USIHUKUMU WATUMISHI, USIJE UKAHUKUMIWA
Maono: Nimeona mtumishi ambaye anaombea watu ingawa
anatuhumiwa kwa tabia fulani mbaya. Alikuwa kwenye uwanja ambako anajiandaa
kuombea watu. Mahali hapo palikuwa jirani na nyumba ambapo kulikuwa na wanaume
na wanawake wanaosubiri kuniona ofisini. Akaniomba nimruhusu atangaze jambo
fulani kwao. Nikamruhusu. Kabla sijatoka ofisini ili niwajulishe, akawa
ameingia na anataka kuwatangazia. Watu wakaniambia, Mchungaji! hivi hujui huyu
mtu alivyo? Atatuambia nini huyu? Nikawauliza maswali haya: Hakuna watu hapa
ambao hawatoi zaka na wataenda motoni? Hakuna watu hapa ambao hawatoi malimbuko
na wataenda motoni? Hakuna watu hapa ambao hawafanyi uinjilisti na wataenda
motoni? Hakuna watu hapa wanalawiti wake zao na wataenda motoni? Niliposema
hivyo, wote wakanywea (wakanyamaza) na kumruhusu aongee nao. Kisha maono
yakaishia hapo.
Haya maono hayana maana kwamba tabia mbaya za watumishi
zipuuzwe. La hasha! Tunakumbushwa kwamba tusiingilie kazi ya Mungu ya kuhukumu.
Lakini pia sisi wenyewe tujihoji na kujikagua. Tusidhani dhambi fulani
tunazofanya ni ndogo kuliko za wengine.
Mathayo 7:1-5 “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”
Tunaposhuku au kuona kwamba mtumishi ana tabia ambayo haimpendezi Mungu tunapaswa kufanya yafuatayo:
1. Tukemee tabia yake mbaya bila kuichanganya na huduma yake. Mtu anaweza kuwa na huduma njema na bado aende motoni kwa vile hafanyii kazi tabia yake. Paulo aliwahi kusema kuwa mtu anaweza kuhubiri na bado akataliwe kama hajui kuutumikisha na kuutesa mwili wake. 1 Wakorintho 9:27 “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” Uhakika wa mhubiri kuingia mbinguni uko mikononi mwake mwenyewe. Kama anachotuambia leo kina ukweli tukifuate, kama ni uongo tukatae. Lakini tusikatae ukweli wa leo kwa vile tu jana alikosea. Ndiyo maana tumepewa kupambanua roho ili tujue kwa sasa ni roho ipi inasema na sisi. 1 Kor 14:29 “Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue.” Kuna wakati Mungu anamtumia hata wapagani. Mungu aliwahi kusema na Farao kuhusu shibe na njaa itakayotokea na ndoto hiyo ikatimia. Lakini pia Mungu akamtumia huyohuyo Farao kumuinua Yusufu kama Mungu alivyokuwa amesema naye. Wewe hujawahi kuona Mungu akimtumia daktari ambaye hana dini au mwenye tabia mbaya akanusuru maisha yako au ya ndugu yako?
2. Tuonye tukiwa na nia ya Kristo. 1 Wakorintho 2:16 “Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.” Tusiruhusu kutumiwa na shetani tunapoona makosa ya wengine. Shetani ni mjanja sana. Anaweza kukufanya umchukie mwenye dhambi badala ya kuichukia dhambi yake. Paulo aliwahi kuwatahadharisha Wakorintho kwamba wawe makini wasije wakashindwa kumsamehe mtu ambaye alitenda dhambi akatengwa na sasa amebadilika. Mara nyingi mtu akianguka dhambini, hata kama ametubu na Mungu akamsamehe, wengi wetu tunagoma kumsamehe. Huu ni ujanja wa shetani wa kupoteza wateule wengi. 2 Wakorintho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.” Pengine hata wewe kuna watu unaendelea kuwanyoshea kidole hadi leo ingawa inawezekana walishatubu na kusamehewa na Mungu. Isaya 58:9 “Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu.” Tunahitaji kuwa na nia ya Kristo aliyemchukulia mtu aliyemchoma mkuki na kumpigilia misumari kwamba hajui atendalo badala ya kumuona kwamba anafanya hivyo kwa makusudi. Lakini pia tujifunze kuona mazuri ya watu kama yapo. Ikibidi tusifie mazuri na hata kuyaiga na wakati huohuo tukikosoa na kukemea mabaya.
3. Tusisahau mapungufu yetu wakati tunapowaonya na kuwakemea wengine. Tunaweza kuwa na dhambi kubwa sirini kuliko wale ambao wanatenda dhambi zao hadharani. Kufanya kwako dhambi chumbani ndani ya ndoa hakukufanyi uwe salama kuliko yule anayejiuza barabarani! Ndoa inahitaji kuheshimiwa na malazi yawe safi (mtindo wa kulala uwe katika utakatifu). Mnaweza kuwa na cheti cha ndoa na bado siku ya hukumu mtahukumiwa kama wazinzi kwa vile malazi yenu chumbani ni machafu. Waebrania 13:4 “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” Huwezi kuona kibanzi (tatizo dogo) kwenye jicho la mwenzako wakati jicho lako mwenyewe lina boriti (tatizo kubwa zaidi). Anza na wewe!!!
4. Tusimhukumu mtumishi wa mwingine Warumi 14:4 “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.” Mara nyingi ukimuuliza mtumishi yeyote atakuambia anamtumikia Mungu. Kwa vile hajasema anakutumikia wewe, uwe makini ili isije ikawa Mungu amempa huduma tofauti na ya kwako ndiyo maana humuelewi. Kumbuka hakutumikii wewe na wala Mungu hajawahi kukuambia chochote kuhusu mtumishi huyo. Wewe unaruhusiwa KUONYA lakini hujapewa mamlaka ya KUHUKUMU. Usipende kujiingiza katika majukumu ya Mungu ambaye ndiye HAKIMU (MHUKUMU MWENYE HAKI). Warumi 12:19 “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.”
5. Jihoji kabla ya kuhukumu wengine. Kwa kawaida kabla ya kushiriki meza ya Bwana huwa tunapewa nafasi ya KUJIHOJI na sio KUHOJI MAISHA YA WENGINE. 1 Wakorintho 11:28 “Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.” Usipende kuwatupia mawe wale ambao dhambi zao zimejulikana wakati wewe mwenyewe unafanya yanayofanana na hayo. Yohana 8:7 “Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.” Bwana Yesu hakufanya hivyo ili kuitetea dhambi. La hasha. Alitaka kuhakikisha wanaomnyoshea kidole huyu mwanamke wanatambua pia dhambi zao na kujiona wanastahili pia hukumu. Pia alitaka kuwazuia kufanya kazi ya Mungu ya kuhukumu. Yn 8:4-11 “Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.”
Mungu atusaidie tusihukumu ili tusije tukahukumiwa. Lakini pia tusiache kuonyana na kuombeana. Isije ikawa watu tunaowasema vibaya hatujawahi kuwaombea hata mara moja ili watambue dhambi zao na kuzitubia. Waebrania 10:25 “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” Yakobo 5:16 “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.”
NB: Tafadhali shirikisha jambo ulilojifunza au unalohimizwa kufanya kupitia makala hii.
Dr. Lawi Mshana, 0712-924234, Korogwe,
Tanga, Tanzania