Mungu anapenda tumwabudu kwa hofu na kutetemeka
Kuabudu ni sifa ambayo Mungu peke yake anastahili. Neno ibada (WORSHIP) limetokana na neno la Kingereza cha zamani (Anglo-Saxon word) la WORTH-SHIP. Neno hili lina maana ya kutoa heshima anayostahili mtu fulani. Kinyume chake baadhi ya watu wanawaabudu hata viongozi wao, madhehebu yao na kazi zao badala ya Mungu ambaye amri ya kwanza na ya pili zinadhihirisha wazi kwamba hataki kushirikiana utukufu wake na mtu yeyote. Kutoka 20:3-5 “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao.”
Mungu (Elohim) hahitaji ibada kanisani tu wala kuabudiwa kwa kuimba peke yake bali katika maeneo yote ya maisha yetu. Adhabu ya kumchanganya Mungu na miungu mingine pamoja na kuabudu kazi yako, mumeo, mkeo, dhehebu lako, kiongozi wako wa dini nk ni kubwa sana – kipigo chake kinaweza kuendelea mpaka kizazi cha nne. Pengine hata wewe leo umepigika kwa sababu babu zako walitenda dhambi hii.
Tunahitaji hofu na kutetemeka katika maeneo gani?
1. Katika maisha yetu ya
kila siku
Kama kweli unamuogopa Mungu hutaangalia wanadamu
wanaokutazama. Hupaswi kuogopa kufumaniwa na wanadamu bali Mungu aonaye sirini.
Wafilipi 2:12 “Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.”
Inawezekana bado ni mtu wa kujificha viongozi wako au waumini wenzako wasikukute ukifanya jambo fulani. Ni wakati wa kujisimamia kama mtu atakayetoa hesabu peke yake mbele za Mungu. Wagalatia 6:5 “Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.”
Hata maneno unayoongea ambayo hayana maana yanahifadhiwa na malaika. Siku moja yatakuhukumu. Mathayo 12:36 “Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.” Badala ya kuwasema watu vibaya, washauri, waonye au waombee ili wajitambue na kumrudia Mungu.
2. Katika ofisi na kazi zetu
Mungu ameagiza katika Neno Lake kwamba tuwaheshimu mabosi na wakuu wetu kama kumtii Kristo. Kujifanya unamuabudu Mungu ibadani wakati huheshimu wakuu wako wa kazi ni dhambi mbele za Mungu.
Waefeso 6:5 “Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo.”
Hata katika huduma za kiroho unapaswa kuwaheshimu viongozi wako. Unawaheshimu kwa kutii maagizo wanayotoa. Wakihuzunika kwa ajili yako itakuwa laana kwako. Waebrania 13:17 “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.”
3. Katika utumishi wetu kwa Mungu
Tusimtumikie Bwana kwa mazoea. Tumtumikie kwa hofu na kutetemeka. Kama hujisikii kumuogopa Mungu, muombe akuonyeshe utukufu Wake. Ukisoma Isaya 5 utaona nabii akisema OLE WAO/WENU nyingi sana. Alipoona tu utukufu wa Mungu katika Isaya 6 akaanza kusema OLE WANGU. Utaendelea kuona dhambi za wengine mpaka pale utakapoona utukufu wa Mungu ndipo utaanza kuona dhambi zako mwenyewe. Kila ujumbe anaokupa Mungu unadhani ni kwa ajili ya watu wengine. Lakini kuna wakati Mungu anasema na wewe mwenyewe. Anza na wewe mwenyewe usije ukahubiri wengine na mwisho uwe mtu wa kukataliwa. 1 Wakorintho 9:27 “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”
Zaburi 2:11 “Mtumikieni Bwana kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka.”
4. Katika ibada yetu mbele za Mungu
Kama Mungu alitaka makuhani wavae mavazi maalum katika kazi ya kikuhani, hata leo anataka tuvae mavazi yenye heshima tunapomuabudu. Kuna nguo za nyumbani, za kulalia, za shamba au kazini nk. Utahukumiwa kwa kuvaa mavazi ya chumbani unapoenda kanisani. Mavazi yako yakimkosesha mtu utahukumiwa kwa dhambi ya kukosesha (Mt 18:6).
Kutoka 40:13 “Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani.”
Watu wa Mungu hawakuthubutu kwenda kumjengea Mungu madhabahu wakati wakiwa wamevaa fasheni na miungu ya kigeni. Na walipochukua tu hatua ya kuacha vyombo vya uzuri (makeup). Ezekieli 16:17 “Ezekieli 16:17 “Pia ulivitwaa vyombo vyako vya uzuri, vya dhahabu yangu na vya fedha yangu, nilivyokupa, ukajifanyia sanamu za wanaume, ukafanya mambo ya kikahaba pamoja nazo.” Mungu hapendi ukosoe uumbaji wake kwa pete, herein, bangili, kujichubua, kujipaka rangi nk. Unaweza kudharau hili lakini kuna siku utajuta kwamba ulipuuza Neno la Mungu utakapoteswa milele na milele. Lakini pia ukivaa miungu migeni unakosa kitu muhimu sana katika maisha yako – UTISHO WA MUNGU. Matokeo yake watu wabaya na mapepo yanakuwa na mlango wazi (access) ya kukufuata. Soma vizuri andiko linalofuata.
Mwa 35:1-4 “1 Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako. 2 Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu. 3 Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. 4 Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. 5 Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo.”
Mungu atusaidie tumuabudu Mungu kwa hofu na kutetemeka isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia. 1 Wakorintho 11:32 “Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia.”
Dkt. Lawi Mshana,
Freelance Facilitator & Public Speaker, +255-712924234, Tanzania