JIPE MOYO MAANA WEWE NI NABII WA MAISHA YAKO
Nilipata sauti hii katika maono: Jipe moyo ili mambo yako
yafanyike kama yalivyopangwa.
Utangulizi
1. Mungu yuko tayari wakati wote kukutendea mambo makuu lakini anategemea utayari wako. Mungu hafanyi kazi na mtu aliyekata tamaa na anayejilaani hata kama ni mwombaji kiasi gani. Luka 18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.” Jifunze kupuuza mambo mengine badala ya kuyawaza sana kana kwamba ni wewe tu unayekumbana na changamoto hapa duniani.
2. Unapojiona panzi wakati Mungu anakuona kama mtu wake wa thamani, unajitengenezea mazingira ya kutofika Kanani (ndoto) yako. Hesabu 13:33 “Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.” Hes 14:23 “hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona.”
3. Lazima ujifunze kuwa na mtazamo sahihi kuhusu Mungu. Usimlaumu Mungu kwa kunena kwako na hata kwa mawazo yako. Ayubu alipata jaribu zito lakini alijilinda sana asimuwazie Mungu vibaya. Ayubu 1:22 “Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.” Paulo alipogundua hali anayopitia imeruhusiwa na Mungu, aliipokea kwa furaha ingawa kibinadamu alikuwa haipendi. Kubaliana na mpango wa Mungu kwako kwa gharama yoyote. 2 Wakorintho 12:9 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”
4. Usisahau kwamba hapa duniani tu wasafiri na uraia wetu uko mbinguni. Usihangaike sana na mambo ya hapa duniani na kusahau umilele wako utakuwa wapi. 1 Petro 2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.” Wafilipi 3:20 “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo.”
Mifano ya Maandiko Matakatifu kuhusu faida ya KUJIPA MOYO:
1. Ukiwa na moyo mkuu, Mungu atashughulika na maadui zako na kukuokoa. Usipigane nao. Mungu mwenyewe atapigana nao kwa ajili yako.
Isaya 35:4 “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.” Yeremia 1:19 “Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.”
2. Ukijipa moyo unapokea msamaha na uponyaji kutoka kwa Bwana. Inawezekana Mungu ameshakusamehe lakini wewe mwenyewe umeshindwa kujisamehe. Usikubali hukumu anazokuletea shetani moyoni mwako kwamba huna thamani tena. Pokea msamaha wa Mungu ili iwe rahisi kupokea uponyaji wako.
Mathayo 9:2 “Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako.”
Mathayo 9:22 “Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.”
3. Ukijipa moyo, mashaka kuhusu Mungu wako yanaondoka. Usimtilie mashaka Mungu. Kuwa na uhakika na upendo wake kwako. Hajawahi kukuacha. Wewe ndiye mara nyingi unamuacha.
Mathayo 14:27 “Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.”
4. Ukijipa moyo, unakumbuka ushindi ambao Bwana alikupatia na kuupokea leo (ushindi wake unakuwa dhahiri kwako leo). Yesu hakumshinda tu shetani. Pia aliushinda ulimwengu. Hivyo ukimuishia anaweza kukuokoa na dunia hii mbovu isikusumbue. Hutahangaika na kazi zako mpaka unakosa muda na Mungu wako.
Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu.
Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”
Wagalatia 1:4 “ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe
na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu.”
5. Ukiwa na
moyo mkuu ndipo unaweza kuwafikisha watu katika hatima yao. Kazi yetu sio
kuhubiri, kuombea na kufundisha. Hizo ni njia tu za kusaidia tufikie lengo.
Lengo kuu ni kuwasaidia watu wafikie hatima zao walizopangiwa na Mungu. Lazima
tuwarithishe watu nchi yao ya maziwa na asali na sio kuwakusanya tu kila siku
ya ibada.
Yoshua 1:6 “Uwe hodari na
moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii
niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa.”
Hitimisho
Kwa hiyo acha kujikatia tamaa na kujiona kwamba ni wewe tu mwenye
shida duniani. Shetani anakufanya umuwazie Mungu kwa upumbavu maana anajua
hicho ni kikwazo kikubwa cha majibu ya maombi yako.
Nataka kukutia moyo kwamba, Wewe umembwa kwa namna ya ajabu sana.
U mzuri kwa mambo mengi ila watu wenye wivu wanaogopa tu kukuambia. Leo
katazame kwenye kioo (mirror) na yule mtu utakayemuona mtabirie mema na
mafanikio tele. Hutakosa mazuri yake na mafanikio yake. Hata kulala tu kwenye godoro
na kuwa na chandarua kiasi kwamba huumwi na mbu ni jambo kubwa la kumshukuru
Mungu.
Naomba ujumbe huu ukuinue viwango vingine na kuirudisha thamani yako iliyoibwa na shetani. Pokea majibu ya maombi haya katika Jina la uweza la Yesu Kristo!
NB: Tafadhali shirikisha jambo ulilojifunza, lililokugusa au unalohimizwa kufanya kupitia makala hii.
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (sms au
whatsapp), Korogwe, Tanga, Tanzania