
TUNAWEZAJE
KUMTIA MOYO MCHUNGAJI NA FAMILIA YAKE? (Sura ya 5)
NB: Kumbuka kufuatilia muhtasari wa sura ya 1-4 kupitia kwenye Tovuti hiihii ili ujengwe. Ili kupata kwa urahisi angalia sehemu iliyoandikwa SEARCH halafu andika WACHUNGAJI ndipo itakuwa rahisi kuzipata mada hizo. Kwa sasa sipatikani Facebook.
Sura ya Tano (kwa muhtasari)
Tunawezaje Kumtia Moyo Mchungaji na Familia yake
Matendo haya ni ya muhimu sana baada ya kuwaombea wachungaji
na familia zao. Maombi yana sehemu yake kwa vile yanamfanya Mungu aingilie kati
kwa uwezo wake wa ajabu. Lakini sisi pia tumepewa wajibu katika utumishi huu.
Ndiyo maana Mungu alipowatenga Paulo na Barnaba kwa ajili ya kazi yake, bado
aliliambia kanisa nalo limtengee watu hao kwa kazi aliyowaitia (Mdo 13:2).
Mungu anafanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema (Rum 8:28).
1. Jitiishe katika mamlaka ya mchungaji na kuwahamasisha
wengine pia wafanye hivyo. Maombi peke yake kwa ajili yake hayatoshi. Kanisa
linapaswa pia kutii maagizo ya mchungaji wake. Muonyeshe mchungaji kwamba
unatambua kazi yake na kuithamini hata kwa kumlaki tu na kumpokea mfuko wake
anapoingia ibadani au kumsaidia kazi za ofisini kwake na nyumbani kwake. Mchungaji akikuhitaji kwa ajili ya huduma,
fika nusu saa kabla ya muda aliokuhitaji. Kwa kufanya hivyo utamfanya ajisikie
kwamba unamheshimu.
2. Onyesha ukarimu kwa mchungaji na familia yake kwa
kuwaalika nyumbani kwako kwa chakula na kuwashirikisha katika sikukuu muhimu za
familia. Unaweza kuwaandalia chakula na kuwajulisha mapema kwamba wasipike
nyumbani kwao kwa vile watakula nyumbani kwako. Ni vizuri zaidi kuwaalika wote,
yaani, mchungaji, mkewe na watoto. Tunapomwalika mchungaji na mkewe na kuwaacha
watoto wao, tunawafanya watoto wajisikie kutengwa na kujiona wao hawatambuliwi.
Tunaweza kuwaalika katika sherehe kama vile kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa
(birthday) ya mmojawapo katika familia zetu.
3. Mpe mchungaji na mkewe nafasi ya kuwa na faragha kwa
kuwasaidia kulea watoto au kumlipa mtu wa kuwasaidia kazi za nyumbani. Mara
nyingi mchungaji na mkewe wanatingwa na shughuli nyingi kiasi cha kukosa nafasi
ya kuwa pamoja katika utumishi. Mchungaji anatamani aingie katika maombi ya
kufunga pamoja na mkewe lakini mke ana majukumu mengi ya watoto ambayo
yanamfanya ashindwe kushirikiana naye. Kumbuka Biblia inasema, ‘Afadhali kuwa
wawili kuliko mmoja’ (Mhu 4:9). Mungu hakumpa mchungaji mke kwa ajili ya huduma
za nyumbani tu bali pia kwa ajili ya huduma za kiroho.
4. Andaa chakula na kuwapelekea pamoja na neno la kuwatia
moyo. Sio lazima wakati wote uikaribishe familia ya mchungaji nyumbani kwako
kwa chakula. Unaweza pia kuwaandalia chakula au kitu chochote kitakachowagusa
mioyo yao ili wajisikie kwamba wana watoto wanaowajali. Ingawa mchungaji anajua maandiko mengi, kuna
wakati anatamani kusikia neno la faraja kutoka hata kwa mtoto mchanga kiroho.
Mchungaji akiwa anaumwa hahitaji tu maombi bali anahitaji pia kadi za kumtakia
kupona haraka au ujumbe mfupi wa simu wa kumpa matumaini. Ukijua pia tarehe za
matukio muhimu katika nyumba ya mchungaji unaweza kuwapa hongera za kushtukiza
(surprise).
5. Chunguza kama kuna mahitaji katika nyumba ya mchungaji na
uyashughulikie mfano, bati linalovuja, kitasa kilichoharibika, bomba la maji
linalovuja nk. Unaweza kukuta mke wa mchungaji amevaa nguo iliyochanika lakini
watu hawaioni wala hawaoni kwamba wakimshonea nguo watakuwa wamefanya kazi ya
Mungu. Mchungaji anatiwa moyo akiona kwamba kuna watu wako tayari kufua na
kupiga pasi nguo za familia yake au za wageni wake bila kusubiri kuombwa
kufanya hivyo. Tusipoweza kuihudumia nyumba ya mchungaji tunayemuona, hatuwezi
kumhudumia Yesu (Mchungaji Mkuu) tusiyemuona kwa macho.
6. Shirikisha wenzako ili mgharamie safari ya maombi au
mapumziko (retreat) ya mchungaji na mwenzi wake. Wachungaji wengi hawana likizo
na matokeo yake wanazeeka kabla ya wakati wake. Mtu anayejitoa kugharamia
mapumziko ya mchungaji na mkewe lazima atabarikiwa kwa vile anawafanya wawe na
faragha ya utulivu inayowapa maono mapya ya kazi ya Mungu. Mchungaji pia
anaweza kujisikia kupumzika unapompunguzia majukumu kama vile kusomesha watoto
wake, kulipia kodi ya nyumba, kumnunulia chakula nk.
Kipindi kijacho utajifunza kuhusu MASWALI KWA AJILI YA MCHUNGAJI KUJIHOJI KIBINAFSI
Niandikie lolote kupitia sehemu ya (CONTACT US) WASILIANA NASI au COMMENTS (MAONI).
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (sms au
whatsapp), Korogwe, Tanga, Tanzania