Ticker

6/recent/ticker-posts

Matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI au wanaougua UKIMWI



MATUNZO KWA WATU WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI AU WANAOUGUA UKIMWI 

Bado wapo watu wengi ambao hawajui tofauti ya KUISHI NA VVU na KUUGUA UKIMWI. Mtu anaweza kuishi na VVU na awe bado hajawa na UKIMWI. Kuugua UKIMWI ni kufikia hatua ya mwisho tangu mtu aambukizwe VVU. 

Mtu anapoambukizwa VVU anapitia hatua kadhaa kv kuwa na VVU lakini vipimo havionyeshi kwamba ameambukizwa kwa vile mwili wake haujaanza kutengeneza kingamwili dhidi ya VVU, vipimo kuonyesha kwamba ana VVU lakini mtu hana dalili zozote, vipimo kuonyesha kwamba ana VVU na dalili kuanza kuonekana na hatua ya mtu kuugua UKIMWI. Mtu akifikia hatua hii kama hatapata dawa za kupunguza makali (ARV) au Mungu mwenyewe kuingilia kati, atachukua muda mfupi kuishi pengine muda usiozidi miaka miwili. 

Lakini pia ni vizuri kuwaita WATU WANAOISHI NA VVU badala ya WAATHIRIKA. Ukifuatilia sana utagundua kwamba hakuna familia ambayo haijaathiriwa na VVU kwa namna moja au nyingine. Sio lazima mtu awe na VVU ndipo awe ameathirika. Ikiwa ndugu yenu amefariki kwa UKIMWI akawaachia watoto wake muwalee tayari mmeathirika, ikiwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake amefariki tayari tumeathirika, ikiwa ndugu aliyekuwa anakusomesha amefariki ukaacha shule tayari umeathirika, ikiwa mwenzi wa maisha amefariki hata kama aliyebaki hakuambukizwa pia anakuwa ameathiriwa na kifo hicho. Mtu mmoja aliwahi kusema HATA KAMA HUJAAMBUKIZWA, UMEATHIRIKA (If you are not infected, you are affected). 

Lakini pia kuna watu wana VVU kwenye damu zao lakini wana maisha mazuri kuliko hata wale ambao hawana. Ndiyo sababu tunatumia lugha ya WANAOISHI NA VVU. Mtu anaweza kuishi na VVU na wakati huohuo akatae au acheleweshe kufikia hatua ya kuugua UKIMWI. Ili mradi aikubali hali yake na kuwa tayari kujifunza jinsi ya kuishi na hali yake na kumtegemea Mungu. 

KWA NINI TUJIFUNZE KUWATUNZA WANAOISHI NA VVU NA UKIMWI? 

1. Wagonjwa wa UKIMWI ni wengi kuliko uwezo wa wahudumu wa afya. Ukizingatia kwamba wanawahudumia pia watu wenye magonjwa ya aina mbalimbali. 

2. Ugonjwa wa UKIMWI hauna tiba hivyo sio ugonjwa unaohitaji mtu akae muda wote hospitalini. 

3. Wagonjwa wa UKIMWI wanahitaji huduma katika kipindi chote wakiwa hai. 

4. Ushauri wa mapema baada ya mtu kujua ana VVU kunamsaidia kukubaliana na taarifa mbaya na ajue mabadiliko ya kitabia yatakayompata. 

5. Ingawa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) zinapunguza kasi ya ugonjwa, msaada wa kihisia na kiroho unahitajika kwao na familia zinazowatunza. 

6. Watu wanaoishi na VVU wanatakiwa kushinda vikwazo vya kijamii, kitamaduni na kiuchumi ili waishi kama watu wengine. 

7. Baadhi ya wahudumu wa afya pia wanakufa kwa UKIMWI hivyo wahudumu wanapungua katika taasisi za afya. 

8. Tunaweza kupunguza maumivu yao hata pale wanapokuwa wamefikia hatua za mwisho (tiba shufaa). Ingawa tiba hii haiondoi chanzo cha tatizo, inaboresha maisha ya mgonjwa na familia kisaikolojia, kijamii na kiroho. Inamsaidia mtu afe kwa amani na heshima. Tiba hii inagusa pia watu wanaougua magonjwa mengine sugu kv saratani nk. 

HUDUMA HII INAGUSA MAENEO MAKUU MANNE: 

1. AHUENI YA DALILI ZA UGONJWA Wagonjwa wengi wa UKIMWI wanapata uchovu, maumivu, kupoteza uzito, kukosa usingizi, kupumua kwa shida, kuharisha, homa , matatizo ya ngozi na sonona (depression). Kwa bahati mbaya dalili hizi mara nyingi zinapuuzwa. 

2. MSAADA WA KISAIKOLOJIA NA KIROHO Mgonjwa anaweza kusaidiwa kuikubali hali yake, kuizungumzia na kushinda hofu kwa kupewa ushauri binafsi, kukutana na watu wengine wanaoishi na VVU na kupatiwa msaada kutoka katika jamii na familia. 

3. HUDUMA KARIBU NA KIFO Watu wengi hawapendi neno kifo litamkwe. Lakini ukweli ni kwamba tuwe tuna UKIMWI au la siku moja tutakufa. Kifo sio dharura ni jambo ambalo Mungu ameliweka wazi hivyo kila mtu anapaswa kujiandaa kwamba ATAONDOKAJE na ATAWAACHAJE WANAOMHUSU. 

Walezi wa watu wenye UKIMWI wanaweza kuwasaidia wagonjwa na ndugu zao wa karibu kwa: 

• Kuwafanya wajisikie vizuri kwa kuwauguza vizuri kwa kuwajali. • Kuwaandaa kwa kifo pamoja na mipango ya wategemezi wao. 

• Kuwashauri wafiwa (familia na marafiki) washinde simanzi. 

4. HUDUMA KWA WALEZI Walezi wanaweza kuwa wanafamilia, wanaojitolea katika jamii (valantia) au wahudumu wa afya. Huduma hii inaweza kutolewa nyumbani, hospitalini,kwenye mashirika na kwenye taasisi za dini. Watu wanaoishi na walioathiriwa na VVU wanaweza kutoa mchango mkubwa kwa vile wana uzoefu. Katika hatua za mwisho walezi wanatoa huduma za kusaidia kulisha, kupeleka uani, kuogesha, kusafisha vidonda, kusimamia unywaji wa dawa, faraja, ukaribu (company), kushauri na maombi. Hivyo wanahitaji uelewa wa kutosha kuhusu UKIMWI, njia za maambukizi, kinga na jinsi ya kutoa huduma bora. 

Dr Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania