Ticker

6/recent/ticker-posts

UNAJUA USIPOTII AGIZO KUU, UTALAZIMISHWA KWA FIMBO? (Karibu Mission to Burundi)

 Mission to Burundi (Bofya hapa)

UNAJUA USIPOTII AGIZO KUU, UTALAZIMISHWA KWA FIMBO? (Usipotii Mdo 1:8, Mdo 8:1 itakupata!)

Wengi wetu tunafahamu AMRI KUU (Mt 22:36-39) na AGIZO KUU (Mt 28:19,20). Kiongozi katika familia anapokaribia kufa na kisha akawaita watoto wake kusema nao, maneno hayo ya mwisho yanapewa uzito mkubwa sana. Mtu anapoyakiuka sio tu kwamba anaweza kulaaniwa lakini pia anaweza kukosa baraka alizokuwa amekusudiwa. Hivyo AGIZO KUU ni agizo la mwisho la Bwana wetu Yesu kabla ya kurudi kwa Baba Yake mbinguni. Agizo hili linahitaji kuchukuliwa uzito wa kipekee sana bila kulichanganganya na tafsiri zetu za kidini na kimadhehebu.

Mt 28: 19,20 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

Unajua tusipotii Mdo 1:8 (agizo kuu), lazima Mdo 8:1 (adha kuu) itupate?

Mdo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Mdo 8:1 “Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.

Lakini Mdo 1:8 hasa ina maana gani? Je, Mdo 8:1?

1. Roho Mtakatifu atawajilia juu yenu kwa lengo maalum na sio kujifurahisha tu – MPOKEE NGUVU YA KUWAWEZESHA KUTENDA YASIYOWEZEKANA KIBINADAMU  (DUNAMIS)

2. Nguvu hiyo haitaishia wakati wa maombi, mahubiri au uimbaji ibadani bali itawafanya muwe tayari hata kufa (kuwa mashahidi). Ili mtu aweze kuwa ‘shahidi’ lazima Roho Mtakatifu amjilie JUU yake na sio kumpokea tu NDANI. Haitoshi kumpokea Roho ndani na kunena kwa lugha na kukemea mapepo. Lazima Roho AJE JUU YAKO (Isa 61:1) ndipo utaweza kuwafungua waliofungwa na kuwaweka huru mateka (waliofanywa misukule). Hapo huduma itakuwa na matokeo makubwa (impact) kwa wale uliotumwa kwao.

3. Huu utayari wa kufa ni zaidi ya kuandaa kampeni za Uinjilisti na Ushuhudiaji – kiasi gani tunahatarisha maisha yetu au kujinyima (kujitoa kisadaka) kwa ajili ya Bwana. Hatufanyi kazi ya Bwana kwa muda tunaotaka au kujisikia? Tunajisikia ‘ole’ tusipofanya kazi ya Bwana?

4. Je ni kweli Yerusalemu inawakilisha pale tulipo? Mbona hawa waliopewa huu ujumbe walitoka Galilaya na sio Uyahudi ambapo Yerusalemu ipo? Unaijua vizuri Yerusalemu yako?

5. Je Uyahudi ni katika kitongoji kanisa lenu lilipo? Je kuna huduma tunazotoa zinazogusa eneo pana zaidi ya nyumba zetu za ibada? Je ni lazima kila anayeguswa na huduma zetu ajiunge na kanisa letu? Katika hao tulio nao makanisani wangapi hata shida zao tumeshindwa kuzijua na kuzishughulikia?

6. Je kuna watu tunaowafikia mahali pengine ambapo hatuna maslahi yoyote ya kidini? Tumewahi kuwafikia watu maeneo ambayo hatuna matawi yetu? Wayahudi walikuwa hawachangamani na Wasamaria lakini bado waliagizwa kufika Samaria. Hivi kuna mahali ambapo watu hawawezi kuokolewa na Yesu? Tunaweza kubinafsisha wokovu kiasi hicho? Lazima tutoke katika mazingira tuliyozoea na tunayofurahia (comfort zone) bila kujali uwezo wetu wa kiuchumi!

7. Je tuna mpango (hata kama pesa hatuna) wa kufika mbali iwezekanavyo ili kutimiza agizo la HATA MWISHO WA NCHI? Je ni kweli hiki tunachokifanya kila siku katika maeneo yetu ndicho agizo kuu la Bwana Yesu? Hagai 1:5 “Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.”

Kanisa lilipofurahia bubujiko la Roho Mtakatifu na kusahau lengo lake (ENENDENI), ilibidi lilazimishwe kutawanyika kwa fimbo? Usipotumika kwa hiari katika wito uliopewa, Mungu atakutengenezea mazingira ya kukulazimisha. Anaweza kuumba samaki kwa ajili ya kukumeza ili akakutapike kule unakotakiwa kwenda (kama utatubu).  

Unadhani kwa nini fimbo haikuwagusa wote? Mitume hawakuguswa kwa sababu walikuwa mahali sahihi kwa wakati huo. Walitakiwa wasimamie utekelezaji wa umisheni wa dunia. Hivyo acha kusema, TUNATAKIWA… badala yake sema, NINATAKIWA…

Ninapoamua kuwafikia watu wa mataifa mengine nafanya hivyo kwa hofu ya Mungu ili nisije nikaadhibiwa. 1 Wakorintho 9:16 “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” Sisahau mwaka fulani niliamua kwenda nchi fulani kwa ajili ya umisheni. Tukaenda vijijini ambapo tuliandaliwa ugali na panya na nililala mahali ambapo nchini kwangu sijawahi kulala katika mazingira hayo.  

Karibu ushirikiane nami utume huu wa Burundi kwa kuchangia chochote ulicho nacho. Taabu yako haitakuwa bure katika Bwana. Utajiwekea akiba kwa ajili ya umilele wako. 1 Timotheo 6:19 “huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli.”

Natarajia kwenda kutia moyo makanisa na watumishi wa Mungu wa Burundi katika mwezi Oktoba 2024.

Tuma kwenye TigoPesa 0712-924234, Mpesa 0754-653217 au Akaunti yangu ya CRDB Bank

Jina la Akaunti: Lawi E. Mshana; Namba ya Akaunti: 0152219784300.

Ukituma nijulishe Jina lako na mahali ulipo ili nimshukuru Bwana kwa ajili yako ili akukumbuke zaidi.

Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania