Kipindi cha Maswali na Majibu kuhusu Utoaji kinaendelea (nimejibu swali namba 1 hadi 4 katika Makala zilizopita. Sasa ni swali namba 5 hadi 7.
Swali
la 5. Kuna mtu amekuwa akiniombea na kunishauri kwa njia ya mtandao. Sasa
ameniambia nimtumie sadaka ya shukrani. Je, nimtumie?
Kama mtu huyo angekuwa ni mtaalamu wa ushauri nasaha
ambaye anahitaji kulipwa ada ya ushauri, hapo hakuna shida. Ni sawa na kumuona
wakili kwa ajili ya kesi yako ambaye unamlipa kwa huduma yake ya kitaalamu.
Huyu mtu anayekuombea na kukushauri kiroho kwa njia ya
mtandao, alipaswa kukujulisha tangu mwanzo kwamba anataka huduma yake ilipiwe.
Kimsingi anapokuambia umpe sadaka ya shukrani ana maana hii:
1. Anataka umlipe kwa huduma anayokupatia ingawa hapendi
kukutajia kiasi maalum cha kutoa kwa vile anaogopa kwamba ataonekana sio
mtumishi wa Mungu.
2. Anataka kuchukua nafasi ya Mungu katika maisha yako.
Mtu anapotoa sadaka ya shukrani, hampi mchungaji au kiongozi wa dini bali
anampa Mungu. Hata kama sadaka hiyo itatumiwa na kuhani, haina maana mtoaji amempa
kuhani. Matumizi ya sadaka yanasimamiwa kwa kanuni maalum za Neno la Mungu kwa
watumishi wake.
3. Hatambui kwamba wewe una kanisa na pia una kiongozi wa
kiroho anayekulea. Ingawa ukipata changamoto za maisha hataweza kukusaidia kwa
vile yuko mbali, hatambui taabu ya viongozi wako wanaukulea kiroho.
Nashauri viongozi tutafute njia za kuingiza kipato
zinazokubalika kwa vile hatujakatazwa kufanya kazi baada ya muda wa huduma zetu
za kiroho. Lakini tusitoze watu kwa huduma ambazo tumepewa bure na kukatazwa
kulipisha watu. Mathayo 10:8 “Pozeni
wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.”
Swali
la 6. Ni lazima nitoe malimbuko ya kila mazao ya shamba langu au naweza kutoa
ya shamba moja tu?
Kila shamba linahitaji baraka zake kwa vile changamoto
zake ni tofauti na pengine mazao yake pia ni tofauti. 2 Mambo ya Nyakati 31:5 “Mara ilipotangaa amri, wana wa Israeli
wakatoa kwa wingi malimbuko ya nafaka, na divai, na mafuta, na asali, na mazao
yote ya mashamba; na zaka za vitu vyote wakazileta nyingi.” Nehemia 10:35 “tena kuleta malimbuko ya ardhi yetu, na
malimbuko ya matunda yote ya miti ya namna zote, mwaka kwa mwaka, nyumbani kwa
Bwana.”
Kusudi la malimbuko ni KUKALISHA BARAKA KATIKA NYUMBA
YAKO. Ezekieli 44:30 “Na kitu cha kwanza cha malimbuko yote ya
vitu vyote, na kila toleo la kila kitu cha matoleo yenu, litakuwa la makuhani.
Tena mtampa kuhani sehemu ya kwanza ya unga mbichi,
ili kukalisha baraka juu ya nyumba yako.” Kumbuka unaweza kupata baraka
na zisikae (zisidumu) bali ziwe kama zinazopita tu. Unashika pesa nyingi
mkononi lakini hazikufanyii kitu cha maana katika maisha yako. Unatakiwa kutoa malimbuko ili baraka zako
zidumu.
Swali
la 7. Ni sawa kutoa sadaka kama mbegu katika madhabahu ya Mungu kwa mahitaji
maalum?
Wengi wetu tumezoea kutoa sadaka siku za ibada peke yake.
Hatujui kwamba sadaka ni njia ya kujiunganisha na madhabahu ya Mungu kila
unapoiendea kwa suala nyeti. Waabudu shetani wanajua sana kanuni hii kwa mungu
wao.
Lazima tujue kwamba madhabahu haina maana kama hakuna
SADAKA na KUHANI WA MADHABAHU HIYO. Kwa hiyo unapotoa sadaka kwenye kanisa
ambalo hujajiridhisha kwamba kuhani wake ni wa kweli, unahatarisha maisha yako.
Akiitumia sadaka yako vibaya lazima utapata madhara.
Kumbuka kuna wakati Mungu anatupa ‘mbegu’ na wakati
mwingine anatupa ‘mkate’. 2 Wakorintho 9:10 “Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa
mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu.” Mungu anapokupa mbegu anataka upande ili usife njaa msimu
ujao. Anapokupa mkate anakutia moyo ule vizuri kwa vile ulipanda msimu
uliopita. Maana yake ni kwamba sio wakati wote tunatakiwa kupanda mbegu. Wakati
mwingine tunafurahia mavuno ya upandaji wetu.
Kwa hiyo ni sawa kutoa sadaka kama mbegu kwa ajili ya hitaji maalum. Unaweza kufanya hivi kwa mtumishi ambaye ana funguo za baraka zako. Usiwe mwepesi kutoa sadaka kwa mtumishi ambaye hujui madhabahu yake ni ya aina gani. Kum 12:13,14 “Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo; bali katika mahali atakapopachagua Bwana katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo.”
Dr. Lawi Mshana, 0712-924234, Korogwe, Tanga