 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

Jambo la kujifunza

Kama mtu hana akili anaweza kuomba ulinzi wa Mungu lakini hachukui tahadhari zozote za kibinadamu. Hata kama u mwombaji kama hujali ubora na usalama wako unaitwa mpumbavu.

Swali la kujiuliza: Mara ngapi umeombea vitu ambavyo ulitakiwa uvifanyie kazi wewe mwenyewe? Mfano, ukuta wa nyumba yako umepinda ila wewe unaamua kuupiga plasta na kuulazimisha uonekane kwamba umenyooka.

4. Tumia vizuri msimu wa neema kwa ajili ya vipindi vyenye changamoto.

Mwanzo 41:28-37 “28 Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. 29 Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. 30 Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. 31 Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. 32 Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. 33 Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. 34 Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. 35 Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, akaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. 36 Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. 37 Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote.

Jambo la kujifunza

Yusufu hakumwambia mfalme atangaze maombi ya kufunga nchi nzima ili njaa isije ikatokea. Alitoa mkakati wa kutumia vizuri kipindi cha neema kwa ajili ya kukabiliana na kipindi cha njaa kali.

Swali la kujiuliza: Umejiandaeje na dharura za maisha? Unapofanikiwa unawaza kiasi gani kuhusu dharura za maisha kwa siku zijazo kv kifo, njaa, kukosa kazi, uzee, magonjwa ya mlipuko nk. Ugonjwa wa UVIKO-19 ambao ungesababisha au ulisababisha kushindwa kuingiza kipato kwa muda, umebadilisha mfumo wako wa maisha kiasi gani? Unaendelea kuchangia pesa nyingi kwenye sherehe wakati huna akiba yoyote uliyoweka mahali salama?

Wewe unatakiwa kujifunza kwa wadudu maana wamekuzidi: Mithali 6:6-8 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.”

Makala hizi zinapokusaidia usiache kutoa ushuhuda maana lengo ni kuona maisha yanabadilika!

Tangazo

Jipatie kitabu-pepe (Ebook) cha ‘Mbinu za Kiroho na Kiuchumi za Kushinda Utegemezi na Umasikini’ kwa Tsh 5,000 tu.

Hiki kitabu kina sura 10 za kukuwezesha kuishi katika uhuru wa kifedha kama kutumia imani kupata mafanikio, kushinda utegemezi (kuwa ombaomba), kushinda utumwa wa madeni, sababu za kushindwa kurejesha mikopo, jinsi ya kutambua raslimali ulizo nazo, kushughulikia mambo yanayohujumu mustakabali wa maisha yako, kukabiliana na roho zinazozuia maendeleo yako, kumtolea Mungu kama inavyotakiwa, kutokiuka kanuni za Mungu kuhusu mafanikio na kutambua visababishi vikuu vya kushindwa katika maisha.

 kitabu hiki kwenye simujanja (smartphone) kwa mfumo ambao macho hayaumii kabisa na unasogeza kama unavyosogeza kurasa za kitabu cha kawaida (Epub format).

Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (Simu na Whatsapp)