Ticker

6/recent/ticker-posts

KWA NINI WANANDOA WANATOKA NJE HATA KAMA TENDO LA NDOA LIPO NDANI? (Click 'Translate button' for translation)

KWA NINI WANANDOA WANATOKA NJE HATA KAMA TENDO LA NDOA LIPO NDANI?
Napenda kukushirikisha mambo yanayosababisha watu wasiridhike na tendo la ndoa kwa wenzi wao. Sio mpango wa Mungu kwa wanandoa kuongozana barabarani na ibadani wakati kiuhalisia wamechokana na wanavumiliana tu. Mungu anataka watu wafurahie ndoa zao bila majuto wala kutishiana kuondoka. Kwa Wakristo tunaamini kwamba ndoa ikishafungwa hakuna wa kuitenganisha isipokuwa Mungu mwenyewe. Ndiyo sababu inafaa kuomba na kuwa makini kabla ya kuamua kufunga ndoa na mtu fulani. Lakini pia kama ndoa ina matatizo Mungu hashindwi kuiponya na kurejeza mahusiano yaliyovunjika. Kwa hiyo hakuna sababu yoyote inayokubalika kwa mtu kutoka nje ya ndoa yake. 
Hata hivyo nataka kukusaidia ugundue mambo yanayoweza kufanya tendo la ndoa lifanyike bila kuwa na mvuto na hivyo kumfanya MTU ASIYE NA HOFU YA MUNGU kutafuta njia nyingine mbadala. 
1. Kufanya tendo la ndoa wakati mmetofautiana au mmekwazana. 
Kiungo kikuu cha tendo la ndoa ni ubongo hivyo mnatakiwa kuwa na amani ndipo mtafurahia tendo la ndoa. Tendo la ndoa halianzishi upendo bali linakamilisha upendo. Hivyo ni vizuri kushughulikia tofauti zenu kwanza. Wengine hata katika tendo la ndoa wanaanza kukumbushana matatizo na kulaumiana jambo ambalo ni baya sana. 
2. Kutumia tendo la ndoa kama fimbo.
Mnaposhindwa kushughulikia mgogoro wenu na kusameheana ni rahisi mmojawapo kuamua kumuadhibu mwenzake kwa kumkatalia tendo la ndoa. Kwa vile mtu akikosa tendo la ndoa anakuwa na msongo wa mawazo na hasira, kinachotokea ni mahusiano katika maeneo mengine kufa pia. Njia hii ya mgomo imesababisha wengi kutafuta njia mbadala kv kutoka nje au kupiga punyeto/kujichua. Njia zote hizi zina madhara makubwa sana kiroho na kisaikolojia. 
3. Kufanya tendo la ndoa bila maandalizi ya awali na subira.
Ingawa madhara ya kutoandaliwa ni makubwa zaidi kwa mwanamke lakini pia hata mwanaume hataridhika vizuri hivyo ni rahisi kuhitaji tendo la ndoa mara kwa mara kupita kiasi. Mwanaume anayejali atamuandaa mwenzake vizuri na hatamaliza mapema bali atamsubiri ili wamalize wote wakiwa wametosheka. Nguvu nyingi zinapotea mwanaume anapofanya tendo hili mara kwa mara sana hasa ikiwa ulaji wake ni wa vyakula visivyo na virutubisho mwilini kama vile chipsi. Kutokana na nguvu kubwa inayotumika katika tendo la ndoa, hata kipindi cha Biblia mtu anayeenda vitani hakulala na mkewe. 
4. Uchafu na harufu mbaya
Kuna watu hawajali usafi wala kuoga. Wana tabia ya ‘kujimwagia maji’ badala ya ‘kuoga kwa kujisugua vizuri.’ Wengine hata wakioga hawabadili nguo wanavaa zilezile chafu. Wengine wanaoga na kuvaa vizuri kama tu wana safari. Tabia hii inawafanya hata watoto wamuulize mama au baba kwamba anakwenda wapi kwa vile hajawahi kumuona akivaa vizuri halafu abaki nyumbani. Tunatakiwa kukabili harufu ya kikwapa na kunuka mdomo. Mwenzako anaweza kuogopa kukuambia ili asikukwaze lakini hii ni sababu mojawapo ya kupoteza hamu na wewe. 
5. Chumba kutovutia
Hata kama hakuna anayeingia chumbani kwenu zaidi ya ninyi wenyewe lazima kitanda kitandikwe na chumba kivutie. Kama kitanda kimegeukia upande fulani kwa miaka mingi, mnaweza kukigeuza upande mwingine mwaka huu mpya ili kuleta mvuto mpya (kama chumba chenu kinaruhusu kufanya hivyo). Kama kitanda chenu ‘kinaimba’ mnapofanya tendo la ndoa, mnatakiwa mkiimarishe kwa misumari au kununua kingine. Hamuwezi kuwa na utulivu mtu akipita huko nje. Msiwekeze tu kwenye TV na simu, bali pia kwenye chumba chenu. 
6. Kutoshirikishana
Sio rahisi kujua hisia za mwenzako kama hakuna muda wa kushirikishana. Muulize anapenda nini na hapendi nini ili usibahatishe unapotaka kuugusa moyo wake. Usijione mjuaji sana wa maisha ya mwenzako. Unaweza kumfanyia jambo ambalo uliliona kwenye picha za ngono kumbe yeye linamkwaza sana ila tu anashindwa kukuambia. Mpe uhuru aseme anachofurahia. 
7. Kumbukumbu mbaya za zamani
Kama uliwahi kufanyiwa ukatili zamani kv kubakwa, unaweza kuwa na chuki kila unapokumbuka. Hivyo unatakiwa kuponywa kihisia ili usione kama unafanyiwa ukatili wakati wa tendo la ndoa. Lakini pia ili kuepuka kutafakari mambo ya zamani ni vizuri mfanye tendo la ndoa wakati kuna mwanga kiasi na sio gizani. Kwa mwanaume ni hatari zaidi kufanya tendo la ndoa gizani kwa vile wanaume wanavutiwa zaidi kwa kuona tofauti na wanawake ambao ni kwa kupewa maneno mazuri au kuonyeshwa hali ya kujali. 
8. Mmojawapo kukosa hamu mara nyingi
Kila mmoja ana haki ya kuanzisha tendo la ndoa. Ikiwa ni mmoja tu anayeonyesha kuhitaji mara kwa mara, anashindwa kuelewa kama mwenzake anamuhitaji au la. Anaweza kudhani anamlazimisha tu mwenzake. Hivyo akiona wengine wanaoonyesha kumuhitaji anaweza kusumbuka sana moyoni. Unapochukua muda kumtafakari mwenzako kwa mema anayokufanyia na kusahau kwa muda mabaya yake, lazima hisia za kumpenda zitakuja. Upendo unafunika wingi wa dhambi yaani, upendo unakufanya usihesabu makosa ya mwenzako. 
9. Kulogwa
Sio wote wanaofurahia kuwaona mnakaa vizuri kwa amani. Hivyo unaweza kulishwa limbwata ukaanza kumuona mtu mwingine ni mzuri kuliko mwenzi wako wa maisha. Kama mnamjua Mungu, mnahitaji maombi ya mara kwa mara kwa ajili ya ulinzi wa ndoa yenu. Maadui hawashindwi kumfanya mwenzako akose nguvu za kiume anapokuwa na wewe na awe na nguvu hizo akiwa na wao tu. Hawashindwi kumfanya mmojawapo amuone mwenzake ana sura mbaya kwa vile tu wamemvalisha kinyago usoni ingawa yeye mwenyewe hajui. Nimewahi kumuombea dada ambaye alikuwa hachumbiwi. Mapepo yaliyomvalisha sura bandia yalipotoka tu, alichumbiwa na watu watatu kwa wiki moja. Dada mwingine hakuchumbiwa na kaka yeyote wanayefanya naye kazi. Baada ya kuombewa na kufunguliwa, ndipo wafanyakazi wenzake wakaanza kuona uzuri wake. Mmoja akamwambia hivi sura yake ilikuwa wapi mpaka akatafuta mke mbali. Shetani anaweza kukupa sura mbaya ili usimvutie mwenzako. 
Yako mengi lakini ngoja nimalize kwa kusema kwamba jambo la msingi ni kujua kwamba ndoa haitakuwa nzuri kwa vile tu imefungwa kanisani. Inategemea mnajali kuilea kiasi gani. Hata nguo yako nzuri na ya thamani kama utaivaa kila siku bila kuifua, utaikimbia mwenyewe wakati fulani. 
Uko huru kuuliza swali lolote la kukusaidia upate furaha ya kweli. Siamini kwamba kuna ndoa ambayo haitengenezeki. Mungu ndiye muasisi wa ndoa zetu hivyo yuko tayari kuzirejeza na kuziponya. (Tumia sehemu iliyoandikwa WASILIANA NASI ili nikujibu kibinafsi kwenye baruapepe au email yako).

Mungu akubariki na kukukumbuka.

Dkt. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania