NINI KINASABABISHA FARAKA KATI YA WAPENTEKOSTE NA WANA-UAMSHO (CHARISMATIC)
Na Dr Lawi Mshana (kutoka jarida la Hema Aprili-Juni 2009)
Mungu tunayemuabudu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. (Mdo 10:34,35). Pia Mungu huyo huyo huwaangazia jua lake waovu na wema na huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki (Mt 5:45,46). Je ni mpango wa Mungu kwamba watu wanaomwabudu wapambane badala ya kuelekezana kwa upendo? Napenda kutumia nafasi hii kukupa sababu zinazosababisha ufa huu kati ya makundi haya yaliyopokea neema ya Mungu na vipawa vya Roho Mtakatifu:
1.Kuangalia zaidi majina ya madhehebu kuliko uhusiano wa mtu na Kristo.
Watu wengi wanaitambua imani ya mtu kwa kuulizia dhehebu lake badala ya kuchunguza mwenendo na matunda ya Roho ndani yake. Si mpango wa Mungu tuitwe wakristo kwa vile tu tu washirika wa dhehebu fulani bali kwa kuwa na tabia ya Kristo. Hatutakiwi kujiita wakristo bali tuitwe wakristo! Mdo 11:26b “Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.” Mtu anaweza kukutana na Yesu mahali popote ingawa hawezi kukua kiroho mahali popote. Ukuaji unahitaji utaratibu maalum wa kulea wakristo wapya. Ukristo kamili sio tu kumpokea Yesu na kuwa mshirika katika dhehebu fulani bali ni kuwa mwanafunzi hai wa Yesu katika kanisa la Mungu.
2. Kujali zaidi mambo yanayotofautisha na kusahau yanayounganisha.
Ni ukweli usiopingika kwamba kama tutatafuta mambo yanayotutofautisha, sio tu kwamba hatutaweza kuishi pamoja bali pia tutapoteza maana ya sisi kuitwa viungo katika mwili wa Kristo. Tukianza na mambo yanayotuunganisha inakuwa rahisi kusaidiana katika yale tunayotofautiana. Kwa mfano makundi haya yanasahau kwamba yanakubaliana kwamba Mungu wetu ni mmoja katika nafsi tatu, Biblia ni Neno la Mungu, Yesu ndiye Mwokozi pekee wa ulimwengu, wenye haki watakwenda mbinguni na wasio haki watakwenda motoni. Tukianzia na haya, tutaweza kusaidiana hata na yale mengine. Yn 17:8-11 “Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.”
3. Kulinda mafundisho ya kidini badala ya kuilinda imani.
Kuna watu wanasahau kwamba dini haiendi mbinguni na dini ndiyo ilikuwa mstari wa mbele katika kumuua Bwana Yesu kupitia wakuu wa makuhani wa kipindi hicho. Mt 27:1,2 “Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua; wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali.” Watu wa dini wako tayari kulinda mapokeo ya kidini hata kama hayana uthibitisho wowote katika maandiko ili mradi tu yanawasaidia kukubaliwa na wanadamu na kujiona salama katika hali waliyo nayo. Wakolosai 2:23 anasema, “Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.” Ndio maana Paulo badala ya kuyalinda mapokeo ya dini anasema, ‘Imani nimeilinda’ (2 Tim 4:7).
4. Kushindwa kutambua utendaji mpya wa Roho Mtakatifu.
Kuna watu hawajui kwamba ingawa Mungu habadiliki, anaweza kubadilisha watu na hata mfumo wa utendaji wake. Kuna wakati Mungu alisema na watu moja kwa moja kama Baba, baadaye akakaa na watu kama Mwana na mwishowe, akaamua aishi ndani ya watu kama Roho Mtakatifu.
Joshua alitaka Musa awakataze Eldadi na Medadi wasitabiri. Hes 11:27-29 “Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake.” Musa akamkatalia ombi lake. Mwanafunzi wa Yesu naye alimpa Yesu taarifa kwamba aliona mtu anatoa pepo kwa Jina la Yesu akamkataza. Yesu akamwambia, Msimkataze kwa kuwa yuko upande wenu (Lk 9:49,50 “Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu.” Mfumo wa dhehebu hauwezi kuzuia utendaji wa Mungu kupitia mtumishi wake kama atatii uongozi wa Roho Mtakatifu. Lakini kama atang’ang’ania kuwepo mahali kinyume na mpango wa Mungu atakuwa anatumika bila matokeo mazuri ya huduma aliyopewa.
5. Kutumia maneno ya kudhalilisha badala ya kusaidiana kwa upendo.
Kila kundi limembatiza mwenzake majina ya kudharau kiwango chake kiroho. Na wakati huohuo kila kundi linafanya uinjilisti wa kuwatafuta waliopotea. Swali ni je, nani yuko karibu zaidi? Ni yule asiyejua kabisa maana ya wokovu au ni yule aliyempokea Yesu ila tu amebakiza kuwekwa huru katika mambo machache? Je, ni halali mpentekoste na mwana-uamsho kushindwa kukaa pamoja wakati katika misiba na sherehe wanakaa pamoja na wapagani waliolewa pombe? Naomba Mungu atupe ufunuo zaidi wa ‘Msifungwe nira na wasioamini kwa jinsi isivyo sawasawa’ (2 Kor 6:14). Jinsi iliyo sawa sawa ni kuhusiana na wasioamini kwa malengo ya kuwavuta kwa Kristo bila kuichafua imani yako.
Ndugu yangu kama tutakuwa na nia ya Kristo ya kusaidia watu waende mbinguni, badala ya kujali maslahi binafsi na ya dini zetu, hatutaridhika kuwa na waumini wengi ambao hawana ushindi wa dhambi. Hebu tuungane na mtume Paulo katika maneno haya: Fil 3:4-15 “Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia hilo nalo.
Unauthorized use and/or duplication of this material without express and written permission from this site’s author and owner is strictly prohibited.
Excerpts and links may be used, provided that full and clear credits is given to Lawi Mshana and www.lawimshana.com with appropriate and specific direction to the original content.