Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini baadhi ya watu wanalemewa na madeni yasiyolipika?

KWA NINI BAADHI YA WATU WANALEMEWA NA MADENI YASIYOLIPIKA 

Mtu anaweza kuwa na madeni kwa sababu zisizozuilika au sababu zinazozuilika. Sababu zisizozuilika ni kama kupata dharura za maisha kv magonjwa au misiba. Sababu zinazozuilika ni mtu kukopa vitenge halafu analipa zaidi ya gharama yake halisi mwezi ujao. Madeni hayapaswi kuwa mtindo wa maisha (lifestyle). Madeni yakiwa mtindo wa maisha mtu anakuwa MTUMWA WA MADENI. Na jambo la kushangaza katika kipindi chetu ni kwamba wenye kipato na uwezo mkubwa ndio wanaoongoza kwa madeni yasiyolipika kuliko wasio na uwezo. 

Biblia inasema nini kuhusu kukopa? 

1. Kuna nyakati mtu anaweza kuhitaji kukopa hivyo akopeshwe. Mt 5:42 “Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.” 
2. Anayekopa akubali kwamba anakuwa mtumwa wake akopeshaye. Yaani asijisahau akaendelea kuvaa vikali kwa kutumia pesa za watu. Mit 22:7 “Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.” 
3. Anayekopa awe mwaminifu kulipa deni la watu. Zab 37:21 “Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.” 

Kwa nini watu wengi wametawaliwa na madeni? 

 1. Si waaminifu kwa Mungu. 

Mal 3:10 “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.” Tunapokuwa hatutoi zaka kamili (tunapopunguza kiasi tunachotoa au kutoa zaka ya baadhi tu ya baraka zetu) na tunapokuwa hatutoi kwenye “ghala ya Mungu” (kutoa mahali ambapo sio sahihi) hatuwezi kuwa na baraka tulizokusudiwa. Usipunguze kiasi unachotakiwa kutoa zaka (10%). Afadhali uongeze kuliko kupunguza. Toa zaka kwa kila baraka unayopata kwa msaada wa Mungu. Acha kumtolea Mungu kama hukupata kwa njia halali. Mal 1:13 “Tena mwasema, Tazama, jambo hili linatuchokesha namna gani! Nanyi mmelidharau, asema Bwana wa majeshi; nanyi mmeleta kitu kilichopatikana kwa udhalimu, na kilema, na kilicho kigonjwa; ndivyo mnavyoleta sadaka; je! Niikubali hii mikononi mwenu? Asema Bwana.” Napenda kukuasa kwamba unapotoa zaka usione kama unampa kiongozi wa dini au taasisi ya dini, hutabarikiwa. Jione kwamba unampa Mungu. Ukiamua kuipangia matumizi zaka yako, unajiingiza kwenye huduma ya kikuhani (kazi za watu) jambo ambalo linaweza kukupa laana. Lakini pia ni laana kuendelea kupokea huduma za kiroho wakati hutoi zaka wala sadaka. Unaombewa na kupewa malezi ya kiroho halafu hutoi zaka wala sadaka! Kama unasema hupati huduma nilizotaja hapo ndiyo maana hutoi zaka, afadhali utafute mahali pengine utakapohudumiwa ili utoe zaka na sadaka zako hapo. Usiache kutoa zaka na sadaka wakati unaendelea kupokea huduma za rohoni. Neno la Mungu linasema watumishi wa Mungu wakipanda vya rohoni wanatakiwa wavune vya mwilini kutoka kwa waumini. 1 Kor 9:11 “Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini?” Lakini pia timiza ahadi ulizomuahidi Mungu ili shetani asipate nguvu ya kukushitaki kila unapomuomba Mungu akubariki. Shetani akiwa na haki ya kisheria (legal right) katika eneo lolote katika maisha yako huwezi kumdhibiti hata kama una cheo gani cha kidini! Ufu 12:10 "Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.” Mtu ambaye sio mwaminifu kwa Mungu hata akipata pesa nyingi hazifanyi cha maana. Na kama atafanya cha maana hatakifurahia. BARAKA SIO KUMILIKI TU MALI BALI NI KUFURAHIA UNACHOKIMILIKI. Ndiyo maana tuna watu wengi wenye mwenzi (mke au mume) wa kuonyesha watu lakini wao wenyewe hawapendani. Niliwahi kupata ushuhuda kwamba kuna Profesa wa chuo kikuu aliendelea kukaa nyumba za chuo kwa miaka akiwa hana ya kwake wakati dereva wake anamiliki shule yenye magari ya kusafirisha wanafunzi. Unaweza kuwa na pesa nyingi halafu shetani azipangie matumizi. Kuna watu wamepanda pesa nyingi kwenye arusi za watu kuliko kwa Mungu. Ila wakihitaji maombi hawaendi kuwekewa mikono na maarusi waliowachangia bali wanakimbilia kwa watumishi wa Mungu. Hag 1:6-9 anasema “Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka. Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema Bwana. Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema Bwana wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake.” Jitahidi pia kumheshimu Mungu kwa kutoa zaka kabla ya kutumia pesa yako badala ya kuitoa mwishoni baada ya matumizi. 

2. Kukopa ni njia yao ya kwanza katika kutatua matatizo yao 

Kuna mtu hata akiwa kwenye maombi mbele za Mungu bado anawaza akitoka hapo akamkope fulani. Kwa mtu kama huyo maombi ni kutimiza tu wajibu. Hajafunga macho yote mawili. Amefunga jicho moja kwa ajili ya Mungu na la pili linamtazama yule atakayeenda kumkopa. Inafaa kukopa iwe ni njia ya mwisho (last option) baada ya zingine kushindwa kuleta ufumbuzi. Unapomuomba Mungu unatakiwa kumpa muda na kufuatilia dalili za majibu yako. Kila jibu lina dalili zake. Dalili ya mvua ni mawingu. Eliya hakujipa moyo kwamba mvua itanyesha mpaka mtumishi wake alipoona wingu dogo kama mkono wa mtu.1 Fal 18:43-45 “Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba. Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli.” Hata hivyo tusimpangie Mungu majibu. Majibu ya Mungu yanaweza kuwa NDIYO, HAPANA au SUBIRI. Yote ni majibu sahihi kulingana na Mungu anavyotuwazia mema. Hayahaya ndiyo majibu tunayowapa pia watoto na rafiki zetu kwa nyakati tofauti. Amini kwamba Mungu yupo na anajibu maombi ukimngoja. Ebr 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” 

3. Kushindana na majirani zao 

Kuna mtu anaamua kukopa ili tu amuonyeshe jirani yake kwamba naye ana uwezo. Kibaya zaidi hana mpango wala mkakati wowote kwamba atalipaje. Neno la Mungu linasema ukikopa ujiandae kulipa kama u mwenye haki (sio tapeli). Zab 37:21a “Asiye haki hukopa wala halipi.” Kwa maneno mengine kama unajiona huna uwezo wa kulipa, usikope. Fanya unaloweza tu au tafuta kazi ya kufanya. Kipindi hiki watu wengi wanapenda anasa kuliko kumpenda Mungu (2 Tim 3:4). Pamoja na juhudi za maendeleo ni vizuri kutambua kiwango chako cha maisha na kuridhika nacho. Ebr 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Fedha sio mbaya ila tatizo ni TABIA YA KUPENDA FEDHA. Ukiwa na tabia ya kupenda fedha, UTAITUMIKIA FEDHA BADALA YA FEDHA KUKUTUMIKIA WEWE. Kitakachotokea ni wewe kutaka uonekane tajiri wakati wewe mwenyewe huufurahii huo utajiri. Ndiyo sababu sahani nzuri ulizo nazo ni za wageni wewe mwenyewe unatumia mbaya. Unavaa nguo nzuri ukijua utatembelewa na wageni lakini wewe mwenyewe hufurahii kuvaa nguo nzuri. Ukivaa vizuri hata watoto wanajua unaenda mahali fulani maana huwezi kuvaa vizuri ukiwa nyumbani kwako. Unapaka mafuta mazuri ukiwa unaenda mahali lakini wakati wa kulala hata kuoga ni shida. Nimewahi kusimuliwa kwamba kuna dada alikuwa amepanga chumba na sebule. Uwezo wake kiuchumi ni mdogo lakini alijitahidi kununua sofa kwa ajili ya sebule lakini yeye mwenyewe analalia mabox huko chumbani. Hivyo wageni wakimtembelea kama anaumwa atajivuta kwa shida atoke sebuleni wasije wakagundua analalia mabox. Mashindano ya maisha yamewafanya wengi wawe na maisha bandia na watawaliwe na madeni mengi. 

4. Kuwa na haraka ya maisha 

Watu wengi wanataka kufanikiwa kwa njia ya mkato. Hali hii haisababishi tu madeni bali pia inasababisha wezi waongezeke. Mit 13:11 “Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.” Wengi wenye utajiri wa kudumu walichuma kidogokidogo. Wanaochuma kidogokidogo wanakuwa na uzoefu wa kila hatua katika mafanikio. Ndiyo maana watoto wakiachiwa utajiri mara nyingi wanafilisika kwa vile hawajui changamoto wala tahadhari zozote za utajiri. Matokeo yake tunasema fulani amekufa na pesa zake. Mtu mwingine ingewezekana kabisa kwa kiwango chake cha kipato akajenga nyumba yake kwa miaka mitano bila mkopo wa riba. Lakini kwa vile anataka kumiliki nyumba kwa haraka anajikuta amemiliki nyumba ndani ya mwaka mmoja na deni kubwa analolilipia kwa muda mrefu sana. Muda huo wote anakuwa sio mmiliki wa nyumba na akipoteza kazi nyumba inaweza kupigwa mnada. Kibaya zaidi kuna mtu anakopa na kujenga nyumba kubwa inayoishia njiani huku akiwa anaendelea kulipa kodi ya pango. Ninakuambia hili kwa vile nimejenga jengo la kituo cha jamii na nyumba ya kuishi bila kukopa kwenye taasisi za fedha wala maduka ya vifaa vya ujenzi. Hata hivyo imenichukua muda kidogo lakini siishi kwa “presha” maana sidaiwi (niko debt-free). Ninaenda “mdogomdogo” lakini kwa neema ya Mungu nitafika tu. Pengine similiki vitu vingi kama wewe lakini namshukuru Mungu sidaiwi. Unapoamua kukopa hakikisha umeanza na pesa zako au juhudi yako hadi kufikia hatua fulani ndipo ukope. Kama u mfugaji jenga banda kwa nguvu yako mwenyewe kuliko mkopo ukianzia kwenye kutengeneza banda. Lakini kuna watu siku hizi wanawafanyia kazi watu wengine. Anachukua mikopo kwenye taasisi kama tatu hivi. Kwa vile tarehe za marejesho ni tofauti. Akikopa hapa, analipa pale. Ila kwa nje anaonekana ametingwa (yuko busy) kumbe hakuna faida anayopata katika huo uzungushaji wake wa pesa. Kimsingi anaonekana anachakarika (busy-ness) lakini hafanyi shughuli ya maana (business). Wapo wengine wanamega mkopo kununulia mahitaji ya familia kwa vile hawana njia nyingine za uhakika za kuingiza kipato. Inatakiwa mkopo wa biashara ukupe hatua nyingine na sio kusaidia kutatua mahitaji ya msingi (basic needs). 

5. Kulimbikiza madeni Watu wengi wanaokopa hawana mpango wa urejeshaji wa madeni.

Kila anapopata pesa hatengi kiasi cha kupunguza madeni. Matokeo yake madeni yanamzidi mpaka anaamua kubadilisha line za simu, kutopokea simu za wanaomdai au hata kukimbia mji. Ukitaka kuishi vizuri hapa duniani shughulikia madeni ya watu. Vinginevyo wanaweza kukuaibisha mbele za watu, kukufunga, kukufilisi, kuishi kwa hofu, unaweza kuugua au hata kufa ghafla. 2 Fal 4:1 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.” Huyu mtumishi wa Elisha alikuwa mcha Mungu lakini bado alikufa na deni kubwa nusura watoto wake wachukuliwe kuwa watumwa. Katika watu wanaolia katika misiba leo baadhi yao wanalia kwamba pesa imepotea kwa vile hawakuandikisha na marehemu katika uhai wake. Unapokuwa na madeni yasiyolipika unaweza kujikuta unakubali mtu asiyeeleweka aoe mwanao au hata kupangiwa ufanye mambo yanayodhalilisha utu wako. Kila unapopata pesa na kutimiza wajibu wako kwa Mungu, tenga kiwango fulani cha kupunguza madeni ili uaminike katika jamii. Hakuna kitu kibaya kama kupoteza “kuaminika” (trust) kwa watu ambao keshokutwa utahitaji tena msaada wao. 

6. Laana au roho ya umasikini 

Kuna watu hata kama utawapa milioni za pesa, hawatafanya cha maana (hawatatoka) kwa sababu kuna laana fulani. Laana inaweza kuwa ya kibinafsi au ya kiukoo. Mtu anaweza kulaaniwa na mzazi wa kimwili (baba, mama nk), mzazi wa kiroho (askofu, mchungaji nk), wachawi au kutokana na dhambi zake mwenyewe. Kum 28:43-46 “Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini. Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia. Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza; nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele.” Ingawa katika maeneo mengine ya kiroho tuko vizuri tukubaliane tu na ukweli wa Biblia kwamba ni laana kwa MGENI ALIYEKUKUTA KUINUKA JUU KIUCHUMI KIASI CHA KUKUKOPESHA WAKATI WEWE UNADIDIMIA NA HUNA CHA KUMKOPESHA. Usiendelee kujifariji kwamba wewe ni kichwa wakati kila mtu anaona kwamba u mkia. La msingi ni kumlilia Mungu atutoe katika laana. Mimi niliwahi kuomba kwa uchungu mpaka nikaonyeshwa ufalme wa giza unaozuia uchumi wangu katika ulimwengu wa roho. Hata Danieli alizuiwa majibu ya maombi yake na wakuu wa Uajemi kwa siku 21. Sijui wewe umezuiwa kwa miezi mingapi au miaka mingapi. Mara nyingi Mungu anaachilia majibu halafu yanashindwa kufika kwetu kwa vile hatujatengeneza mazingira yetu. Kwa wale waliowahi kusafiri nje ya nchi wataelewa mfano huu. HATA KAMA MALAIKA ANA PASSPORT, HATAWEZA KUFIKA KWAKO MPAKA UMPATIE VISA. Kwa kifupi kuna upande wa Mungu na upande wako. Dan 10:12,13 “Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.” Ndiyo maana kuna wakati ninakuwa na semina na kambi za kuangusha ngome. 2 Kor 10:3,4 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome).” Kuna watu wamewekewa mipaka na shetani – wasifikie elimu fulani, wasifanikiwe hata kama wamesoma, wasifanye cha maana hata kama wana pesa, watawaliwe na dhambi fulani mf. Kila anayeoa lazima apige mke, au kila anayeolewa lazima aachike, au lazima mtu azae nje ndipo aoe rasmi nk. Hii ni roho ya KUTOKUWA NA MAENDELEO KWA KASI INAYOTAKIWA NA KUCHELEWA KUPATA MAENDELEO (Spirit of retardation and backwardness). 

7. Kutopenda kujifunza ujuzi mpya 

Watu wengi ni wagumu kubadilika kulingana na mazingira (ku-adapt) hivyo wanapenda kufanya kazi zile tu walizozoea. Hii inatokana na watu wengi kutojifunza au kutoelewa vizuri somo la stadi za maisha (lifeskills). Hata wasomi wengi badala ya kutengeneza kazi au ajira (create jobs or employment) wanazunguka maofisi wakitafuta ajira. Hii imepelekea wasiosoma wengi kuwa wajasiriamali zaidi na kuwaajiri wasomi. Wengine wamesoma elimu ya dini tu lakini ujuzi mwingine hawajajifunza. Matokeo yake wanalazimika kuwafanya waumini kuwa mtaji au waajiri wao au kushindwa kuwaonya waumini wenye kipato kikubwa wanapokosea. Tunahitaji ujuzi wa kiroho kwa ajili ya umilele wetu lakini tunahitaji pia ujuzi wa kidunia kwa ajili mahitaji ya hapa duniani. Mdo 7:22 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.” Ilikuwa rahisi Mungu kumtuma Musa katika ikulu ya Farao kwa vile alilelewa na binti Farao na kubobea katika HEKIMA YOTE ya Wamisri. Bwana Yesu alikuwa seremala (Mk 6:3) na mtume Paulo alishona mahema (Mdo 18:3). Ujuzi haukusaidii tu kufanya kazi ya kipato bali pia unakusaidia kupunguza gharama. Mfano mimi nina majukumu mengi ya kiroho lakini kuna wakati nimeweza kuingiza kipato kwa kufundisha kingereza, kompyuta na kukarabati kompyuta zangu mwenyewe. Pia ni mwezeshaji (facilitator) wa masomo ya kijamii katika warsha mbalimbali kv ujasiriamali, UKIMWI, ukatili wa kijinsia nk. Mambo haya yamenifanya nisiwe tegemezi wala mzigo kwa kanisa. Na mimi pia nachangia kazi ya Mungu kifedha. Watumishi wengi wanahamasisha utoaji lakini wao wenyewe hata kipindi cha sadaka hawatoi. Watashangaa wakiingia mbinguni (kama wataingia lakini) wanakaa makao ya hali ya chini kuliko waumini wao kwa vile hawakupeleka vifaa vya ujenzi kwa kumtolea Mungu wakiwa hapa duniani. Hakuna mtu mwenye msamaha katika kumtolea Mungu. Gal 6:7 “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” 

8. Kukopa na kutumia fedha kwa ajili ya vitu visivyostahili 

Kama nilivyosema hapo awali, haifai kukopa kuwe ni njia ya kwanza ya kutatua tatizo. Kuna watu wanapenda kukopa kwa ajili ya kila jukumu la maisha. Wengine wanakopa hata kwa ajili ya kutoa michango ya arusi. Hivi kuna ubaya gani ukimwambia mtu sina mchango kwa leo? Tatizo ulijifunga kitanzi kwa kuwachangisha watu katika sherehe zako sasa lazima uwachangie hata kama ni kadi 10 kwa mwezi. Mwingine kwa bahati mbaya amechangia wafanyakazi wenzake na sasa amestaafu kabla mtoto wake hata mmoja hajaoa au kuolewa ili naye achangiwe. Hata kukopa kwa ajili ya kazi ya Mungu sio busara. Kuna mtu aliniomba ushauri kwamba anataka kukopa ili wajenge kanisa. Nikamuuliza swali: Kuna uhakika (guarantee) gani kwamba hao waumini watakuwepo hapo muda wote wa kulipa deni? Lakini kwa nini hatutaki gharama ya kumlilia Mungu ili atupe upenyo (breakthrough)? Tito 3:14 “Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.” Watu wa Mungu tunatakiwa kuwa na matumizi ya lazima ili tuwe na matokeo mazuri katika maisha. Pamoja na mikakati ya kukuza kipato tujifunze pia kubana matumizi. Tusiishi kwa mazoea. Kwa familia kubwa kununua vitafunio kila asubuhi ni ghali kuliko kupika chakula (kv wali) asubuhi. Kuwa na ratiba ya chakula kwa wiki kunaweza pia kusaidia kubana matumizi kuliko kuongozwa na hamu ya kula. Hii miili inataka vitu vizuri kila saa. Ndiyo maana Paulo akasema ameamua kuutesa mwili na kuutumikisha usije ukampeleka pabaya. 1 Kor 9:27 “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” 

9. Kutosamehe na kutokuwa makini 

Kila mwaka wa saba taifa la Mungu lilipaswa kusamehe wote wanaowadai. Na jambo hili ndilo lilisababisha heshima na baraka kubwa kutoka kwa Bwana. Leo hii mataifa mengi hayako tayari kusamehe madeni. Matokeo yake wanakutana na changamoto nyingi pia. Kum 15:1,2 “Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio. Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya Bwana.” Watu wengi wanatamani wangesamehewa madeni yao makubwa lakini wao wenyewe wameshindwa kuwasamehe wanaowadai kiasi kidogo sana. Mt 18:24-28 “Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho.” (Talanta 1 ni sawa na dinari 6,000. Kwa hiyo ingemgharimu mtu wa kipato cha kawaida siku 6,000 (miaka 16) kuingiza kiasi hicho. Sasa jiulize talanta 10,000 ni shilingi ngapi ukilinganisha na dinari 100!) Nimefanya majaribio nikaona kusamehe kunalipa. Mwaka juzi kipindi cha Pasaka nilitamka madhabahuni kwamba nimesamehe wote ninaowadai na kanisa tukasamehe wote tunaowadai. Tangu tufanye hivyo tumebarikiwa sana. Wanaoamini kwa wasioamini wamekuwa wakiguswa kuchangia huduma zetu bila kuwaomba. Nilishangaa muumini nisiyemjua wa hapahapa Korogwe akinipigia simu kuniambia amepata ufunuo anipatie kiasi fulani cha pesa. Nikashangaa akinipatia sh 400,000. Mtu ambaye sio muumini wetu alipita kanisani kwetu wakati tukiweka sakafu ya tiles akaahidi na kutimiza ahadi yake ya kutoa rangi kwa ajili ya jengo zima tena ile ya bei kubwa. Kuna watu wengi wenye pesa zako tatizo hutaki kusamehe! Hivi kama unamdai mtu sh 5,000 halafu mwingine akaguswa kukupa sh 100,000 kwa nini usisamehe tu zile 5,000? Hata hivyo tuwe makini sana katika kukopesha. Watu wengi tuliowakopesha wakatusumbua ni wale ambao tulisita moyoni halafu tukajilazimisha kuwakopesha. Mara nyingi Mungu anatukataza ila hatumuelewi vizuri au tunapuuza sauti yake. Mungu atusaidie ili tusijiingize kwenye majaribu yasiyo na sababu na pale ambapo tumeshajiingiza atupe mlango wa kutokea kwa kuwa Yeye ni mwingi wa rehema. 

Pokea msaada wa Mungu katika ugumu unaopitia sasa kwa Jina la Yesu Kristo! 

Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania