
JE, MKE ANAWEZA KUMSHUTUMU MUME WAKE KWAMBA ANAMBAKA?
Katika warsha mbalimbali za masuala ya Jinsia tumegundua kwamba hata katika jamii ya imani kuna watu wanatumia vibaya maandiko kwa faida zao binafsi. Wengi hasa wanaume walisema mke hawezi kumshutumu (kumsema) mume wake kwamba anambaka. Kumbuka kumshutumu sio kumshitaki polisi au mahakamani bali kumsema kwamba leo mwenzangu naona unanibaka! Wanawake nao walisema wanatimiza tu wajibu wao ili amani iwepo katika familia.
Wanaume walitoa sababu 2 na wanawake sababu 1:
1. Ni mke wangu hivyo
lazima anipe haki yangu kwa vile Biblia inasema, “Mume na ampe mkewe haki
yake.”
2. Nifanyeje kama
ananikatalia? Kuliko nitoke nje ya ndoa afadhali nimlazimishe?
3. Baadhi ya wanawake
walikiri kwamba wanapotakiwa kufanya tendo la ndoa wakati hawako tayari
wanakubali ili tu amani iwepo lakini si kwa utashi wao.
Napenda kuzungumzia hizi sababu zilizotolewa:
Sababu ya kwanza
Ni rahisi kulitafsiri andiko ambalo wanaume walilinukuu kwa namna ambayo ni tofauti na lilivyokusudiwa (out of context). Mwanaume aliyetoa sababu hii ana maana kwamba mke ni chombo cha kumfurahisha tu mwanaume bila kujali kama na yeye anafurahia au la. Hii haki ya Biblia sio ya ‘kudai kutimiziwa’ tu bali ni ya ‘kuvutia ili utimiziwe.’ Sio kusudi la Mungu kwamba tendo la ndoa liwe jambo la kujifurahisha kibinafsi na kulazimisha bila kujali upande wa pili. Kinyume chake Mungu anataka malengo yawe kiasi gani mume anamfurahisha na kumtosheleza mwenzi wake kama Mungu alivyokusudia. Ukimalizia andiko ambalo wanaume walilinukuu linasema hivi, “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.” (1 Kor 7:3,4). Hii ina maana kwamba mume anatakiwa pia kumpa mke wake haki yake. Kila mmoja anatakiwa kumkabidhi mwenzake mwili wake na sio kuendelea na ubinafsi wake.
Neno la Mungu linasema
amebarikiwa anayetoa kuliko anayepokea yaani anayewaza namna atakavyomfurahisha
mwenzake badala ya kuwaza tu namna atakavyojifurahisha. Mungu anataka kila
mmoja amuone mwenzake ni bora kuliko yeye mwenyewe. Mdo 20:35 “…… kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi
alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.” Fil 2:3 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala
kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora
kuliko nafsi yake.”
Sababu ya pili
Mtazamo kwamba
afadhali “nimbake” kuliko nitoke nje ya ndoa maana yake ni kwamba mtu huyu
anadhani ataepuka Jehanamu kwa kujizuia tu kuzini nje ya ndoa lakini hajui
kwamba anaweza kwenda motoni kwa kubaka mkewe ndani ya ndoa (kutokuiheshimu
ndoa yake kama Mungu alivyoagiza). Mungu hakusema ndoa zinakuwa takatifu kwa
kufungwa tu kanisani bali kwa kuziheshimu na kufanya tendo la ndoa kama
inavyotakiwa. Mtu anaweza kuhukumiwa kama mzinzi na mwasherati bila hata kutoka
nje ya ndoa yake. Waebrania 13:4 “Ndoa
na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na
wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” Kama mwenzako amechoka au anaumwa
lazima kumheshimu kama hiyo ndoa ni takatifu. Vinginevyo unaweza kujikuta
mmebaki tu na cheti cha ndoa sandukuni lakini mioyo iko mahali pengine.
Sababu ya tatu
Inaonyesha wanawake
wanatimiza tu wajibu wao katika tendo la ndoa kwa vile wanaume hawajali kwamba
na wao wafurahie. Hii inatokana na ukweli kwamba wapo wanaume ambao hawajui
kwamba wanaume wameumbwa tofauti na wanawake. Wanashangaa kuona kwamba wanawake
hawaonyeshi kutaka tendo la ndoa mara kwa mara kama wao. Mungu aliweka tofauti
hii ili kazi zingine pia zifanyike. Kwa hiyo usishangae kipaumbele kikuu cha mume
kikiwa tendo la ndoa (sex) wakati kipaumbele cha mke ni upendo au kuthaminiwa (affection).
CHANGAMOTO ZA NDOA
NYINGI ZA LEO:
1. Kuoa na kuolewa
bila kujali vigezo vya mwenzi wa maisha. Badala yake tunaangalia zaidi uwezo wa
kiuchumi na uzuri wa kuonyesha watu. Badala ya kuolewa au kuoa mwenzi wa maisha
wa kukupa MAHUSIANO BORA, unakuwa umetafuta mtu wa kukupa MTAJI, MIRADI na SIFA
KATIKA JAMII. Kwa hiyo mnajikuta mnaishi kama WAPANGAJI au WADAU na sio
WANANDOA.
2. Kushindwa kujua
tofauti za kimaumbile kati ya mwanaume na mwanamke. Mungu hakukusudia mke awe sawa
na mume bali akamilishane na mume wake. Asichokuwa nacho akipate kwa mumewe na mume apate
kwake kile asichokuwa nacho. 1 Wakorintho 7:3 “Mume
na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.” Watu wa aina hii lazima
WATAHITAJIANA (they will need each other) kwa vile WANAKAMILISHANA.
3. Kushindwa kujua
vizuri tendo la ndoa katika utakatifu kwa vile wengi walizoea zinaa kabla ya
kuoa na kuolewa. Kwa hiyo Mungu hapewi nafasi yake katika tendo la ndoa. Ndoa inahitaji kuheshimiwa na malazi (namnaya
kufanya tendo la ndoa) yawe safi. Waebrania 13:4 “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana
waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” Katika semina zangu nyingi nimegundua ni watu wachache sana wanaoombea tendo la ndoa.
Ila wakiandaa ugali mezani wanauombea. Hivyo mara nyingi mgeni rasmi kwenye
tendo la ndoa ni shetani badala ya Mungu. Matokeo yake shetani anahakikisha
wanandoa wanashindwa kufanya tendo waliloruhusiwa ili awapeleke kufanya lile
walilokatazwa.
4. Kutojua kwamba
tendo la ndoa sio upendo peke yake bali linakamilisha tu upendo. Katika ndoa
inatakiwa tendo la ndoa liwe ni kilele cha upendo (climax). Kama hakuna
maandalizi ya upendo haiwezekani wahusika kutoshelezana hivyo ni rahisi mtu
kuona anapotezewa muda wake. Upendo hauna ubinafsi (hautafuti mambo yake) hivyo
lazima utapenda kujua mwenzako anapenda nini na sio tu wewe unapata nini kutoka
kwake. 1 Kor 13:4,5 “Upendo huvumilia,
hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na
adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya.” Kama akija
mgeni nyumbani kwako humpi soda ya aina yoyote bali unamuuliza ili umpe huduma
bora. Katika ndoa pia usijione mjuaji sana bali muulize mwenzako anapenda nini
na hapendi nini. Hii itakusaidia umpatie huduma ambayo ni muhimu kwake badala
ya kukuvumilia tu. Tambua kwamba ndoa ni taasisi kubwa iliyoanzishwa na Mungu
mwenyewe, hivyo tuache mazoea na ubabaishaji!
Hata hivyo mke ana
wajibu wa kumsaidia mwanaume kwa vile wanaume tuna uwezo mdogo wa kuzisoma na
kuzielewa hisia za wanawake hasa pale wanaposhindwa kuzielezea kwa maneno. Ni
rahisi kudhani mume wako anafanya mambo fulani kwa makusudi na kumbe
hajakuelewa.
Mungu atusaidie na kuponya
mahusiano yetu.
Toa maoni yako au
uliza swali lolote hata la kibinafsi.
Dkt. Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker,
+255712924234, Tanzania