Ticker

6/recent/ticker-posts

Nini kinawafanya watu washindwe katika maisha hata kama fursa zipo

NINI KINAWAFANYA WATU WASHINDWE KATIKA MAISHA HATA KAMA FURSA ZIPO?

Wapo wengi wanaodhani kwamba maisha yao yatabadilika kwa kuwa wasomi, kupata kazi, kupata mtaji, nk. Lakini ukifuatilia sana utakuta wapo watu ambao ni wasomi, wenye kazi, wenye mitaji nk na bado maisha yamewashinda. Mara nyingi mafanikio yanategemea mtu anavyomuona Mungu na anavyojiona yeye mwenyewe.

1. Unamuonaje Mungu? Lazima utambue kwamba Mungu anataka tufanikiwe pamoja na watoto wetu. Zab 25: 13 “Nafsi yake itakaa hali ya kufanikiwa; Wazao wake watairithi nchi”. (He will spend his days in prosperity and his descendants will inherit the land). Unapokuwa huna taswira sahihi kuhusu ahadi za Mungu kwako huwezi kufanikiwa. Mungu aliahidi watu wake kuwapa nchi ya Kanaani. Musa alipotuma watu 12 kwenda kuipeleleza nchi, wawili wakaja na ripoti nzuri. Hes 13:30 “Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.” Wale 10 wakaja na ripoti mbaya. Hesabu 13:31,33 “Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.” Wenye ripoti nzuri waliuona ukuu wa Mungu na wenye ripoti mbaya waliuona ukuu wa mataifa waliyoyakuta. Waliojiona kama mapanzi sijui walionaje kwamba hata mataifa waliyoyakuta yaliwaona pia kama mapanzi. Unapofikia kiwango cha kuona shida yako ni kubwa kuliko Mungu umejitangazia kifo na mazishi ya mafanikio yako.

2. Unajionaje wewe mwenyewe? Mithali 23:7 “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo”. Wewe unafanana na jinsi unavyojiona. Pesa au kazi havitaweza kukubadilisha kama mtazamo wako haujabadilika. Ndiyo maana Neno la Mungu likasema tunahitaji KUGEUZWA NA KUFANYWA UPYA NIA (MINDSET) ZETU. Rum 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Huwezi kujua Mungu amekupangia nini kwa uhakika hata kama uko vizuri kiroho kama fikra zako zimeharibiwa na shetani. Na hii ndiyo sababu ya baadhi ya waombaji wazuri kuendelea kuwa masikini kimaisha. 2 Wakorintho 11:3 “Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.”

Abraham Lincoln (Rais wa 16 wa Marekani) aliwahi kusema ‘Ninachojali mimi sio kushindwa kwako bali kuridhika kwako na hali yako ya kushindwa.’ (My great concern is not whether you have failed, but whether you are content with your failure). Hivi kama utateleza na kuanguka chini, utabaki hapohapo chini au utainuka uendelee na safari? Abraham anasema vita yake ni kwa watu ambao wakiteleza na kuanguka chini wanaamua kulala jumla.

Sasa ngoja nikupe mambo kadhaa ambayo yanakukwamisha au yatakukwamisha hata kama fursa ziko wazi mbele yako:

1. Kukata tamaa

Luke 18:1 Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.” Ukisoma zaidi sura hii Bwana Yesu alitoa mfano wa mjane ambaye alimsumbua kiongozi mwenye madaraka ambaye ni mkatili na hana hofu ya Mungu mpaka akalazimika kumpatia haki yake. Usumbufu wake ulimfanya awe kero kwa kiongozi huyo mpaka akasema kama sitampa haki yake huyu mjane atakuwa ananisumbua kwa kunijia daima. Inawezekana hata wewe msomaji wangu umeshindwa maisha sababu ya kukata tamaa. Afadhali ujaribu tena na tena kuliko kukaa tu kwa kisingizio kwamba ulishindwa mwaka jana. Nani ajuaye kama hutapenya ukijaribu safari hii! 2 Wakorintho 4:8 “Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa.”

2. Kutojali au kukosa shauku

Huwezi kufanikiwa kama hufurahii unachokifanya. Penda kazi yako unayoifanya na kuibariki na kuitabiria mema badala ya kusubiri mwingine akutabirie. Huwezi kufanikiwa kama hufanyi kazi zako kwa moyo. Nehemia 4:6 “Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi.” Kujenga ukuta uzunguke mji mzima sio kazi nyepesi. Siri ya mafanikio ya Nehemia na wenzake haikuwa kupata wafadhili bali ilikuwa ni MOYO WA KUFANYA KAZI. Kama mtu mwenye moyo wa kupenda wanawake au wanaume angeuhamishia moyo huo kwenye kazi kwa wiki moja tu, makubwa yangefanyika. Lakini yuko tayari akope, ahatarishe maisha yake, atumie vocha nyingi, atumie muda mwingi nk kwa vile ana moyo au shauku ya lile analolifanya. Mtunga Zaburi anasema, “Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana, Naam, na kuzikondea. Moyo wangu na mwili wangu Vinamlilia Mungu aliye hai” (Zab 84:2). Badala ya kukondea maisha ya watu sasa kondea nyua za Bwana na mafanikio ya maisha yako.

3. Kutokuwa mahali sahihi

Mafanikio yako hayako kila mahali unapopataka. Neno la Mungu linasema kuna watu watafanikiwa mjini na wengine kijijini. Ndiyo maana kuna matajiri kijijini na matajiri mjini na kuna walala hoi kijijini na walala hoi mjini. Kum 28:3 “Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.” Baraka za Mungu ziko mahali ambapo fursa zako zipo. Neh 7:4 “Basi mji ulikuwa wa nafasi nyingi, tena mkubwa; lakini watu waliomo walikuwa haba, wala nyumba hazijajengwa.” Nehemia anasema kuna watu hawaoni fursa zilizopo kwenye miji yao. Ukiwa mahali sahihi utaona nafasi nyingi na kuzitumia. Vinginevyo utaishi kwa mazoea ukiendelea kufanya mambo yaleyale maisha yako yote utafikiri ulizaliwa nayo. Usisahau kwamba ulikuja duniani bila nguo na bila nyumba. Wapo waliogundua vitu hivyo sasa na wewe jifunze kuwa mbunifu kuhusu maisha yako.

Wakati mwingine hufanikiwi kwa sababu uko mahali ambapo sio sahihi kwako, au unafanya kazi isiyo sahihi. Mtu mmoja aliwahi kusema ‘Kama samaki na mwanadamu watabadilishana makazi, wote watakufa kwa kukosa hewa.’ Maana yake ni kwamba inawezekana unakosa pumzi ya maisha kwa vile huko mahali sahihi. Mungu anataka uishi nchi kavu lakini umeamua kuishi baharini wakati hukuumbwa uishi huko. Baraka zako haziko kila mahali. Ipo nchi au kazi aliyokuandalia Bwana Mungu wako. Kum 28:8 “Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.” Wewe umeitwa kwa kusudi la Mungu. Unalijua kusudi hilo? Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”

4. Udhuru na lawama

Kuna watu wamekwama maisha kwa vile wanalaumu kila mtu isipokuwa wao wenyewe. Lakini pia wengine wana udhuru kila mara. Hawana maamuzi ya dhati kuhusu mustakabali wa maisha yao. Neno la Mungu linasema Mungu amekuwekea mbele yako uzima na mauti ili uchague mwenyewe maisha unayotaka. Kumbukumbu la Torati 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.” Mungu alikupa utashi (freewill) hivyo ni wajibu wako kufanya maamuzi sahihi badala ya kumlaumu Mungu pale mambo yanapokuendea vibaya. Hata Bwana Yesu aliwahi kusema watu wenye udhuru hawafai katika ufalme wa Mungu. Lk 9:61, 62 “Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.”

Lazima tujifunze kuwajibika na matokeo ya maisha yetu badala ya kuhamisha lawama kwa wengine (blame shifting). Pengine unasema “kama fulani hangefanya vile, ningekuwa mbali, kama singeishi pale singekuwa hivi, kama uchumi wa nchi haungebadilika singekuwa hivi nk.” Wakati unahamishia lawama kwa serikali, ndugu, nk usisahau kwamba wapo watu wenye maisha duni kuliko ya kwako na wamefanikisha mipango yao.

5. Kuogopa

Woga ni adui mkuu wa maendeleo. Ndiyo maana Mungu alipotuma malaika wake alipenda kuikabili kwanza hofu kwa kusema USIOGOPE. Luka 1:30 “Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.” Kwa muda mrefu umeomba Mungu akuponye ugonjwa, umasikini nk. Nakuombea leo uponywe hofu zako zote maana ndicho kizuizi chako kikubwa. Zab 34:4 “Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.” Yoshua alisisitizwa mara tatu kuhusu KUWA HODARI NA MOYO WA USHUJAA ili aweze kuwafikisha watu wa Mungu katika hatima yao. Yos 1:6-9  “Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa.  Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.  Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” Napenda ufahamu jambo la msingi sana kutoka kwa babu yetu Ayubu. Ayu 3:25 “Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia.” Kimsingi Ayubu anasema, JAMBO NINALOLIOGOPA NDILO LINALONIJIA. Hofu ni pepo hivyo ukiruhusu hofu maishani unamfungulia mlango shetani akulemaze. Zab 91:5 “Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana.” 

6. Kutoona mbele

Kuna watu hata wapate baraka kiasi gani hawafikirii kuhusu maisha yao watakapofikia uzeeni au watakapoondoka kazini au biashara ikipata dhoruba. Serikali yetu imeweka utaratibu wa kujiwekea akiba kwenye mabenki na mifuko ya jamii hata kwa wasioajiriwa nk ili kukabili ugumu huo endapo patatokea changamoto za maisha. Mtu mmoja aliwahi kusema inatakiwa mtu ajiulize swali hili: Kama leo nitasimamishwa kazi ghafla au biashara kuanguka ghafla nitakuwa na uwezo wa kuendelea na maisha kwa muda gani? Jibu hili linategemea kiasi gani umejifunza kwa sisimizi anavyoweka akiba. Mit 6:6-8 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.” Kuna bondia mmoja wa kimataifa (sitamtaja jina) hakupanga kustaafu. Alipata pesa sawa na shilingi za kitanzania bilioni 700 kwa michezo ya ngumi lakini akatangazwa kufilisika mwaka 2003. Jambo kama hili linaweza tu kumpata mtu ambaye hana mpango imara wa kifedha. Lazima tuwe na uwezo wa kuona miaka kadhaa mbele ili tusifanye mambo yanayogusa tu maisha yetu ya leo. Katika utamaduni wetu hatukuzoea kuweka akiba ndiyo maana hata matatizo ya kawaida kwetu tunayaita dharura au msiba. Kuna nchi fulani huruhusiwi kuzaa mtoto bila kuandaa mahitaji yake ya miaka minne ili hata ukitangulia mbele ya haki serikali imhudumie. Hata kama hatuwezi kufikia hapo si busara kuendelea kuangalia mimba ya mkeo ikikua kwa miezi 9 halafu mke anajifungua ndipo unakimbia nyumba kwa nyumba kukopa jogoo (tena sio kununua). Lazima tuishi kama wanadamu na si kama wanyama wasio na akili. 2 Petro 2:12 “Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao”.

7. Kukiri kushindwa

Kuna watu hawafanikiwi kwa vile wanalaani kazi za mikono yao na kazi za wenzi wao. Maneno yetu yana uwezo wa kuumba mema au mabaya. Mit 18:20,21 “Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”. Kuna watu wanapenda kukiri shida ili tu waonekane hawana kitu matokeo yake wanaloga mafanikio yao kwa vinywa vyao wenyewe. Wengi wetu ambao tumempa Yesu maisha yetu tumesimama hadi leo kwa vile tumekuwa tukikiri kwamba tumeokoka bila mashaka yoyote ingawa kuna changamoto nyingi. Unapokiri unapata wokovu yaani ushindi, mafanikio, afya nk. Warumi 10:10 “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” Umetegwa kwa maneno ya kinywa chako. Mithali 6:2 “Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako.” Hata shetani anafuatilia sana maneno unayosema ili akushughulikie. Ukisema, Mimi ni wa kuungua jua tu hapa kazini, atahakikisha unaungua jua kweli! Usiruhusu pia mtu atamke mabaya kuhusu maisha yako. Mlazimishe afute au ufute mbele yake hata kama hakukusudia. Lakini pia usitamke mabaya kwa watoto wako, utakwamisha maisha yao. Mungu atusaidie kushinda dhambi zinazotokana na vinywa vyetu kwa vile kuna siku tutatoa hesabu ya maneno hata ya siri mbele za Mungu. Mhu 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.” Zab 141: 3 “Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu”. 

8. Kuishi maisha ya laana 

Ni ukweli kwamba Bwana Yesu amechukua laana zetu pale msalabani. Lakini laana hizi haziondoki tu mpaka tulitumie Jina la Yesu na damu yake inavyotakiwa. Kama unabisha kuhusu hili kwa nini bado tunaumwa na tunahitaji kuombewa tukiwa wagonjwa wakati kwa kupigwa kwake sisi tumepona? Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Kimsingi laana ziko za aina nyingi na zina vyanzo vingi. Kulaaniwa ni kuwezeshwa kushindwa (to be empowered to fail). Laana ikiwa na sababu inakupata hivyo tuwe waangalifu tusiseme tu Yesu amebeba laana wakati tunaishi maisha ambayo hayaakisi kazi aliyoifanya msalabani. Mithali 26:2b “Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.”

Wakati shetani anawafanya watu washindwe, Mungu wetu anatupa NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI. Kama kuna nguvu za maombi, nguvu za kuhubiri, nguvu za kuponya nk pia kuna nguvu za kupata utajiri wa ki-Mungu. Kila eneo lina kanuni zake. Kum 8:18: “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”

Tunahitaji kibali cha Mungu ili wenye baraka zetu wawe tayari kuziachilia. Shetani ana uwezo wa kuwafunga wateja wako na wafadhili wako kama hakushughulikiwa vizuri. Kut 3:21,22: “Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu. Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.”

Nakuombea kwamba Mungu akufungue macho ili uone kile ulichoandaliwa na Bwana. Inawezekana unafanya kazi za watu wengine na umeacha kazi yenye baraka zako. Mimi nilijua baraka zangu zitapitia mkondo gani wakati nikiwa kidato cha pili miaka zaidi ya 25 iliyopita. Inawezekana pia unalolifanya ni zuri (good) kwako lakini sio mpango bora (better or the best) wa maisha yako.

Pokea ufahamu wa rohoni wa kukusaidia kuona ulichoandaliwa na Mungu katika stoo yake katika Jina la Yesu Kristo!

Pokea kufadhiliwa na Wamisri na kuwateka wenye baraka zako alizoziamuru Bwana zije juu yako katika Jina la Yesu Kristo!

Dr. Lawi Mshana, +255712924234; Tanzania