Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini ninaota nikifunga ndoa na wapenzi wangu wa zamani? Nifanyeje nisiwaote?

Kwanini ninaota nikifunga ndoa na wapenzi wangu wa zamani ?  Nifanye nini ili nisiwaote? – Dr Lawi Mshana 

Kuna aina kuu tatu za ndoto: Ndoto kutoka kwa Mungu, za kibinadamu na za kishetani.

Kuota ndoto za kufunga ndoa na wapenzi wako wa zamani ni matokeo ya roho ya kibinadamu, roho ya shetani au Mungu anataka ujue jambo fulani.  Hata hivyo nitazungumzia sababu za kuota aina zote tatu za ndoto. 

(a)        Ndoto za Kibinadamu.

Mhu 5:3 “Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno.” 

1. Unaweza kumuota mtu kwa vile picha yake iko kwenye akili yako kwa sababu ya ukaribu ambao mmewahi kuwa nao, wewe na yeye. Unapokesha kwenye sherehe unaweza kesho yake kuota unakula kwenye sherehe. Hizi ni ndoto zinazotokana na shughuli nyingi.

2. Mpenzi anaweza kuchukua nafasi kubwa kwako kwa vile hujawahi kuona kasoro yake kwa sababu uhusiano wenu ulikuwa wa vipindi vifupi visivyo na nafasi kubwa ya kukwazana. Ni rahisi kudanganyika kwamba mtu ni wa maana sana kwa vile mnakutana kwa muda mfupi hivyo ni rahisi kwake kuificha tabia yake halisi (makucha yake).

3. Inawezekana ulitarajia au uliahidiwa kwamba uhusiano wenu kilele chake kitakuwa ni   ndoa na ukaamini hivyo. Hivyo ulimmeza kabisa moyoni. Hali hiyo inaweza kusababisha ndoto zinazomhusu zitokee.

(b) Ndoto za Kishetani

1. Shetani anapoanzisha uhusiano lazima alete ndoto chafu ili kuchafua maisha yako na kukufanya umkubali mtu huyo kama sehemu ya maisha yako. Yuda 1:8 “Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu.”

2. Shetani anatamani sana mcha Mungu aoe au aolewe na asiyeamini ili amdhoofishe  kiroho. Biblia ilikataza ndoa kati ya mwamini na asiyeamini. 2 Kor 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?” Mtu aliyeokoka ni mbegu takatifu ya Mungu ambayo haipaswi kujichanganya na wasiomjua Mungu. Ezra 9:2 “Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili.”

3. Baadhi ya wazinzi wanatumia uchawi katika kuwanasa au kuwavutia wapenzi wao. Hivyo inawezekana wakafunga ndoa na wewe katika ulimwengu wa roho kwa kupeleka vitu vyako kwenye madhabahu za shetani kv nguo, nywele nk. Lakini pia uhusiano mliokuwa nao mlitengeneza agano fulani la kuwafunga katika nafsi zenu (soul ties). Wakati mwingine mmekula kiapo na hamjawahi kuvunja kiapo hicho bali mliachana kienyeji tu. 1 Kor 6:16 “Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.”

4. Ni tabia ya shetani kuwatumainisha watu maneno ya uongo. Anataka uamini mambo ambayo hayawezi kutokea. Anataka kuvuruga mpango wa Mungu kwako kwa kukung’ang’aniza kwa mtu asiye sahihi ili kukupotezea muda.  Yer 7:4 “Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya.

(c) Ndoto za Ki-Mungu

Mungu anaweza kukuonyesha mawazo aliyo nayo mpenzi wako wa zamani ili umuepuke. Mungu anakupenda ndiyo maana anakuonyesha mipango ya maadui zako. Unaonyeshwa kazi za shetani zinazofanyika sirini katika ulimwengu wa roho ili ukemee. 2 Fal 6: 12 “Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala.”.

Ili  usiwaote:

1. Epuka uhusiano unaoweza kusababisha akuvuvie mawazo ya zinaa kama vile barua, meseji na simu za kimapenzi. Baadhi ya watu katika mitandao ni wachawi ambao kama uta-like picha yake atakuingiza (initiate) katika ufalme wake. Utaingiziwa tamaa ambayo itakuchanganya na kukufanya umfikirie na kushindwa hata kufanya kazi zako vizuri. Kumbuka roho ya kuchanganyikiwa (spirit of confusion) haitoki kwa Mungu (1 Kor 14:33). Hivyo unapompenda mtu kiasi cha kuchanganyikiwa akili umetekwa ufahamu.

2. Vunja maagano mliyofanya kinyume na mapenzi ya  Mungu kwa kuamua kuchoma moto barua zake, picha zake na zawadi zake zinazokusisimua mwili. Lakini pia futa maneno mliyoapishana kv Nikikuacha sitaolewa tena, sitapata mwingine ukiniacha, sitaweza kupenda mwingine kama wewe,  nk. Unaweza kuona kama ni maneno madogo lakini shetani anaweza kuyafuatilia. Pia kama kuna nguo alikupa na ukizivaa zinakupa madhara afadhali usizivae tena.

3. Mwombe Mungu aondoe mawazo ya zinaa na kupandikiza mawazo ya ki-Mungu  ndani yako. (Zab 19 : 14 “Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.”). Omba hii Zaburi mara kwa mara hasa unapolala ili hata unapoamka usingizini fikra zako zitawaliwe na Bwana. Kataa maneno na mawazo yasiyo na kibali kwa Mungu. Huwezi kufanya dhambi yoyote kama utaishinda katika mawazo. Shetani anacheza na fikra zako.

4. Muombe Mungu akupe kuchukia matendo ya mwili. Ujione kwamba kwa dhambi ulizozitenda ulikuwa ukimsulubisha Bwana Yesu msalabani. Gal 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi.” Ondoa programu (kama una kompyuta) au applications (kama una smartphone) au video chafu (kwenye simu/kompyuta) ili usijaribiwe kuendelea kutazama vitu vinavyokusajili kwenye ufalme wa shetani. Kama ni kompyuta unaweza kuiset ili unapojaribiwa kutaka kufungua picha za ngono kwenye mtandao ikatae kuzifungua. Kama hujui waone wataalamu wa kompyuta wakusaidie.

5. Tafakari ubaya wa wapenzi wako wa zamani ambao badala ya kutaka kukuoa walikuwa wanataka tu kuyachezea maisha yako. Ukigundua mapungufu yao, itakuwa rahisi kuwafuta katika mawazo yako na hatimaye ndoto zinazowahusu zitatoweka. Tatizo lako unakumbuka mazuri yao tu ndiyo maana unashindwa kuwaondoa kirahisi moyoni. Kumbuka kwamba “walikutamani” badala ya “kukupenda.” Mtu anayekutamani anawaza kufaidika na wewe (anawaza atapata nini kwako) na anayekupenda anawaza kukusaidia bila kupata kitu kwako. Usidanganyike na maneno ya mdomoni ya “ninakupenda” mara nyingi hayatoki moyoni. Kumbuka watu wanahitaji kupendwa na vitu vinahitaji kutumiwa na kamwe sio kinyume chake (Remember that people are to be loved and things are to be used. It is never the other way round.).

6. Kemea ndoto zote unazozipata ambazo zinapingana na Neno la Mungu. Mfano, kama unaonyeshwa kwamba unaolewa na mume wa mtu, ni wazi kwamba ndoto hiyo haiko katika mapenzi ya Mungu. Mwingine akionyeshwa mume wa mtu anaanza kuombea vibaya ndoa yake ili amuache mkewe au mkewe afe. Huu ni uchawi wa kimaombi (charismatic witchcraft) wa kulazimisha mambo yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu. Tuna waombaji wengi wachawi ambao wanaomba maneno ya shetani badala ya maneno ya Mungu. Hivi Mungu ameishiwa kiasi hicho? Anashindwa kukupa wa kwako ambaye hana agano na mtu mwingine? Hivi wewe utakapoolewa halafu ukasikia kuna mtu anaomba ufe ili naye aolewe utajisikiaje? Usimtendee mwenzako jambo ambalo wewe mwenyewe hutaki kutendewa.

7. Ungama kwa ajili ya mawazo potofu ambayo yamekuwa yakikutawala ili Bwana akusafishe na udhalimu wote (1 Yoh 1: 9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”). Kubali kwamba unamkosea Mungu kwa mawazo mabaya na ndoto mbaya unazopata. Hata kama huna uwezo wa kuzuia ndoto mbaya, kuna mlango uliufungua katika maisha yako. Pengine ulizini na mtu au jinni akachukua sehemu ya viungo vya mwili wako na kupeleka kwa shetani au ulienda kwa mganga wa kienyeji ili uteke waume za watu ukasajiliwa huko. Wapo mawakala wa shetani wanaotumwa kuzini na mtu ili tu wampelekee kitu fulani ili ukawasaidie kazi zao bila kujua au bila kupenda ikiwa ni pamoja na kuwazalia watoto watakaowatumia kuharibu maisha ya watu duniani. Lakini pia shetani anaweza kukupa kazi ya kuwaangusha watu katika dhambi bila kupenda hata kama hutaki dhambi hiyo.  

Napenda kukutia moyo kwamba Bwana anataka kukuponya wewe, familia yako, mji wako na nchi yako. 2 Nya 7 : 14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso na kuziacha njia zao mbaya, basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao na kuiponya nchi yao!

Huu si wakati wa kuendelea kuwa mshirika au msharika. Ni wakati wa kwenda hatua nyingine ya kuwa mwanafunzi wa Yesu. Mwanafunzi ni mtu anayeishi kwa malengo ya ki-Mungu na sio kuongeza idadi (namba) ya waumini ibadani. Kuwa pamoja na watu wengi kanisani hakukusaidii kama kibinafsi umepishana na Mungu katika maisha yako.

Chukua pia hatua ya kuombewa na mtumishi ambaye unajisikia amani na kibali moyoni na mwenye historia nzuri ili kinyago (mask) ulichovalishwa na shetani kiondoke. Vinginevyo utaendelea kuonekana tofauti na jinsi wewe mwenyewe ulivyo. Watu wanakuona unacheka na kutabasamu lakini ndani ya moyo unalia na maisha yamekuchosha.

Ubarikiwe na Bwana.