Ticker

6/recent/ticker-posts

Aina za mitaji

Je ni kweli kwamba wewe ni masikini kwa vile huna mtaji? – Dr Lawi Mshana

Mmoja wa wasomaji wa makala zangu aliwahi kuniuliza swali hili: “Mimi sina biashara yoyote hivyo naomba msaada wa mawazo ili niweze kufungua biashara na sina mtaji “ Kujibu hili swali kwa ukamilifu lazima mambo kadhaa yazungumziwe. Hata hivyo kwa sasa nitazungumzia zaidi kuhusu MTAJI kwa vile watu wengi wanapenda sana kusema hawana mtaji. Napenda tujue kwamba tunapozungumzia mtaji hatuzungumzii pesa peke yake. Zipo shughuli zinazohitaji mtaji wa pesa na ambazo hazihitaji mtaji wa pesa.

Aina za mitaji:

1. Mtaji wa fedha:

Huu ndio mtaji ambao unajulikana kwa wengi. Ni kweli mtaji huu una nafasi kubwa lakini sio mtaji pekee unaoweza kututoa. Wapo watu wenye pesa lakini wameshindwa kuyabadili maisha yao. Wapo maafisa wanaolipwa mishahara mara 8 zaidi kuliko walinzi au madereva wao lakini hawamiliki uchumi kama walinzi hao na madereva hao. Ukitaka ujue fedha sio kila kitu, safiri siku moja ujikute uko mahali ambapo hakuna duka wala hoteli. Utashangaa ukilala njaa na pesa yako mfukoni.

2. Mtaji wa vitu tunavyomiliki:

Huu ni mtaji wa vitu tulivyo navyo. Wengine wanaishi kwa shida na kutegemea mikopo ya riba wakati wana mtaji wa vitu. Mfano mtu ana mashamba 10 lakini anasema hana pesa za kununulia mabati ya nyumba yake. Angeliweza kuuza tu shamba moja na kupaua nyumba yake asiendelee kuvujiwa. Lakini pia kuna watu wana simu tatu na zote ni za laini mbilimbili. Simu hizo haziwaingizii chochote katika maisha lakini wanashindwa kuuza moja ili badae mambo yakikaa vizuri ndipo wanunue tena. Hakuna sababu ya kukaa na kitu cha thamani ambacho hakitumiki vizuri kwa sasa wakati kuna mahitaji mengine ya kuongeza kipato.

3. Mtaji wa vitu vya asili:

Mtaji huu unahusiana kwa karibu na wa mali tunazomiliki. Lakini huu ni wa vitu ambavyo tunavitegemea kwa ajili ya uhai wetu kv maji, hewa, mimea, wanyama nk. Mfano kuna watu wamezungukwa na mito lakini wameshindwa kulima kilimo cha umwagiliaji. Wengine mvua ikinyesha wanaitengenezea mifereji ya kuelekeza maji porini badala ya kuvuna maji hayo kwa ajili yao wenyewe. Wengine wamekimbilia mijini kubangaiza na kuacha mashamba yenye rutuba kijijini. Kama wanapenda sana mjini angalau msimu wa kilimo wangerudi kijijini kulima ili wanufaike na raslimali zao na mvua ya bure kutoka kwa Mungu ili angalau wawe na uhakika wa chakula.

4. Mtaji wa jamii:

Huu ni mtaji wa mahusiano na jamii. Ukiwa na mahusiano mazuri na jamii unaweza kuunganishwa na fursa mbalimbali ambazo hukuzijua awali. Kuwepo kwako tu kwenye mitandao kv facebook kunakuunganisha na fursa nyingi. Ni wajibu wako kutengeneza mtandao wa kuzifikia baraka zako. Usijidanganye huwezi kufanikiwa bila mahusiano imara na watu mbalimbali. Tunahitaji wateja wengi na wadau wengi ili tuweze kuendelea. Ukiwa na wivu huwezi kufikia malengo yako uliyojiwekea. Lazima ufurahie jamii nzima ikipata maendeleo. Kwa vile huwezi kuanzisha kila mradi unahitaji wengine nao waanzishe. Kama una hoteli, unahitaji mwingine afungue duka ili ununue bidhaa fulani kwake. Na yeye muda fulani aje kula chakula kwenye hoteli yako. Lakini pia wazo lako na ndoto yako inaweza kutimia ukiwa na mahusiano na wenye pesa. Mfano, umeona hitaji la mashine ya kusaga. Sio lazima uinunue wewe. Mwenye pesa ambaye hana muda anaweza kununua mashine hiyo na kufanya kazi na wewe. Ili mradi tu uaminike na utambue vizuri fursa. Jenga mahusiano yenye tija unapokutana na watu wenye neema mbalimbali.

5. Mtaji wa ujuzi:

Huu ni mtaji unaotokana na ujuzi ulio nao kupitia elimu na mafunzo uliyopata shuleni na chuoni. Kuna watu wamebadilisha maisha kwa vile wamewekeza kwenye mafunzo na kupata ujuzi na vyeti vinavyotambulika. Zipo kazi ambazo ni vigumu kuzipata hata kama utafunga na kuomba kwa vile hujazisomea mfano, kuwa rubani wa ndege au daktari. Vinginevo utahatarisha maisha yako na ya watu wengine. Tatizo la watu wengi wenye ujuzi ni fikra potofu kwamba watafanikiwa pale watakapoajiriwa. Hawako tayari kutengeneza kazi na ajira kwa kutumia ujuzi wao. Ujuzi sio kuongea kingereza kuliko watu wengine bali ni kuwa na uwezo wa kubadili mazingira yako kwa kutumia raslimali zilizopo na ujuzi ulio nao.

6. Mtaji wa uzoefu:

Huu ni mtaji unaotokana na uzoefu unaoupata kwa kufanya kazi na wenye ujuzi mbalimbali. Wapo saidia-fundi ambao leo wanapewa kazi za ujenzi wakati hawajawahi kwenda chuo cha ufundi. Wanapopata zabuni wanajitahidi kufanya kazi pamoja na wenye ujuzi rasmi ili kazi yao ikubalike zaidi. Kuna watu wanajua kompyuta leo na hawajawahi kukaa darasani na wamenufaika nayo kuliko wenye shahada za TEHAMA. Sio kazi zote zinahitaji kuonyesha cheti. Hebu jiulize lini ulipopelekea simu mbovu kwa fundisimu mwenye elimu ya msingi ulimuuliza kwanza cheti cha kutengeneza simu. Uliridhika na uzoefu wake na sifa ulizopewa na marafiki zako. Na inawezekana tayari maisha yake yako juu kiuchumi kuliko wewe mwenye vyeti vikubwa.

7. Mtaji wa utamaduni:

Huu ni mtaji unaopata katika jamii. Ni vigumu kubadilika sana kama unaishi kwa mazoea ya watu wanaokuzunguka wasiopenda maendeleo. Usiposafiri na kujifunza kwa wengine unaweza kuridhika na maisha yako ya chini ya kiwango. Lakini pia kama umebahatika kukaa kwenye utamaduni mzuri unaweza kufika mbali kuliko wenye kipato kama cha kwako lakini wanaishi utamaduni ambao wameridhika na maisha duni. Utabadilisha maisha yako kama unaishi mahali penye ushindani mzuri wa maendeleo. Ukiwa mgeni mahali ni rahisi kuona fursa ambazo wenyeji hawazioni kwa vile wamezoea maisha yao duni.

8. Mtaji wa kiroho:

Huu ni mtaji ambao upo kwa watu wanaomjua Mungu na kumsikia. Unapojitambua wewe ni nani na Mungu amekupa nini utaishi kwa kusudi la Mungu hivyo shetani atashindwa kukukwamisha katika mipango yako. Lakini kama humjui Mungu na hujitambui vizuri utakuwa fotokopi na kujikuta unajaribu kuishi maisha ya mtu mwingine. Utafanikiwa kama tu utaishi maisha yako halisi uliyopangiwa na Mungu. Lakini pia mtaji wa kiroho unakuwezesha kuvunja maagano na madhabahu za kiukoo zinazokwamisha maisha yenu. Vinginevyo utafanya kazi kwa bidii zote na kusoma mpaka shahada ya mwisho na kujikuta bado unaishi kama mtumwa katika nchi yako mwenyewe.

Mungu atusaidie ili tujitambue, tujue ametupa nini na tuweze kumiliki milki zetu.