MUNGU ALIKUWA ANAWAZA NINI ALIPOKULETA DUNIANI?
Sidhani kwamba Mungu ametuleta duniani ili tule na kunywa kisha atuchukue na kutupumzisha. Hawezi kufanya kazi ya hasara kiasi hicho. Lazima tujue wazo lake lilikuwa ni nini ili tuthamini kuwepo kwetu hapa na tuhakikishe tunatimiza kusudi lake.
Ninaposoma maandiko najifunza mambo ya msingi kama ifuatavyo:
Mwa 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
1. Mungu alipanga kupanua utawala wake usiwe mbinguni peke yake. Ndiyo sababu hata Adamu alipomkabidhi shetani utawala aliopewa na Mungu, Bwana Yesu alipokuja akahubiri kuhusu kuurudisha Ufalme wa Mungu. Mathayo 4:17 “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Kimsingi, Bwana Yesu alikuja kumpokonya shetani mamlaka na kuwapatia wale waliompokea na kumtii. Fil 29-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Bila Bwana Yesu kumseta shetani chini ya miguu yetu hakuna mtu anaweza kumkanyaga. Warumi 16:20 “Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. Amina.” Luka 10:19 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”
2. Mungu alipanga dunia iwe na raslimali mbalimbali ambazo haziwezi kujisimamia zenyewe kama vile wanyama. Lakini pia aliweka raslimali ambazo zitahitaji kuendelezwa ndipo zitakuwa na manufaa kwa mwanadamu. Mfano madini. Mungu hakumjengea Adamu nyumba wala barabara bali alimpa uwezo wa kubadili mazingira yake au kuumba ulimwengu wake. Mwa 2:11,12 “Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu; na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham.”
3. Mungu alipanga kumuumba mwanadamu ambaye atakuwa mtawala wa dunia – alipanga kumpa mwanadamu huyo uwezo na tabia fulani alizo nazo ili atawale kwa niaba yake. Hakukusudia huyo mwanadamu amuulize kila kitu ili amfanyie. Usipokuwa makini unaweza kumuomba Mungu akufanyie mambo fulani ambayo sio kazi yake bali amekupa wewe jukumu hilo.
Ndiyo maana kuna mambo kadhaa alimuachia Adamu ayafanye:
1. Mungu alimpa kazi ya kulima na kutunza bustani aliyoipanda Mwenyewe. Hapa tunajifunza kwamba kufanya kazi sio laana. Laana ni kula kwa jasho (kuteseka ndipo upate kipato).
Mwa 2:8,15 “Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.”
2. Mungu alimpa Adamu kazi ya kuwapa majina viumbe na akaheshimu majina aliyowapa
Mwa 2:19 “Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na
kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai,
jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake.”
3. Mungu alimuacha yeye mwenyewe aamue atamuitaje msaidizi aliyemuumba kwa ajili yake. Mungu hakumlazimisha Adamu amuoe Hawa. Adamu mwenyewe ndiye alimuita ‘mke wake.’ Mungu anakutengenezea mazingira halafu unafanya maamuzi mwenyewe na kuwa tayari kuwajibika kwa lolote litakalotokea.
Mwa 2:23 “Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.”
Sio mpango wa Mungu uishi hapa duniani kama kuku wala mnyama yeyote ambaye anafugwa tu ili siku moja achinjwe. 2 Petro 2:12 “Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao.”
Lazima utambue kazi ambayo Mungu alikusudia uifanye katika Ufalme wake hapa duniani. Hukuzaliwa kwa bahati na wala hujaletwa duniani ili tu ufanye mambo yako halafu badae uende mbinguni. Hebu jiulize utahitaji kupumzika mbinguni kwa sababu ulifanya kazi gani ya kuchosha na yenye thawabu kwa Mungu ukiwa dunian?
Ufu 14:13 “Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.”
Kumbuka ufalme wa Mungu una kazi nyingi sana hivyo usidhani ni kazi za kidini peke yake. Kama serikali za duniani zina idara nyingi, serikali ya Mungu ni zaidi. Hivyo lazima utambue kilichomsukuma Mungu akulete duniani. Huna sababu ya kujilinganisha na watu wengine wala kutafuta kujibadilisha. Jigundue na kujikubali hivyo ulivyo ili utende lile linalompendeza Mungu. Ndiyo sababu saini ya dole gumba lako haifanani na mtu yeyote duniani.
Mungu akusaidia kupitia ujumbe huu utambue ulivyoumbwa kwa jinsi ya ajabu na kukataa sababu zozote zinazokufanya ujione hupendezi au huna thamani. Hukuletwa duniani kumuabudu tu Mungu kwa vile mbinguni kuna viumbe wanamuabudu muda wote. Tambua kazi yako ya msingi anayotaka umfanyie.
Barikiwa.
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (sms au
whatsapp), Korogwe, Tanga, Tanzania