Hivi karibuni
tulikuwa na kikao cha viongozi cha masaa takribani sita kwa ajili ya kujadili
taarifa ya kila mmoja ya miezi mitatu. – mafanikio, changamoto, mapendekezo nk.
Baadhi yetu tunakazia tu upatikanaji wa fedha na kusahau mikutano muhimu ya pamoja.
Madhara ya kutofanya vikao vya pamoja
ni:
1. Kiongozi
kuchoka na kudhoofika (burn-out). Inabidi kiongozi huyu afanye kila kazi hata
kwenda kulipia bili za maji wakati wasaidizi wapo. Musa alishauriwa na mkwe
wake kwamba akiendelea hivyo atadhoofika. Viongozi wa dini wanaongoza kwa kuwa
na msongo wa mawazo (stress) duniani kwa sababu ya kufanya kazi nyingi bila
sababu. Kutoka 18:18 “Huna budi utadhoofika
wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako;
huwezi wewe kulitenda peke yako.”
2. Kiongozi
anakosa muda wa kufanya mambo ya msingi. Mitume walijikuta wanaacha huduma ya
msingi ya MAOMBI na NENO majukumu yalipoongezeka. Ikabidi wawe wabunifu. Hapa ndipo
huduma za mashemasi zilianza. Matendo ya Mitume 6:3 “Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa
wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili.”
3. Kiongozi
anaweza kujaribiwa kuwa na matumizi yasiyo na utaratibu. Matokeo yake
uwajibikaji unakosekana. Anaagiza tu pesa zitolewe bila kupanga na wenzake.
Lakini pia ni rahisi kila mtu kujifanyia lililo jema machoni pake mwenyewe bila
kuangalia maslahi ya taasisi. Waamuzi 21:25 “Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya
yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe.”
4. Taasisi
haitakuwa na bajeti wala vipaumbele. Mambo mengi ya msingi yatasahaulika. Huwezi
kushangaa michango ikilenga eneo moja na kusahau maeneo mengine muhimu. Hakuna mgawanyo
mzuri wa raslimali fedha. Kinafanyika kile tu kilichokumbukwa leo. Utakuta kuna
watu wamesahaulika kulipwa posho zao kwa kisingizio kwamba hakuna pesa za
kutosha. Wakati huohuo fedha nyingi zimeelekezwa eneo moja.
5. Viongozi watakuwa
wanategemea utumishi wa dharura zaidi. Badala ya kujiandaa kukabiliana na
changamoto (kuwa ‘proactive’) watakuwa wanasubiri matatizo yatokee ndipo
wayatafutie ufumbuzi (wanakuwa ‘reactive’). Matokeo yake sadaka zinakuwa nyingi
kila ibada mpaka watu wanachoka na kuamua kuchenji sadaka zao. Watoaji ndio
wanasaidia mgawanyo wa sadaka kwa vile viongozi wanakuwa wameshindwa kujipanga.
6. Viongozi
hawawezi kuwa wabunifu na kujituma hasa kiongozi wao mkuu akiwa hayupo. Hawana mahali
pa kutoa maoni na mapendekezo na hawajui wanachotakiwa kufanya. Hutashangaa
kuona watu wameteuliwa kushika nyadhifa fulani lakini hawapewi majukumu maalum ya
kusimamia. Hawana kitu cha kumkabidhi mwingine pale wanapomaliza muda wao. Wanachokabidhi
ni cheo (title) tu lakini hakuna faili la kukabidhi linaloonyesha kazi
iliyofanyika na iliyobaki.
7. Hakuna
mipango, ripoti, tathmini wala maazimio. Viongozi wanaonekana katika kutoa
matangazo lakini hawahusiki katika kusimamia utekelezaji. Hakuna kumbukumbu
zozote zinazohifadhiwa na wala hajulikani mhusika wa ufuatiliaji ni nani kwa
kila eneo. Hili linasababisha watu wamuone kiongozi mkuu kwa kila hitaji. Anaweza
kudhani ana kibali wengi wanapomuona lakini wanamchosha na anasababisha vipawa
vya wengine visifanye kazi.
8. Taasisi
haiwezi kuwa na afya njema. Mtu mwenye afya anakuwa na mizania katika maeneo
yote. Kwa hiyo hatakiwi kula chakula cha aina moja kwa wingi na kusahau
vingine. Taasisi isiyo na afya inajali ukuaji wa aina moja hasa ule unaoonekana
kwa haraka. Kama ni kanisa linaweza kuwa na juhudi nyingi za ukuaji wa kiidadi
(numerical growth) na kusahau ukuaji wa kiroho (spiritual growth) na ukuaji wa
kifedha (financial growth). Matokeo yake idadi inaongezeka lakini wengi
hawamjui Mungu wala kumtumikia na wengi wanalala njaa na hilo halionekani kama
ni tatizo. Hakuna mafunzo wala mkakati wa kuinua watu kiuchumi ingawa mafunzo
ya utoaji yanatolewa zaidi.
Haya ni
machache kati ya mengi yanayotukumbusha kwamba uongozi ni mifupa (skeleton)
wakati ongezeko la watu ni nyama (flesh). Kila upande una umuhimu wake. Hebu
jiulize kama kimojawapo kitakuwa na mapungufu. Tunahitaji viongozi imara na
watu imara kama tunataka kufurahia maisha tele tuliyokusudiwa na Mungu.
Tusipojali
uongozi imara tutakuwa na watu wengi ambao wanaabudu au kutumika lakini wana
migogoro mingi ambayo haishughulikiwi. Wanajilazimisha kucheka na kutabasamu
lakini ndani wanalia.
SASA UNAWEZA KUNIANDIKIA MOJA KWA MOJA KUPITIA BLOG HII KWA AJILI YA KUULIZA SWALI AU KUTOA MAONI YAKO.
Dr. Lawi
Mshana, 0712-924234, Tanzania