Ticker

6/recent/ticker-posts

Unajua ni mambo gani yanasababisha kasi ya maambukizi ya UKIMWI?

Unajua ni mambo gani yanasababisha kasi ya maambukizi ya UKIMWI? 

Wapo watu wanaoamini kwamba wenye VVU/UKIMWI wanalipia matendo yao ya dhambi. Wanasahau kwamba kuna watu hawajaambukizwa UKIMWI ingawa wamebobea kwenye dhambi. Lakini pia wanasahau kwamba kuna watu walikuwa wametulia kabisa kwenye ndoa zao na bado wakaambukizwa kutokana na mmojawapo kutokuwa mwaminifu au kwa kumhudumia mgonjwa bila tahadhari zozote. Lakini pia kuna watoto wamezaliwa na VVU bila kuhusika moja kwa moja na dhambi yoyote. 

Maambukizi yanaenea zaidi kwa ngono lakini mchakato hauanzii hapo bali katika mazingira ya kijamii, kidini na kiuchumi. Hivyo lazima tuwe na mtazamo mpana kuliko kulaumu peke yake. Haitoshi kusema tu kwamba UKIMWI unaenea kwa vile watu wako mbali na Mungu. Lazima kitu kingine kifanyike. Hivi nyoka akiingia nyumbani kwako utaanza kuuliza nani aliacha mlango wazi au utatafuta kwanza namna ya kumuua? 

Sababu za kijamii na kiroho za kasi ya maambukizi ya UKIMWI: 

1.Ujinga 
“Kujua jambo kidogo ni hatari sana.” Ujuzi mdogo unawafanya watu wengi washindwe kubadili tabia. Katika utafiti uliowahi kufanyika Nigeria, iligundulika kwamba mtu 1 kati ya watu 12 aliwahi kujadili UKIMWI na Mchungaji wake na hakuna aliyeorodhesha kanisa au mchungaji kama chanzo cha taarifa. Hii ilidhihirisha kwamba taasisi nyingi za dini zimejikita zaidi katika kukemea dhambi kwa ujumla wake na kuacha kuzungumzia masuala maalum kv UKIMWI, ukatili wa kijinsia nk. Matokeo yake wengi wanakufa au kuathiriwa na tatizo hili bila kujulikana na bila hatua zozote kuchukuliwa. Lazima watu wapewe pia stadi za maisha ili waweze kuepuka mazingira hatarishi na kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha. 

2. Taarifa isiyo sahihi 
Wengi wanaodhani wanajua kuhusu UKIMWI wana taarifa isiyo sahihi. Wapo wanaosema kama ni mapenzi ya Mungu wafe kwa UKIMWI, watakufa tu. Wapo wanaosema nchi za Magharibi zimeingiza VVU Afrika ili kuzuia ngono na kupunguza idadi ya watu. Wengine wanaamini UKIMWI ni laana na adhabu. Tangu nitoe mafunzo ya UKIMWI kwa makundi mbalimbali ya kijamii nimegundua kwamba wengi hawajui hata maana ya VVU au UKIMWI kiusahihi ila ukikutana nao mtaani wanadhani kwamba wanajua sana na hawahitaji mafunzo hayo. 

3.Ukimya wa wazazi na viongozi wa kiimani 
Moja ya silaha kubwa za shetani ni kuzuia tusizungumze na watoto kuhusu ngono na afya ya uzazi. Wapo watoto wanaosoma shule za bweni mbali sana na wazazi wao lakini hawajui hata mimba inavyotungwa. Kuna wazazi walikuwa hawajawahi kumfundisha binti yao kuhusu mabadiliko ya mwili wake. Siku moja binti akashangaa kupata hedhi njiani. Alidhani amepata ugonjwa mbaya sana. Kijana ndiye akamshauri atafute vitambaa hivyo akamnusuru na aibu kubwa. Siku nyingine alipokutana na yule kijana akamwambia anayo dawa ya kumaliza ule ugonjwa wake. Binti akatamani kujua zaidi dawa hiyo ili asiaibike tena. Matokeo yake akamrubuni na kweli hedhi ikakoma maana amempa mimba. Hili lilichangiwa na ukimya wa wazazi unaopelekea vijana kupata taarifa kwa watu ambao sio sahihi. 

4. Utamaduni wa kiafrika 
Wasichana wanashindwa kuwa na ujasiri wa kumkataa mwanaume kutokana na utamaduni wa baadhi ya watu. Wazazi wakishaamua msichana anapaswa kufuata tu. Waliowatafuta machangudoa zamani sasa wanawatafuta wasichana wadogo wakiamini hawana UKIMWI. Vijana wanahitaji kujua kwamba Mungu amewaumba kwa kusudi kubwa na maisha yenye maana. Wathamini miili yao ili ndoto zao zisiharibiwe na wajanja. Lakini pia wapo wavulana wanaorubuniwa na wamama (sugar mummy) kutokana na ugumu wa maisha walio nao na kutafuta njia za mkato katika kufanikiwa. Wangejituma katika kazi wangeweza kuepuka mitego hiyo. 

5.Aibu, unyanyapaa, hofu na kukana tatizo 
Mara nyingi watu wakigundua wameambukizwa VVU, wanaona aibu na hofu. Wanaweza hata kukataa hali yao ya maambukizi na kujaribu kuwaficha wengine. Hawataki kukubali hali yao kwa vile wanaweza kutengwa na familia zao, kupoteza kazi zao, kukataliwa na majirani nk. Hali hii inawafanya washindwe kupatiwa msaada wanaostahili na kujikuta wakiambukizwa tena. Mtu anaweza kuwa na VVU na akutane na mtu mwingine mwenye VVU na kuambukizwa tena. Na kibaya zaidi anaweza kukutana na virusi vyenye kasi zaidi ya kutafuna kuliko vile alivyokuwa navyo. 

6. Umasikini na kuhamia mjini 
Umasikini, lishe duni na huduma duni za afya ni vitu vinavyochangia katika kasi ya maambukizi ya VVU. Vijana wanapohamia mijini wanakosa uangalizi waliokuwa wanaupata wakiwa karibu na ndugu vijijini. Kijana anaweza kujikuta anakaa chumba kimoja na wenzake wanaoingiza wasichana na kufanya ngono. Mazingira haya hatarishi yanamfanya naye atumbukie kwenye mtego huo. Wakati mwingine wazazi wanawalazimisha mabinti zao wadogo waolewe na matajiri ili wapate mahari kubwa na kupewa msaada zaidi. Matokeo yake wakishaolewa wananyanyaswa bila huruma yoyote na matajiri hawa ambao wana wapenzi wengi. 

7. Familia kutengana 
Maambukizi ya VVU ni ya kasi katika maeneo ya mijini kwa vile wengi wanaishi mbali na wenzi wao. Wanaingia katika mtego huo kupitia wanawake waliopanga jirani nao wanaowasaidia huduma za nyumbani au wanaofanya nao kazi. Wanawake nao walioachwa vijijini wanajisikia wapweke na kujikuta wanaanza mahusiano na wafanyakazi waliohamishiwa kijijini kama vile waalimu, madaktari na polisi. Ni vizuri juhudi zifanyike kuhakikisha wanandoa wanakuwa karibu. Ikibidi watembeleane mara kwa mara kwa vile hawatanufaika na pesa wanazochuma kama ndoa zitavunjika. Wafanye kazi kwa malengo. Mfano baada ya muda fulani wabadilishe kazi au mazingira ili wawe pamoja na kulea familia kwa pamoja. 

8. Safari ndefu 
Wengi wanaosafiri safari ndefu kama vile madereva wa malori na wafanyabiashara, wanakuwa katika mazingira hatarishi. Maeneo wanakopumzikia wakiwa safarini, wapo makahaba wanaojifanya kuwaliwaza na kujikuta wakiendeleza mtandao wa maambukizi. Vilevile viongozi wanaoshiriki makongamano na warsha wanakutana na wasichana wa biashara ya ngono mahotelini. Kama wanakuwa na mazoea yasiyo na mipaka ni rahisi kuanzisha mahusiano hatarishi. Lazima kujifunza kuwa na maamuzi thabiti katika maisha badala ya kuongozwa na hisia za mwili. 

9. Mila na desturi 
Mila ya Kiafrika ya mahari kubwa inawafanya vijana wengi wakidhi tamaa zao bila kuoa au kuolewa. Wapo ambao wamelazimika kuchukuana kienyeji kutokana na kutakiwa kulipa mahari kubwa wasiyoimudu. Lakini pia mila ya kushirikiana wake na kurithi wajane inaongeza kasi ya maambukizi ya VVU. Wapo watu wenye desturi ya kumkirimu mgeni kwa kumpa mke alale naye. Wapo watu ambao mtu akifiwa anatakiwa kutakaswa kwa kulala na mtu fulani katika ukoo mwenye jukumu la kutakasa wajane. Mila hizi na zingine potofu zinahitaji kupigwa vita kwa nguvu zote ili tuwe na jamii ambayo iko salama. 

Dr Lawi Mshana, +255712924234; Korogwe, Tanga, Tanzania