KWA NINI HADI LEO HALI YA MAISHA YAKO NI DUNI? – Dr Lawi Mshana
1. Unafanya kazi uliyozoea tu.
Hutaki kujifunza mambo mapya. Kumbuka kazi uliyojifunza kwa baba yako, babu yako au mwalimu wako naye alijifunza kwa mtu fulani. Lazima uwe mbunifu na kuanzisha kazi mpya au kujifunza kazi mpya zenye fursa tofauti. Siku zote utakuwa na mtazamo potofu au kinyume kwa vile hujapenda kuchukua muda kujifunza kwa mtu sahihi. Mimi ni mchungaji lakini pia ni mwalimu wa kompyuta, producer wa program za studio, mpiga vyombo vya muziki, mwandishi na mtafsiri wa vitabu, blogger nk.
2. Hubadilishi kampani au mtandao wako wa marafiki.
Kwa vile marafiki zako ni wale wale kila mwaka huwezi kuwa na mtazamo tofauti. Mfano, kama marafiki zako ni waalimu wenzako au wauza nguo wenzako au wachungaji wenzako hutaweza kujua nini kinaendelea upande wa pili. Baadhi ya watu walioniunganisha na fursa za kiuchumi sio watumishi wa Mungu. Najua kwamba kuna masuala ya kiroho na ya kiuchumi (ya kaisari tumpe kaisari). Sijawahi kwenda dukani nikapunguziwa bei kwa vile mimi ni mtumishi wa Mungu. Hivyo kuna maisha ya hapa duniani ambayo tunahitaji kufuata kanuni zake ili mradi zisitutoe katika kusudi la Mungu.
3. Kazi unayofanya haikupi muda wa kufanya kazi zingine.
Kuna watu ambao wanaamka saa 11 asubuhi na kurudi nyumbani saa 3 usiku kiasi kwamba hata watoto wanashindwa kujua wazazi wao. Kama huwezi kuibadilisha kazi hiyo lazima ikupe kipato kikubwa ili baada ya miaka kadhaa ufanye kazi nyingine ambayo itakuweka karibu na familia. Pesa haina maana kama mahusiano yatabomoka. Kama kipato ni kidogo na muda ni mdogo unatakiwa kutafuta kazi ambazo utaweza kuzifanya hata ukiwa kazini kwako na bado ujiingizie kipato kv biashara ya mtandao.
4. Huwatumii vizuri watu unaokutana nao.
Watu ni raslimali kubwa sana. Nilipoanza kazi ya kichungaji miaka zaidi ya 20 iliyopita nilianza kutumia vizuri teknolojia. Nilisoma diploma kuhusu Raslimali Watu kutoka chuo cha Uingereza kwa njia ya posta. Na baadaye kwa miaka tisa nikasoma shahada ya uzamili (udaktari) ya masuala ya imani kutoka chuo cha Marekani kwa njia ya video. Nilitambua uwepo wa vyuo hivi na kuweza kusoma bila mkopo wowote kwa sababu ya kutambua thamani ya raslimali watu. Watu wana thamani kubwa sana kuzidi pesa ambazo unazitafuta. Kuna watu wengi tangu uzaliwe mpaka leo huwajali lakini ni watu muhimu sana kwako. Tena wengine ni madaktari na watumishi waliotumiwa kukunusuru na kifo.
5. Unatafuta ajira badala ya kufanya kazi.
Unapoteza muda wakati kazi zimejaa. Kuna mtu tangu amalize chuo anazunguka tu maofisini kuonyesha wasifu (CV) wake. Kwa muda huo wote angeshatengeneza ajira yake mwenyewe kupitia ujuzi alio nao. Tatizo la wengi wanadhani kazi ni kuwa ofisini tu. Hawaoni uwezo walio nao ila wanaona tu upungufu walio nao. Jiulize watu wanaoenda makazini wana mahitaji gani ili wakuchangie wewe usiye na pesa. Mfano, ukianzisha kituo cha kuwalea watoto wao muda wa mchana (day care) utakuwa umepata kazi tayari. Wenye ajira rasmi watakulipa na wewe.
6. Umeridhika na kipato kimoja tu
Ni hatari sana kuridhika na kipato kimoja tu. Siku kikipata mtikisiko unaweza kupata kiharusi (stroke) kutokana na mshtuko. Lakini pia ukipunguzwa au ukistaafu unaweza kuwa na wakati mgumu kwa vile utakuwa huna uzoefu wa njia zingine za kipato. Matokeo yako wajanja wanaweza kukutapeli kwa vile ndo unaanza kujifunza kazi mpya. Kipato kimoja kikipata changamoto, kingine kinaweza kukusaidia wakati huo.
7. Unapowekeza hufikirii kuhusu gharama za uendeshaji
Watu wengi wanapoamua kuwekeza hawapigi mahesabu kuhusu gharama za uendeshaji (operating costs). Matokeo yake wanajikuta hawapati faida yoyote ila pesa zinaishia kwa watumishi. Nikupe mfano mdogo tu. Umeamua umchukue kijana akuuzie icecream mtaani halafu unamlisha hapohapo nyumbani. Unaweza kudhani unaingiza pesa lakini kimsingi unafanya kazi ya hasara. Hugundui hilo kwa vile unatumia mshahara wako katika kulisha familia. Biashara zinazohusika na gharama nyingi za watu na usafirishaji zinahitaji kushauriwa na wataalamu ili usije ukadhani unaibiwa kumbe ni mahesabu yako mabovu.
8. Unapohitaji ushauri unauliza watu ambao sio sahihi
Sio kila mtu anafaa kukushauri. Lazima umsome mtu kabla ya kumuomba ushauri. Hivi unadhani mtu anayepiga mkewe anaweza kukupa ushauri gani unapomueleza kuhusu changamoto za mkeo? Huwezi kumuuliza mtu akushauri kuhusu biashara ya mtandao wakati hajui internet, hajawahi kutumia smartphone na hajui miamala (transactions) ya kimtandao (online). Fahamu uwezo wa mtu kabla ya kumuomba ushauri. Kwa tatizo la gari lako nenda kwa fundi makenika na sio kwa daktari bingwa wa mifupa.
9. Unategemea huruma za watu kuliko uwezo wako
Kuna watu wanawaza zaidi jinsi watakavyomuomba fulani msaada badala ya kufikiria uwezo gani wanao wao wenyewe. Mimi kama mchungaji nafundisha watu wamtolee Mungu lakini sitaki ifikie mahali ambapo wasipomtolea wanaathiri maisha yangu. Ikifikia hapo nitakuwa naishi kwa kutegemea huruma zao na matokeo yake nitaanza kuwathamini wanaotoa pesa nyingi na kuwatetemekea. Naamini kwamba sio muda wote kwa siku niko busy na maombi na kusoma neno hivyo kuna wakati naweza kufanya jambo fulani la kuongeza kipato changu kv kutengeneza matangazo nk. Hata hivyo najua sitakiwi kufanya kazi za kipato ambazo zitanifanya nisipatikane ninapohitajika kutoa huduma za kiroho. Mfano, mchungaji ana ujuzi wa kutengeneza sabuni. Kuna ubaya gani akizitengeneza halafu akawapa wengine wakauze? Kwa nini alale njaa na Biblia yake ikiwa pembeni wakati hiyo Biblia imejaa maarifa tele?
10. Unaishi kwa mikopo kuliko uwekezaji
Mikopo sio mibaya lakini si vizuri kuitegemea sana. Badala ya kuendelea kuongeza mikopo jitahidi kufanya uwekezaji ili uanze kujisimamia kimaisha. Wekeza kwenye shughuli ambazo hazihitaji wewe mwenyewe uhusike moja kwa moja kv hisa, biashara za mtandao nk. Hizi ni kati ya shughuli ambazo zinafanywa na timu ya watu na sio mtu mmoja ambaye akiumwa na kipato kinasimama. Sio uwekezaji wote unahitaji kiasi kikubwa cha fedha.
11. Unatumia pesa nyingi kwa vitu visivyo na maana
Kuna mtu ukimwambia kiingilio cha chini cha biashara yetu ni laki moja na kitu anashika mdomo. Lakini wakati huohuo anamuomba Mungu awe milionea au bilionea. Biblia inasema apandacho mtu ndicho atakachovuna. Mkulima aliyepanda kisado cha mahindi hawezi kulingana na aliyepnda debe la mahindi labda patokee matatizo mengine kv ukame, mafuriko nk. Lakini pia kuna watu kwa mwaka wanatoa milioni za pesa kwa ajili ya kuchangia sherehe, kununua nguo mpya kwa kila sherehe nk lakini kwa vile hawaweki kumbukumbu wanadhani hawajatumia pesa nyingi.
12. Hutumii muda wako wa ziada vizuri. Unapiga porojo tu.
Kuna watu wakishatoka kazini wanatumia muda wao vibaya. Wanasahau kwamba wangeweza kuingiza kipato kwa kuwatembelea watu wanaojulikana (wenye connections). Mimi nimekuwa tayari kwenda ziara za mafunzo (study tour) kwa mtu aliyefanikiwa ili nijifunze zaidi. Nakumbuka kuna siku nilishiriki semina Dar ya wajasiriamali wakubwa duniani waliookoka. Walikuja watu wanaomjua Mungu kutoka Nigeria waliojaa Roho Mtakatifu na pesa pia. Sikwenda kama mchungaji bali nilikwenda kama mjasiriamali ninayeamini kwamba sio mpango wa Mungu watu wake wawe masikini wakati neno lake linasema fedha na dhahabu ni mali yake.
13. Unamiliki vitu vya thamani visivyo na msaada kwako.
Haina maana kumiliki vitu vya kuonyesha watu wakati havina manufaa yoyote kwako. Unawafanya watu waje kukuomba uwakopeshe wakati pesa hazipo. Utajiri ni wewe mwenyewe kufurahia maisha na sio kuwaonyesha wengine. Unaweza kujificha wageni wakija kwa kuwaandalia vyakula vizuri sana lakini watoto watakuumbua mbele ya wageni. Utashangaa wakati unamshukuru Mungu ili wageni wale, mtoto amechukua soda ya mgeni ameinywa nusu au amekimbia nayo kabisa. Kama una smartphone mbili na pesa hazipo, uza moja upate mtaji halafu baada uchumi kuimarika utanunua nyingine.
14. Hutaki kufanya kazi za kujitolea
Watu wengi wenye shida ya pesa wanawaza kuomba tu kazi za kulipwa. Wanasahau kwamba unaweza kuomba kumsaidia mtu kazi bila malipo na baadaye akuhurumie au akuunganishe na fursa. Lakini pia unapojitolea unauza ujuzi wako na kutengeneza mtandao na wateja wanaokuja mahali hapo kila siku. Mimi sijawahi kuwauliza watu wanaoniita kwa huduma kwamba watanilipa kiasi gani. Lakini kwa kufanya hivyo nimepata baraka nyingi sana. Hata nilipoalikwa siku moja kuhubiri kwenye kanisa ambalo mchungaji wake ana tabia ya kuiba pesa waliyotoa waumini kwa ajili ya mtumishi mgeni, nilijikuta nimepewa kiasi kidogo lakini mtu aliyeshiriki semina akaguswa kunitumia pesa benki kwa zaidi ya mwaka mzima. Mtumikie Mungu kwa kile alichokupa lakini pia watumikie watu na Mungu hatakupungukia wala kukuacha.
Dr Lawi Mshana, Korogwe, Tanga, Tanzania
Unauthorized use and/or duplication of this material without express and written permission from this site’s author and owner is strictly prohibited.
Excerpts and links may be used, provided that full and clear credits is given to Lawi Mshana and www.lawimshana.com with appropriate and specific direction to the original content.