Ticker

6/recent/ticker-posts

MAMBO YANAYOSABABISHA UGUMU WA MAISHA KWA MTU WA MUNGU WAKATI WENZAKE WAKINEEMEKA

MAMBO YANAYOSABABISHA UGUMU WA MAISHA KWA MTU WA MUNGU WAKATI WENZAKE AU MAJIRANI ZAKE WAKINEEMEKA?

Kuna kipindi maisha yanakuwa magumu wakati watu wanaotuzunguka wanaofanya shughuli kama za kwetu wanaendelea kufanikiwa. Tatizo hili halipati ufumbuzi kwa vile wengi wetu badala ya KUJITATHMINI maisha yetu,TUNAJITETEA kwamba mafanikio ya wengine yanatokana na shetani. Hata kama shetani anafanikisha watu wake tusisahau kwamba shetani aliumbwa tu kama sisi na kwamba fedha na dhahabu ni mali ya BWANA na sio ya shetani. Hagai 2:8 “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi.” Kabla ya kuangalia makosa ya wengine ni vizuri tuangalie kwanza mapungufu yetu na kuyafanyia kazi. 

Hata hivyo usisahau kwamba hapa ninazungumzia UTAJIRI WA UTUKUFU na sio mafanikio yanayotokana na kutapeli watu, kupunja watu, kudhulumu watu, kukosa muda wa kumuabudu Mungu na kufanya maagano ya kishetani. Fil 4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.” Kol 1:27 “ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.” 

SABABU ZA UGUMU UNAOKUPATA WEWE WAKATI WENZAKO WANAFANIKIWA: 

1. Hupo mahali sahihi au hufanyi kazi yenye baraka zako 

Baraka za mtu ziko kwenye eneo alilowekwa au alipopewa na Bwana. MUNGU ANAKUPA NCHI KABLA YA KUKUPA BARAKA. Kum 28:8 “Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.” Mungu anaweza kukufanikisha kwa kukufungulia mlango mbele yako. Ufu 3:8 “Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.” Unadhani ingekuweje kama Eliya hangeenda karibu na kijito cha Kerithi wakati wa njaa? 1 Fal 17:2-6 “Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko. Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.” Mungu alikuwa ameandaa kunguru wa kumpelekea mkate na nyama hapo na sio mahali pengine. Kama kunguru anaweza kulazimishwa asile nyama bali akuletee, Mungu anaweza kumfanya mtu bahili na mgumu kukubariki hata kama hapendi. Lakini pia sio kila kazi ina baraka zako. Muombe Mungu usije ukafanya kazi ya mtu mwingine na kuacha ile yenye baraka zako. 

2. Umelaaniwa kwa kutotii sauti ya Mungu 

Laana ni “nguvu inayomfanya mtu ashindwe (to be empowered to fail).” Mtu aliyelaaniwa anaweza kukwama wakati wageni waliomkuta wanaofanya kazi kama ya kwake wanafanikiwa. Kum 28:43 “Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.” Sio tu kwamba mgeni anazidi kufanikiwa na wewe kubaki katika hali ya kawaida bali unashuka zaidi. Haya yanakukuta kwa vile kuna maagizo au wito umepewa na Mungu ukauacha na kufanya mambo yako tu. Kum 28:15 “Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.” 

3. Humng’ang’anii mwenye funguo za baraka zako 

Mungu anapotaka kubariki watu wake, anapitia mahali fulani au kwa mtu fulani. Tunapogundua mtu mwenye baraka zetu tunapaswa kujua jinsi ya kumtumia. Yakobo alimng’ang’ania malaika mwenye baraka zake mpaka akambariki. Mwa 32:24-29 “Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye. Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina lako n'nani? Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda. Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko.” Baraka hazipatikani kwa kuwekewa mikono peke yake. Yakobo alimng’ang’ania malaika mpaka akatenguliwa mguu. Kuna gharama yake na hata kuhatarisha maisha. Hata Isaka alitaka kumbariki mwanae baada ya kuhatarisha maisha katika uwindaji na kuandaa chakula kitakachomgusa moyo wake. Mwa 27:2-4 “Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa.” Unapohitaji baraka kutoka kwa mtu yeyote fanya utafiti anapenda nini na kumgusa kwa namna ambayo itamfanya akutamkie neno kutoka moyoni mwake. Vinginevyo, atakutamkia neno linalotokea kinywani mwake tu ambalo halitaleta matokeo unayotarajia. 

4. Hutoi zaka kamili 

Utoaji wa zaka (fungu la kumi) ni moja kati ya mambo ambayo wengi hawataki kuyasikia. Ila napenda ujue kwamba hakuna mtu aliyepewa msamaha kwamba hahitajiki kutoa zaka awe ni muumini, mchungaji au askofu. Yeyote anayekwepa lazima ataona madhara yake hata kama kwa nje anaonekana kama amebarikiwa. Na ni lazima iwe zaka kamili – Asilimia 10 ya mapato yako ya aina zote. Mal 3:9-12 “Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi. Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.” Wengi wamekuwa hawapati baraka za utoaji zaka kwa vile hawatoi zaka kamili, wanaichelewesha na kuna baraka nyingi wanazopata ambazo hawazitolei zaka. Matokeo ya kutokuwa mwaminifu katika eneo hili ni kukosa baraka za ki-Mungu, Mungu kutomkemea alaye (alaye ni pamoja na uliowakopesha wakagoma kurejesha, hasara katika biashara, majanga yanayosubiri upate pesa ndipo yatokee), kupata faida ndogo (mzabibu kupukutisha matunda kabla ya wakati wake) na kukosa mguso kwa jamii (huitwi mbarikiwa na wala hupendezi yaani, unasema umebarikiwa lakini maisha yako hayaakisi kile unachosema). 

Zaka imetajwa pia katika Agano Jipya tofauti na wapinzani wengi wanavyodhani kwamba ni utoaji wa Agano la Kale pekee. Ebr 7:8,9 “Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yu hai. Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi.” 

5. Umekosa upako wa Roho Mtakatifu au huutumii ipasavyo 

Mtu anaweza kukosa upako wa Roho Mtakatifu au kushindwa kuutumia upako alio nao. Ebr 1:9 “Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio.” Mtu anaweza kuwa na upako wa aina fulani na asiwe na upako wa eneo jingine. Lakini pia mtu anaweza kuwa na upako lakini hautumii. Mfano mtu anaweza kutumia upako wake kwenye kutoa mapepo tu na kushindwa kuutumia kwa ajili ya kushinda roho ya umasikini. Isaya 10:27 “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Upako unaweza kuharibu vifungo vya shetani ulivyo navyo na kuondoa mzigo mzito uliokulemea kwenye maisha yako. 

6. Umeuza haki yako ya mzaliwa wa kwanza 

Inawezekana umepuuzia nafasi yako kwenye familia yenu, kanisani kwenu na katika jamii yako. Changamoto za maisha zinaweza kukufanya upuuzie nafasi yako na kujikuta umemuachia mwingine baraka zako. Mwa 25:29-34 “Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.” Jihoji ulikuwa unamfanyia nini Mungu na sasa unafanya nini. Kama Mungu alikubariki kwa vile unahudumia nyumba ya mchungaji wako halafu ukaacha na mwingine akaanza kufanya huduma hiyo, unaweza kupoteza baraka zako. Ufu 3:11 “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.” Mungu anatubariki ili TUWE BARAKA KWA WENGINE na sio kutufanikisha kibinafsi tu. Mwa 12:2 “nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka.” 

7. Unampa Mungu mabaki badala ya sadaka 

Kimsingi sadaka ni kitu ambacho ni muhimu kwako lakini unaamua kumpa Mungu. Sadaka sio ziada au mabaki. Watu wengi hawajawahi kutoa sadaka katika maisha yao kwa vile hawajawahi kuamua kubadilisha mtindo wa maisha kwa kubana matumizi ili wamtolee Mungu. Ibrahimu alibarikiwa kwa vile alimpa Mungu mwanae pekee kama sadaka au kafara kwa Mungu. Mwanzo 22:16-18 “akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.” Tunaposema Mungu wa Ibrahimu atatubariki lazima tujihoji ni kwa namna gani tunafanana na baba yetu Ibrahimu. Kama tuna uchoyo na ubinafsi katika kumtolea Mungu hatuna sifa za kusema Ibrahimu ni baba yetu. 

8. Unapenda kusaidiwa wakati wewe mwenyewe hujali wengine 

Kuna watu wanalaumu sana wanapoona mtu ni tajiri lakini hawapi msaada. Lakini watu haohao hawajawahi kugusa maisha ya watu wengine kwa namna yoyote. Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.” Usimdhihaki Mungu lazima utavuna unachopanda. Gal 6:7-9 “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.” Kama ulivyowasahau wengine tena waliowahi kugusa maisha yako, ndivyo wenye baraka zako nao wanavyokusahau wewe pia. 

9. Umelogwa 

Unapopungua kiroho unaweza kulogwa wewe mwenyewe au shughuli zako. Utagundua umelogwa pale unapoona umeacha mambo mengi uliyokuwa unafanya kwa ajili ya Mungu. Gal 3:1-3 “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?” Shetani anaweza kuzuia au kuchelewesha majibu ya maombi kama hakudhibitiwa. Shetani alichelewesha maombi ya Danieli kwa siku 21. Danieli 10:13 “Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.” Pia shetani alizuia safari za mtume Paulo na wenzake. 1 The 2:18 “Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.” 

Unaweza ku-share ujumbe huu kwa wengine na kutoa maoni yako. 

Dr Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania