KWA NINI WACHA MUNGU WENGI HATA WANAOTOA ZAKA NI MASIKINI?
Wapo wengi wanajiuliza maswali kwa nini pamoja na kumpenda sana Mungu na kumtumikia na ni waaminifu katika kutoa zaka (fungu la kumi) maisha yao bado ni duni.
Kwanza napenda ujue mambo kadhaa muhimu kuhusu utoaji zaka wenye tija:
1.
Toa zaka (10%) unapopokea tu mapato. Zaka ni sehemu ya kumi ya kwanza katika
mapato yako. Unapotumia kwanza mapato yako halafu mwisho ndipo unatoa zaka
unakuwa hujamheshimu Mungu hata kama umetoa kiwango kinachotakiwa. Mungu
hahitaji tu mali zako bali anataka umheshimu (umpe nafasi ya kwanza). Mithali
3:9 “Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.” Inafaa
kutoa zaka kabla ya kutoa matumizi yoyote ili Mungu alinde kile kilichobaki.
Tambua kwamba NI HERI KUWA NA SHILINGI 90 ILIYOBARIKIWA KULIKO KUWA NA
SHILINGI100 ILIYOLAANIWA!
2.
Toa zaka ya kila baraka unazopata. Kuna watu wanatoa zaka ya mshahara tu na
hawatoi ya baraka zingine. Kama unampenda Mungu unapopewa kitu unaweza kukithaminisha
na kutoa zaka yake. Mfano kama umezawadiwa vitenge 10 kwenye harusi unapaswa
kutoa kitenge kimoja kwa Mungu kama zaka. Vinginevyo unafunga milango ya baraka
za aina hiyo kujirudia. Mambo ya Walawi 27:30 “Tena zaka yote ya nchi, kama ni
mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana”.
Nehemia 13:12 “Ndipo Yuda wote walipoleta zaka za nafaka, na mvinyo, na mafuta,
kwenye hazina.”
3.
Toa zaka mahali sahihi. Mtolee Mungu mahali ambapo ni madhabahu yake na sio
katika madhabahu zilizozikwa vichwa vya watu. Kama zaka yako inaenda kwa miungu
mingine badala ya Mungu aliye hai usitegemee upenyo. Kum 12:11 “wakati huo
itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wenu, alikalishe jina
lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za
kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono
yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa Bwana.”
4.
Unapotingwa na kulazimika kuikopa zaka unatakiwa wakati unapoitoa uongeze
asilimia 20 (sehemu ya tano). Pengine umepata dharura ya ugonjwa au tatizo
lolote. Law 27:31 “Na kama mtu akitaka kukomboa cho chote cha zaka yake,
ataongeza sehemu yake ya tano juu yake.”
5. Toa zaka kamili bila kupunja. Mara nyingi wanaotoa zaka kubwa ni rahisi kupongezwa ingawa baadhi yao hawatoi zaka kamili ila ukilinganisha na wenye kipato kidogo wanaonekana ni waaminifu. Kutoa zaka sh 100,000 badala ya 115,000 ni wizi mbele za Mungu. Mungu anataka ZAKA KAMILI. Mal 3:10 “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.”
Sasa inawezekana uko vizuri katika utoaji wako wa zaka lakini bado maisha yako ni duni. Kumbuka zaka ni mali ya Mungu uliyo nayo. Ni kama kodi yako ya kuishi katika serikali ya Mungu (ufalme wa Mungu). Na pia ni kama kiasi cha fedha cha kuilinda akaunti yako isifungwe. Kwa hiyo kama utatoa zaka peke yake unaweza kukosa baraka zinazotokana na utoaji katika asilimia 90 ya kwako iliyobaki. Mtu ambaye hatoi zaka anafutwa katika uraia wa mbinguni na asiyetoa katika 90% iliyobaki hawezi kupata baraka kamilifu. Pia hupati thawabu yoyote kwa kuitumia zaka yako kumsaidia mtu kwa vile si wewe uliyempa bali ni Mungu mwenyewe amempa. Unapata thawabu pale unapotumia sehemu yako iliyobaki baada ya kutoa zaka, yaani 90%.
Tatizo la wengi lipo katika matumizi ya fedha walizobaki
nazo baada ya kutoa zaka. Pamoja na kwamba taifa la Israeli walikuwa na sadaka
za aina nyingi bado waliishi maisha ya baraka tele kuliko mataifa yaliyokuwa
hayamtolei Mungu. Baada ya kutoa zaka walimtolea Mungu kwa namna mbalimbali
kama ifuatavyo:
(i) Mwaka wa saba ilikuwa ni sabato ya shamba. Kwa kutii kupumzisha shamba (shughuli ya kipato) kwa mwaka mzima ilikuwa ni sawa na kumtolea Mungu 14.3%. Mwaka wa sita ulikuwa na baraka kubwa sana ili kufidia mwaka ambao mashamba yatapumzishwa (hakutakuwa na uzalishaji). Law 25:20,21 “Na kama mkisema, Je! Mwaka wa saba tutakula nini? Angalieni hatutapanda mbegu, wala kukusanya maongeo yetu; ndipo nitawaamria baraka yangu iwe juu yenu mwaka wa sita, nayo utazaa matunda hesabu ya miaka mitatu.”
(ii) Kila mwaka wa saba walisamehe madeni. Kuna sikukuu mojawapo ya pasaka nilitangaza kanisani kuhusu kusamehe ninaowadai wote na tangu nifanye hivyo nimezidi kubarikiwa. Kusamehe madeni ni njia pia ya kuonyesha kwa vitendo kwamba unatambua ukombozi wako ulivyomgharimu Mungu. Kum 15:1,12-15 “Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio. Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako. Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu; umwangalie kwa wema katika kundi lako, na sakafu yako ya nafaka, na kinu chako cha divai; mpe kama alivyokubarikia Bwana, Mungu wako. Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa Bwana, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo.”
(iii) Walisaidia masikini na wageni kwa mpango maalum na si kwa kusubiri masikini au mgeni aombe msaada. Law 19:9,10 “Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako; wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” Hata Bwana Yesu katika kipindi chake akiwa katika mwili alikuwa na mfuko wa kusaidia masikini. Yohana 13:29 Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu.
(iv) Mara tatu kila mwaka walikwenda Yerusalemu tena hawakwenda mikono mitupu. Pamoja na gharama za kusafiri na chakula bado hawakwenda bila sadaka. Wakati leo hii watu wengi wanaenda kanisani na sadaka kilema au bila sadaka kabisa. Kum 16:16 “Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu.”
(v) Walitoa sadaka za aina mbalimbali kv sadaka za unga, vinywaji, za amani na za dhambi. Ukisoma kwa wakati wako Law 1-5 utajionea mwenyewe jinsi walivyotoa sadaka nyingi.
Kwa hiyo kimsingi pamoja na kutoa zaka
(10%) ya mapato yao yote, ukijumlisha aina mbalimbali za utoaji nilizozitaja ni
kama walitoa 50% - 60% ya mapato yao. Kwa hiyo walibaki na takriban 40% hadi
30% kwa matumizi yao binafsi. Walifanya hivi kwa vile walikuwa na imani kwa
Mungu aliye hai. Matokeo yake mataifa mengine waliwaonea wivu jinsi
walivyobarikiwa. Ni kweli kwamba kuna aina ya sadaka hatuwezi kuzitoa tena
katika kipindi chetu kwa vile Bwana Yesu ameshachukua dhambi zetu msalabani.
Lakini nilichotaka ni kukuonyesha jinsi ambavyo walibaki na kisi kidogo kuliko
kile walichompa Mungu. Matokeo yake walilindwa na Bwana na kubarikiwa kwa kile
walichobaki nacho.
Watu wengi wanadhani watabarikiwa wakitimiza tu majukumu ya kutoa zaka na sadaka kanisani. Biblia imetuonyesha njia mbalimbali zingine za kusababisha mafanikio katika maisha yetu kiuchumi.
1. Wape watu vitu ili ukumbukwe. Luka
6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na
kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa
kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”
Watu wengi wamebaki kuomba wenzao waguswe kuwasaidia lakini wao wenyewe hawagusi maisha ya watu. Hakuna mtu ambaye hana mahitaji na hakuna mtu ambaye hana cha kutoa. Zamani mtu alipomuendea mtu amsaidie fedha angalau alimletea machungwa au mboga. Leo hii mtu akimtembelea ndugu au rafiki yake mwenye uwezo kuliko yeye anakwenda mikono mitupu na hachangii chochote hata kama atakaa mwezi mzima. Unaposhindwa kwenda na kitu angalau wape zawadi watoto siku ya kuondoka. Wekeza kwa watu ili siku moja wakukumbuke. Hata kama hawatakukumbuka wote uliowahi kuwasaidia, wapo watakaokumbuka ukarimu wako. Na kama hawatakukumbuka uliowasaidia moja kwa moja, Mungu atagusa wengine wakujali. Sina maana iwe kama sheria kwamba lazima ukienda kwa mtu uende na kitu. Nakumbusha tu ufanye kitu pale unapoweza. Kumbuka watu muhimu katika maisha yako ili watamke baraka juu yako. Mfano, daktari aliyetumiwa kunusuru maisha yako au ya mwanao, mwalimu aliyekusaidia sana ukapenda shule, mtu aliyewahi kukukopesha mtaji, mtu aliyewahi kukusaidia mchakato wako wa kuoa au kuolewa, mtu aliyekuunganisha na wenye baraka zako nk (PALE UNAPOKUWA UMEBARIKIWA USIMTEMBELEE RASMI UKIWA MIKONO MITUPU). Mwaka fulani nilienda Dodoma kufanya semina ya neno la Mungu. Ndugu fulani nisiyemjua ambaye alishiriki semina hiyo akawa ananipigia simu na kuniingizia vocha mara kwa mara kati ya sh 500 na 2000. Siku moja nikawa nasimamia ofisi fulani inayohitaji mhasibu. Nikasema hebu nimuulize huyu ndugu amesomea nini.Nikagundua amesomea uhasibu ila hana kazi. Nikamuita mara moja afanye kazi bila interview. Hakufanya hivi ili apate kazi kwa vile hakujua kama nina nafasi za ajira ila alitengeneza mahusiano yakaugusa moyo wangu. Siku nilipompokea wakati anashuka kwenye basi ndipo nilipomfahamu na akanieleza alivyonifahamu. Sasa wewe unayewabip watu na kuwatumia “tafadhali nipigie” kwa matatizo yako mwenyewe lini utakumbukwa maana unakuwa kero. Hata kama mtu ni tajiri sio wakati wote ana vocha (airtime) kwenye simu yake. Tena akikupigia wakati mwingine ungekata umpigie na kumwambia umejiunga kwa hiyo una muda wa kutosha wa maongezi. Hivi kuna mtu anathubutu kumbip daktari pale anapokuwa na mgonjwa? Wakati mwingine tuwabariki watu hata kwa vocha.
2.Unapokuwa na uwezo wekeza kwa watu kwa
ajili ya baadae. Lk 16:4-9 “Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika
uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.
Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza,
Wawiwani na bwana wangu? Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati
yako, keti upesi, andika hamsini. Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani?
Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.
Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa
wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa
nuru. Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili
itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele.”
Kuna watu wanadhani maisha yatakuwa
hivyohivyo siku zote za maisha yao. Kwa hiyo hawajali watu wengine pale
wanapokuwa na mafanikio. Wakili alipoona kazi yake inafikia mwisho alitengeneza
urafiki na wateja ili akiwa mtaani hana kazi wamkumbuke. Unapokuwa daktari
unaweza kupuuza wagonjwa kumbe mgonjwa unayempuuza ni afisa ardhi. Siku unaenda
kutafuta kiwanja unaona aibu mwenyewe.
Kuna mtu mmoja alikuwa na wadhifa mkubwa
zamani serikalini. Alikuwa anahusika na kuchagua majina ya wanafunzi
watakaoenda sekondari. Alichokuwa anafanya ikawa ni kuhakikisha watoto wa watu
asiowapenda anawafelisha. Aliwafanyia wengi hivyo na hakujua kuna siku
atastaafu. Siku moja wakati amestaafu alihitaji huduma muhimu sana katika ofisi
moja Dar. Alipofika akakutana na kijana aliyemfelisha. Mungu alikuwa amempa huyo
kijana njia nyingine ya kufikia ndoto zake. Ilikuwa kidogo huyu mzee apigishwe
push up. Na angepiga push up kwa jinsi ambavyo hitaji lake lilikuwa muhimu
sana. Hujui kesho yako itakuwaje na huwezi kujua mtu unayemnyanyasa atakuwa
nani kesho kutwa. Mtu baki anaweza kukusaidia kuliko mtoto wako uliyemsomesha
kwa gharama kubwa.
Lakini pia kuna msichana alikuwa anakwenda kutambulishwa kwa mchumba wake. Akiwa ndani ya basi akawa anamsukuma na kumtukana mzee ambaye hakuwa na siti kwa vile anamuangukia kwa kuchoka. Walipofika mwisho wa safari akashangaa kijana anampokea pamoja na yule mzee. Uso wake ukabadilika hapohapo akawa kama aliyemwagiwa maji. Kumbe alikuwa ni babamkwe. Wakafika nyumbani bila kuongea kwa uhuru njia nzima. Kutokana na yaliyotokea, alipewa tu nauli ya kurudi kwao na uchumba ukaishia hapo. Hata yeye mwenyewe alijiona hana sifa ya kuwa sehemu ya familia ile.
3. Jitolee kuliko kutafuta ajira na
kuomba pesa. 2 Kor 8:1-6 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu,
waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki
nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea
utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya
uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na
kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.
Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao
kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu. Hata tukamwonya Tito
kuwatimilizia neema hii kwenu kama vile yeye alivyotangulia kuianzisha.”
Watu wengi wakimaliza tu chuo wanapenda
kuzunguka kwenye maofisi kutafuta kazi. Na wengi wanalalamika kwamba hawapati
kazi kwa vile waajiri wanataka wenye uzoefu wa miaka mitatu hivi. Na wanaweza
kuzunguka na vyeti hivyo kwa miaka hata minne mpaka soli ya kiatu inaisha. Sasa
ngoja nikupe ushauri wa bure. Ni hasara kubwa kumfundisha mtu kazi na wakati
huohuo unamlipa mshahara na huna uhakika kwamba atafaa maana hakuna wa
kumuuliza (reference). Lakini pia ni ofisi chache sana zitamkataa mtu anayeomba
kujitolea kwa muda fulani kuwasaidia kazi hata kama halipwi. Kitendo cha
kujitolea kina faida nyingi sana. Kwanza unauza ujuzi na tabia yako ambayo
inaweza kuwavutia kukuajiri au kukupa nafasi ya kwanza pale mmojawapo
atakapoacha kazi au kuhamishwa au kupandishwa cheo. Pili wateja wanaotembelea
pale wanaweza kuulizia mtu mwenye sifa ulizo nazo kisha ukapata kazi. Tatu
mahali unapojitolea panaweza kutumiwa kama reference katika kuuliza utendaji
wako ukoje utakapoomba kazi mahali pengine. Nakuambia hivi kwa vile nimefanya kazi
nyingi za kujitolea kwa jamii, serikali, mashirika na watu binafsi na leo
nimeona matunda yake. Ngoja nikupe mfano wangu:
Mwaka fulani niliwaona watu kumi hivi wenye virusi vya UKIMWI wamekuja kwenye ofisi ya serikali ya mtaa kuomba msaada. Nikawachukua nyumbani na kuwaeleza jinsi ninavyotaka kukutana nao mara moja kwa mwezi. Wakati mwingine niliwapa tu gilasi ya maziwa na kuongea nao kwa upendo. Siku walipoulizwa na tume ya taifa ya kudhibiti UKIMWI kwamba ni nani anawasaidia wakanitaja. Ndipo nilipoweza kuomba ruzuku na kupewa fedha za kutoa mafunzo katika kata mojawapo ya Korogwe. Pia wao niliwaandikia andiko la mradi wakapata fedha za kuwasaidia. Baada ya kufanya vizuri katika mradi huo nikachaguliwa kuwakilisha mikoa miwili katika semina ambayo ni mara yangu ya kwanza kulipwa posho kubwa kiasi hicho kwa siku. Iliandaliwa na shirika la kimataifa jijini Dar. Leo hii mimi ni mlezi wa asasi za watu wanaoishi na VVU na nimewapa mahali pa vikao vyao bure na ninatoa mafunzo haya nikishirikiana na serikali na mashirika mengine.
Leo hii mashirika mengi yamekuwa yakitangaza nafasi za kujitolea na watu hawataki kwa vile hawatalipwa chochote. Hawajui hiyo ni interview pia ya aina yake (entry point). Sisemi haya kwa vile hata mimi nimekuwa nikifanya kazi na valantia (volunteers). Ila ukweli ni kwamba ni ngumu sana kumuacha mtu mwenye ujuzi anayejitolea pale nafasi ya kazi inapopatikana na kumchukua mtu ambaye hujui tabia yake wala uwezo wake bali ana cheti tu kikubwa. Nimewasaidia wanafunzi wengi wanaosoma computer application kupitia somo la stadi za maisha na baadhi wamepata kazi kwa wepesi.
Kuna watu wako tayari kuomba pesa badala ya kumuomba kupewa kazi yenye pesa. Hivi mtu anakuja kwako anakukuta unalimia nyumba yako halafu anakuomba uache kidogo ili aongee na wewe halafu anasema anaomba sh 20,000 utamuelewa kweli. Kwa nini asiseme mpendwa nipe kazi hiyo maana nina shida ya sh 20,000 au akusaidie kulimia nyumba ndipo baadaye aseme? Kwa nini hatujui hata kula na vipofu? Tuwe waungwana jamani. Haiwezekani mwenzako asulubike kufanya kazi halafu wewe akupe wakati ungeweza kumpunguzia uzito wa majukumu yake pia. Tuwahurumie pia watu wenye pesa kwa vile wanatumia muda mwingi na ujuzi mwingi kuzipata. Wengine wamesoma mpaka nywele zimenyonyoka na bado wanadamka asubuhi na kuchelewa kurudi jioni.
4. Toa sadaka katika madhabahu ya Bwana.
Law 6:9,13 “Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie,
Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale
motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu
utawaka juu yake usizimike. Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima;
usizimike.”
Madhabahu sio mahali pa kuhubiri na
kuimba kwaya na pambio tu. Nguvu ya madhabahu ni sadaka. Hata shetani anajua
ndio maana hamfanikishi mtu bila kutoa kafara kwake. Lakini wizi hauko kwenye
zaka tu bali hata kwenye sadaka. Malaki 3:8 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu?
Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani?
Mmeniibia zaka na dhabihu.” Mungu anataka ujue kiwango cha sadaka
kinacholingana na maisha yako na sio kutoa tu chochote kilichoko mfukoni. Kama
unajua bei ya daladala, kodi ya nyumba, bili ya umeme nk unatakiwa ujue kiwango
chako cha sadaka kwa kila ibada. Unapotoa sadaka kilema au mabaki unajilaani
mwenyewe. Sadaka ni kitu chenye thamani kwako unachoamua kumpa Mungu. Unatakiwa
pia kuwa na kiwango maalum cha chini (minimum) ambacho ni sadaka yako kila
unapokwenda kanisani. Hupaswi kutoa chochote kilichoko mfukoni. Kumbuka unaweza
pia kuwa mwizi wa sadaka na sio zaka tu. Mimi najua kiasi ninachotakiwa kutoa
kwa kila ibada. Kama nimesafiri na huko nilikoenda sikubahatika kushiriki
baadhi ya ibada, nikirudi natoa sadaka zangu za siku ambazo sikwenda kanisani.
Pengine unashangaa. Ngoja nikuulize swali. Hivi ukisafiri miezi miwili na
kufunga chumba chako ulichopanga ukirudi utalipa kodi ya watu? Kwa nini unalipa
na hukulala kwa miezi miwili? Basi kama utalipa, lipa na sadaka za Mungu ili
uwe salama. Najua umeiba kwa muda mrefu. Omba rehema kwa Mungu na kuanza
ukurasa mpya. Acha mazoea kwa vile Mungu anakujua sana na jinsi anavyokubariki.
Mwaka mpya ni siku ambayo tunamshukuru
Mungu kwa mambo aliyotutendea na kisha nawaombea watu wanaoahidi kuchangia
huduma ya kimisheni kila mwezi kwa mwaka mzima. Mwaka mpya fulani wakati wa
kutoa sadaka ya shukrani nilipotaka kutoa, nikakosa amani. Roho Mtakatifu
akaniambia moyoni haitoshi. Nikaongeza kiasi kama hicho na bado nikakosa amani.
Nilipoongeza kiasi kama kile mara ya tatu ndipo nikapata amani kisha nikamtolea
Mungu. Roho Mtakatifu ni mshauri wetu ili tusimkosee Mungu. Kimsingi alikuwa
ananiambia hivi kweli hiki kiasi unachotoa kinalingana na mambo makubwa
uliyotendewa na Mungu kwa mwaka mzima.
WAPENDWA, KUNA UWEZEKANO WA WACHA MUNGU KUTAJIRISHWA NA BWANA KAMA WALIVYOKUWA IBRAHIMU NA AYUBU HATA KAMA HATUNA KAZI, HATUJASOMA, HATUNA MITAJI, HATUNA UZOEFU NK. ILI MRADI TUMJUE MUNGU NA TUISHI KWA KUFUATA KANUNI ZA SERIKALI YAKE. NIMEWEZA KUFANYA MAMBO MENGI KWA KUMUENDEA MUNGU NA KUMNGOJA BILA KUMTEGEMEA MWANADAMU. TUTAMBUE MAISHA TULIYOPANGIWA NA MUNGU BADALA YA KUISHI MAISHA YA WATU WENGINE.
Ayubu 22:21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na
amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.”
Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania