Ticker

6/recent/ticker-posts

Kanuni 30 za msingi katika kuanzisha na kuendesha mradi usiofilisika

KANUNI 30 ZA MSINGI KATIKA KUANZISHA NA KUENDESHA MRADI USIOFILISIKA 
(Unaweza kuzitumia kwa miradi ya kiuchumi au kwa huduma za kiroho) 

1. Muombe Mungu. Mit 16:3 “Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.” Swali: Je wazo la shughuli yako lilizaliwa wakati ukiwa magotini? Na kama la, ulipiga magoti kuthibitisha kwamba wazo hilo limepata kibali kwa Mungu? 

2. Thubutu Yos 1:6 “Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa.” Swali: Kiasi gani uko tayari kuhatarisha maisha yako au kujinyima ili ufanikiwe? Umeshinda hofu ya kushindwa ambayo imetawala wengi? 

3. Fanya utafiti – Mfano tambua raslimali zilizopo, fursa nk Lk 18:37,38 “Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.” Swali: Je umeainisha raslimali ulizo nazo zinazohitajika kwa shughuli yako na je kuna fursa unazoona au ni vile tu umeizoea hiyo shughuli kwa miaka mingi? 

4. Tambua uwezo wako . Usikimbilie kuiga watu. Mt 25:15 “Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.” Swali: Je ukijitazama una sifa za kupata mtaji unaohitaji? Je utaweza kuuingiza mtaji wote kwenye mzunguko kwa faida au sehemu ya mtaji utaitumia tena kwenye kurejesha mkopo? 

5. Fahamu jinsi ya kuutekeleza huo mradi Luka 16:3 “Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya.” Swali: Je unajua hiyo shughuli vizuri au unategemea wasaidizi wako ndio wakuongoze? Je unajua vyanzo vya taarifa muhimu ili uutekeleze kwa ufanisi? 

6.Mazingira yavutie Usijali tu biashara au shughuli yako ukasahau kwamba wateja wako ni watu wanaohitaji kuvutiwa na mazingira. Hebu jiulize kama utafika kwa mama au baba ntilie anayeuza supu nzuri sana lakini hajanawa uso (ana matongotongo machoni), au unasubiri hotelini kwa robo saa na hakuna anayekusogelea kukuuliza unahitaji huduma gani. Au je kama mtu anauza maandazi mazuri sana lakini yuko eneo ambalo ni karibu na choo cha jirani yake? Mazingira bora sio usafi peke yake bali pia ucheshi (kama hujui kutabasamu katafute kioo cha kujitazama ufanye mazoezi), kauli nzuri (acha lugha za mkato, unafukuza wateja mwenyewe. Usitusumbue tukuombee wala usisingizie kwamba kuna mkono wa mtu wakati mchawi ni wewe mwenyewe kwa kauli zako!). 

‏ 7.Mpangilio mzuri wa bidhaa (goods) au mazao (products) Kadri inavyowezekana pangilia vizuri bidhaa zako kama ni dukani au mafaili yako kama ni ofisini. Mpangilio mzuri sio tu kwamba unakusaidia umhudumie kwa haraka mteja bali pia unakusaidia kutambua mahitaji ya duka au ofisi kwa haraka zaidi. Vinginevyo utagundua kwamba bidhaa fulani imeisha pale mteja atakapokuja tena akiwa na kitita cha pesa. Utaona uchungu ukimuona anaondoka kutafuta bidhaa au huduma hiyo mahali pengine. Lakini pia unajisikia vizuri kutazama bidhaa au mafaili yako yakiwa yamepangika vizuri. Ofisi ambayo imewekwa vitu kiholela inaweza kukufanya ujisikie kuchanganyikiwa na kuumwa kichwa kwa vile kila unachohitaji ni lazima akili itumike sana kukumbuka kwamba kiko wapi. 

8.Weka vivutio Inategemea shughuli yako ni ya aina gani. Lakini vivutio ni muhimu sana ili mteja aliwazwe na huduma fulani mf redio,TV, internet au magazeti hasahasa kama ni shughuli inayowalazimu wateja wasubiri muda mrefu kabla ya kupata huduma iliyowaleta. Kama ni ofisi inaweza kuwa na feni au viti vya ofisi ambavyo havichoshi kukalia kwa muda mrefu. Unaweza kukuta duka lina wateja wengi wanaosubiri kuhudumiwa lakini hata kiti kimoja cha kukalia hakuna. Jambo hili linaweza kuwafanya wateja wasioweza kusimama kwa muda mrefu waondoke au kuhamia duka jingine. 

9.Ratiba ieleweke (reasonable timetable) Kuamua kufungua duka au ofisi kwa wakati unaoona kwamba unakufaa wewe mwenyewe kunaweza kuwa na madhara makubwa kuliko unavyofahamu. Mtu mmoja anaweza kufukuza wateja wengi kwa vile tu alifika siku fulani saa 3 akakuta duka halijafunguliwa. Anapokutana na mtu anakuja dukani kwako anaweza kumwambia, ‘Saa hizi yule hajafungua au Alhamisi kama leo hafungui’. Bila kukusudia anaweza kukufukuzia wateja wengi. Ni vizuri kutoa tangazo kama kuna mabadiliko ya ratiba yaliyotokea au kuweka namba ya simu kama ni ofisi inayotoa huduma. Ili kuepuka usumbufu simu hiyo inaweza kuwa maalum kwa masuala ya ofisi tu ili kuepusha usumbufu unapokuwa nyumbani kifamilia. 

10.Uwe na bidhaa au huduma za aina tofauti (varieties of goods or services)‏ Usipendelee kutegemea biashara ya bidhaa moja au huduma moja. Kama unategemea bidhaa ya aina moja unaweza kufilisika kama itakosekana ghafla au mamlaka itaipiga marufuku wakati imejaa kwenye duka lako. Pia bidhaa nyingi zinahitajika kwa misimu. Ni mara chache sana bidhaa ya aina moja itahitajika kwa mwaka mzima. Mfano soda zinanywewa zaidi kipindi cha joto, miavuli inatoka zaidi kipindi cha mvua na chai inanywewa zaidi kipindi cha baridi. Kuna kipindi watu hawanunui nguo kwa vile kipindi hicho kuna njaa. Kama mafunzo yako yanaandaa tu wanafunzi wanaojiunga na sekondari, jiandae kuwa na darasa miezi miwili tu kwa mwaka pengine Novemba na Desemba tu. 

11.Jali mahitaji ya wateja – wanapenda nini Ni jambo la kawaida kwa wajasiriamali wengi kununua bidhaa au kutoa huduma bila kufanya feasibility study ili kutambua mahitaji ya wateja. Ni eneo moja tu ambapo watu wengi tunafanya vizuri katika kujali mteja. Nalo ni pale tu tunapotembelewa na mgeni huwa tunapenda kumuuliza anapendelea soda gani ili tuguse moyo wake zaidi kuliko kumpatia yeyote. Tusijaribu kulazimisha wateja wapende bidhaa zetu. Hata hivyo kwa bidhaa mpya tunaweza kutembelea wateja tunaowalenga na kuzitangaza ili wazipende lakini tusizijaze dukani kwa vile hakuna uhakika kwamba mwitikio wao utakuwa chanya. 

12.Usigawe bidhaa bure bila kuzilipia Wamiliki wengi wa maduka hasa ya chakula wana tabia ya kuchota unga na kutumia kwenye nyumba zao bila kulipia kama wateja wanavyolipia. Mwingine anapompa mgeni wake soda dukani, hailipii. Wengi wanadanganyika na mauzo kwa siku yanavyoonyesha kwamba kuna pesa nyingi wamepokea. Wanasahau kwamba hata kama pesa ni nyingi kwa siku, sio zote ni FAIDA. Inategemea vitu vilivyouzwa siku hiyo ni vitu gani. Kuna bidhaa zinakuwepo dukani ili tu mteja akinunua aone na zingine lakini faida yake ni ndogo sana mfano viberiti. Kama itatokea siku hiyo ukauza viberiti vingi inawezekana faida ikawa ni ndogo sana. Hata hivyo lazima ujue faida yako ni kiasi gani na gharama za uendeshaji ni kiasi gani ili usifanye kazi ya hasara. 

13.Usikopeshe mwanzoni mwa biashara. Ikibidi, uwe mfuatiliaji makini. Usipendelee kukopesha wakati bado uwekezaji wako na mzunguko wa biashara yako ni mdogo au hauna uhakika. Kuna watu wamelizwa baada ya kukopesha vitenge mapema na kucheleweshewa au kutolipwa fedha zao kabisa na kisha kushindwa kununua tena bidhaa za kuuza. Unapolazimika kukopesha hakikisha una uwezo wa kufuatilia na kama watu kadhaa watachelewa kukulipa usikose bidhaa za kuzungusha. Hata hivyo, hii sio njia nzuri ya kufanya biashara kwa vile ina changamoto nyingi. 

14.Hakikisha unatunza taarifa ya mapato na matumizi Watu wengi wanaofanya biashara hawana vitabu muhimu. Hata kama mtu hajui vitabu maalum vya masuala ya fedha hapaswi kukosa hata daftari la kumsaidia kujua ameagiza bidhaa gani, ameuza kiasi gani na ametumia kiasi gani, bila kusahau wadeni wake. Usipojua mapato na matumizi ya shughuli yako unaweza kugundua umefilisika ukiwa umechelewa sana. Ni vizuri ugundue mapema mwelekeo wa biashara yako ili uamue kama unaibadilisha wakati bado una fedha au unapunguza gharama za uendeshaji kv umeme, kulipa wafanyakazi nk 

15.Orodhesha bidhaa zako mara kwa mara (stocktaking) Kuna watu tangu wajaze bidhaa kwenye maduka yao hawajawahi kuhesabu na kutambua zipi zinatoka zaidi, zipi zimekaa sana na zimebaki kiasi gani. Madhara ya kutofanya hivyo ni pamoja na kuendelea kuagiza bidhaa ambazo hazitoki, kubaki na bidhaa zilizoisha muda wake, na kukosa fedha za kuagiza bidhaa zingine wakati umejaza dukani bidhaa wasizohitaji wateja wako. Lakini pia unaweza kujikuta unalazimika kuagiza bidhaa nyingi wakati bei zikiwa zimepanda na hivyo kupata faida ndogo au kushindwa kuziuza kwa wakati. Ni vizuri kuweka kumbukumbu pia ya bidhaa ambazo wateja wanaziulizia mara kwa mara ambazo wewe umekuwa huziagizi. Kumbuka walengwa wakuu wa duka lako ni wateja na sio wewe mwenyewe.  ‏

16.Usikae na pesa taslimu. Pesa zako ziwe bidhaa au uziweke katika Akaunti (benki au simu). Ukikaa na pesa taslimu ni rahisi sana kubadili matumizi yake kwa sababu ya dharura na vishawishi mbalimbali. Lakini pia ni rahisi kuzipoteza kwa kuibiwa au kwa majanga mbalimbali. Ni bora kununua bidhaa kwa vile unaweza kuongeza thamini yake pale utakapoziuza. Pia akaunti zinasaidia kuepuka kusafiri na pesa taslimu ili usije ukaibiwa au kuzipoteza. Kipindi tulicho nacho ni rahisi zaidi kwa vile hata pesa zako zilizoko benki unaweza kuzitoa kwa kupitia mtandao wa simu. Hata hivyo ni vizuri kuwa na fedha katika akaunti za benki tofauti na mitandao tofauti ya simu ili usije ukakwama unapohitaji kutoa kwa haraka. Kuna wakati mtandao mmojawapo unaweza kugoma au kuwa kwenye matengenezo. 

17.Epuka gharama zisizo za lazima. Wakati mwingine unaweza kuongeza gharama za uendeshaji wewe mwenyewe. Mfano, unaamua kusafiri kwa gari au daladala wakati unakaa karibu na eneo la biashara au kazi. Kumbuka kutembea pia ni mazoezi mazuri hasa kwa wale ambao muda mwingi wakiwa kazini wanakuwa wamekaa. Au unampigia simu mtu anayekaa nyumba ya pili. Au unamiliki simu tatu wakati hazitumiki kuongea na wateja wanaokuongezea kipato bali zinatumika kwa marafiki ambao unapiga nao tu soga. Jitahidi kwamba gharama za uendeshaji ziwe ndogo iwezekanavyo ili uongeze faida. Jaribu siku moja kutunza kila vocha ya simu unayonunua kwa mwezi mzima. Utalia pale utakapogundua kwamba umetumia pesa nyingi kuliko za chakula na hivyo kusababisha makampuni ya simu yaongeze wafanyakazi wake mishahara wakati wewe mwenyewe unafilisika. Mfano mimi kipaumbele hakijawa kumiliki gari binafsi kwa vile shughuli 4 zinazonihusu ziko jengo hilohilo ninaloishi (nyuma makazi na mbele ofisi) pamoja na jengo lililopakana na nyumba ninayoishi (Hema centre). Hivyo naweza kukaa wiki 2 bila kutoka nje ya eneo na ikitokea ninatoka, naenda mbali sana ambako sio cost effective (ni hasara) kutumia gari binafsi. Hata hivyo jengo jipya ninalojenga mbali likiisha, gari binafsi litakuwa ni hitaji la lazima. 

18.Uza bidhaa zako katika bei rahisi lakini yenye faida ili uvutie wateja Usijaribu kuuza bidhaa zako kwa bei kubwa ili upate faida kwa haraka. Mithali 13:11 anasema ‘Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.’ Kama unauza kila bidhaa kwa sh 5000 na faida unayopata ni sh 1000 kwa kila moja halafu ukauza bidhaa 10, utakuwa na faida ya sh 10,000. Kama utauza kila bidhaa sh 4500 ukapata faida sh 500 kwa kila moja, unaweza kuongeza wateja na kuuza bidhaa 30. Matokeo yake utapata faida sh 15,000. Weka bei ambayo unaweza kumpunguzia mteja kidogo kuliko kuwa na msimamo kwamba imeshapangwa hivyo. Kama ni genge muongeze kidogo bidhaa kv nyanya 2 ili ajisikie vizuri na kurudi tena. 

19.Usile mtaji wako. Uulinde. Jitahidi matumizi yako yaguse tu faida na sio mtaji. Mtu mmoja alipoona kwamba anaingiza sh 50,000 kwa siku katika mauzo yake aliamua kwamba kila siku atoe sh 5,000 kwa ajili ya maandalizi yake ya kujifungua. Matokeo yake duka likafilisika kwa vile hakujua faida ni kiasi gani katika hizo sh 50000 kwa siku. Akala mtaji bila kujua hivyo akashindwa kufungasha tena. Kwa wale waliopata mtaji kwa kukopa wanahitaji uangalifu zaidi kwa vile wanaweza kufilisiwa au kujikuta wanamfanyia kazi aliyewapa mkopo. Wapo watu wanaorejesha faida yote kwa waliowakopesha kwa vile hawajui biashara na mahesabu. Kibaya zaidi hawako tayari kushiriki mafunzo ya ujasiriamali pale yanapotolewa na kama wataitwa kufundishwa wataomba walipwe posho (sitting allowance) kwa vile hawajui ni hitaji lao na hawajui thamani ya mafunzo yanayotolewa. 

20.Epuka maisha ya anasa Mit 21:17 anasema, ‘Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.’ Utajiri hautokani tu na ongezeko la uzalishaji, mauzo na kupata faida kubwa. Matumizi mabaya yanaweza pia kumfilisi anayepata faida kubwa. Nimewahi kushuhudia mtu amepata faida kubwa kisha akaamua kuongeza mke wa pili na kumjengea nyumba wakati mke wa kwanza ana mahitaji makubwa na hayatimizwi kikamilifu. Kibaya zaidi walichuma wote mali hizo. Lakini pia ni vizuri utambue kiwango chako cha maisha bila kushindana na watu wengine ambao hujui njia zao za kipato ni ngapi. Usijaribu kuishi maisha ya mtu mwingine. Be yourself! Mungu ana mpango binafsi na kila mmoja wetu. Umewahi kujiuliza kwa nini alama yako ya dole gumba haifanani na ya mtu yeyote kati ya watu zaidi ya bilioni 6 duniani? Wewe ni wa aina yake (unique). Usipende kuwa photocopy wakati KUNA VITU MUNGU AMEWEKA KWAKO TU. Jitambue na kujithamini ili ufanye makubwa zaidi. Inasemekana ni watu wachache sana duniani ambao wamefaulu kutumia asilimia 10 ya uwezo wao. Wengi wanatumia chini ya hapo. 

21.Usibadili wafanyakazi mara kwa mara. Unaweza kupoteza wateja au kuongeza gharama za uzalishaji. Ni vizuri kuwa na vigezo kamili vya jinsi ya kumpata mfanyakazi atakayekufaa ili kuepuka kubadilisha wafanyakazi mara kwa mara. Kuna wateja wanadumu katika shughuli zako kwa sababu ya mahusiano mazuri waliyoyajenga na wafanyakazi wako. Lakini pia unaweza kumbadilisha mfanyakazi mwenye mvuto mkubwa na kumfanya ahamie katika biashara ya jirani yako na kuondoka na wateja waliokuwa wa kwako. Unaweza pia kuingia gharama kubwa kwa kuajiri wafanyakazi wapya mara kwa mara kwa vile itawachukua muda kufanya kazi zako kwa ubora unaotakiwa. Mwanzoni utakuwa unawalipa kwa kazi ambazo hawazijui vizuri. 

22.Epuka kuhamisha hamisha biashara yako. Unapohamisha biashara unapoteza wateja uliokuwa nao. Hivyo itakugharimu kutafuta wateja wapya. Wakati mwingine itakuwa shida kama huko unakohamia kuna wengine wanaofanya shughuli kama ya kwako au bidhaa zako hazina soko huko. Unapofanya biashara katika mazingira mapya, unakutana na changamoto nyingi ambazo zitachelewesha mafanikio yako. Mojawapo ni utamaduni wa watu husika mfano, wamezoea biashara hiyo ikifanywa na wanawake na sio wanaume. Hivyo itawachukua muda kuamini kwamba mwanaume anaweza kuwapa huduma bora. 

23.Kama hujaajiriwa ifanye mwenyewe ili utingwe ( to keep you busy) Kuna msemo unaosema, ‘Akili isiyotumiwa ni karakana ya shetani’. Shetani hawezi kumtumia mtu ambaye akili yake imejawa na majukumu mengine hasa ya ki-Mungu. Hivyo si busara kazi yako kuwa ni kupanga tu matumizi ya fedha zilizochumwa na wengine wakati wewe mwenyewe ungeweza kuzifanya ili ubaki na faida kubwa zaidi. Ukifanya kazi mwenyewe utajua vizuri gharama za uendeshaji na faida inayopatikana. Matokeo yake utajua vizuri idadi ya wafanyakazi unaowahitaji na uwezo wako wa kuwalipa bila kufilisi bishara yako. 

24. Zalisha bidhaa bora. Kuna watu wanazalisha bidhaa zisizo na ubora halafu wanaziombea ili zipate wateja. Hata Mungu mwenyewe ameonya watu wasidhani kwamba akiwabariki watakuwa hivyo maisha yao yote. Mithali 27:23,24 ‘Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe zako. Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Yadumu tangu kizazi hata kizazi?’ Kama unauza chapatti jitahidi ziwe katika ubora unaotakiwa. Vinginevyo wenzako watauza za kwao ziishe ndipo wateja waanze kununua za kwako. Kama ni icecream, tumia maji yaliyochemshwa wateja wasije wakapata magonjwa na kukukimbia. Kama ni supu, osha vizuri utumbo na kupika uive vizuri usije ukabakiwa na sufuria zima na kurudi nalo nyumbani! 

25.Tangaza biashara yako bila kuona aibu. Utapata wateja wengi kama unaitangaza biashara yako. Kabla hujaingia gharama kubwa ya kuitangaza kwenye magazeti, redio na TV, anza kuizungumzia wewe mwenyewe kwa marafiki, majirani na watu unaokutana nao. Iheshimu kazi yako na kuitangaza kwa kujiamini. Mtu akikuuliza unaendeleaje na biashara yako mf ya kupiga kiwi, usisema, ‘Tunaendelea kuungua jua hapa au tunaendelea kupotea muda hapa!’ Kwa kufanya hivyo, unailaani biashara yako. Furahia unachokifanya na kukitamkia Baraka. Wape watu matumaini ya kufurahia bidhaa zako. Tambua sifa maalum za bidhaa zako ukilinganisha na za wengine. Ukiitangaza vizuri unaweza kushangaa watu wakitoka mbali kuja kupata huduma kwako. 

26.Usifanye shughuli ya ubia (share business) kama huna ujuzi wa kutosha wa aina hiyo ya biashara. Ni kweli kwamba yapo maandiko yanayothibitisha msemo wa ‘Umoja ni nguvu’ kama vile Mhubiri 4:9 ‘Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao’. Hii ina maana kwamba Mungu anapenda ushirikiano. Lakini Biblia hiyohiyo inatutahadharisha tusiwe na umoja bandia. Amosi 3:3 ‘Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?’ Hapa tunapewa swali lisilohitaji kujibu mtu bali ujijibu mwenyewe (rhetorical question). Kuna watu wengi wameporomoka kiuchumi kama sio kulizwa kutokana na ubia ambao sio makini. Afadhali wale ambao biashara zao ni kubwa hivyo wanaingia mikataba ya kisheria kwa kusaini makubaliano (memorandum of understanding or agreement). Kumbuka watu wanabadilisha nia zao kila kukicha. Mnapofanya biashara lazima mzungumzie mtakavyokabiliana na hasara au changamoto za kiuchumi. Hivyo ni bora ukang’ang’ana na biashara yako mwenyewe ili uifanye kwa ufanisi zaidi hadi utakapokuwa na ujuzi wa kutosha kuhusu shughuli za ubia. 

27.Uwe na malengo ya muda mfupi na ya muda mrefu. Wapo watu ambao wanaingia kwenye huduma au biashara lakini hawaweki malengo yoyote ya mbele. Wanaongozwa na kazi zinazojitokeza kila siku. Mtume Paulo hakuwa holela katika huduma yake.1 Kor 9:26 ‘Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa’ Wafilipi 3:14 ‘nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu’. Tuna watu wengi ambao kazi zao ni kama mtu anayepigana ngumi (boxing) lakini hakuna hata ngumi moja iliyompata mwenzake hivyo mwisho anakuwa amechoka kwa kupiga hewa. Paulo alijua anakwenda wapi. Ndiyo maana akafikia mahali akasema, ‘Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda’ (2 Tim 4:7). Ni vizuri kuwa na malengo ya muda mfupi na ya muda mrefu. Hata hivyo muda unategemeana na aina ya shughuli. Malengo yanakusaidia kuona huduma au shughuli yako itakuwaje miaka 5 au 10 ijayo badala ya kushtukizwa na matukio. Malengo ya muda mfupi yanaweza kuwa chini ya miaka 5 na muda mrefu unaweza kuwa kati ya miaka 5 na 10. Lazima utambue umefika umbali gani katika safari yako ili ujipongeze au uongeze mwendo. Bila malengo huwezi kamwe kufanya hayo. Sifa ya malengo bora ni yale ambayo ni SMART (Specific-Yanayolenga kitu maalum, Measurable-Yanayopimika, Achievable-Yanayofikika, Relevant/Realistic-Yenye maana na Time bound-Yenye muda maalum). Kumbuka, MTU ASIYEJUA AENDAKO, HAWEZI KUPOTEA! Kila njia iliyoko mbele yake ni sawa tu. Mtu anayejua amepotea ni yule tu ambaye alikuwa anajua kwamba anakwenda wapi. 

28.Tafuta marafiki waliofanikiwa au wenye maendeleo. Biblia inatuambia kwamba marafiki wabaya wanaharibu tabia njema. 1 Wakorintho 15:33 ‘Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema’. Tafsri ya kingereza iko wazi zaidi, ‘Evil company corrupts good habits’. Siku zote utafanana na aina ya watu wanaoshawishi maisha yako. Hutafikiri kufanya mambo yanayozidi marafiki zako. Marafiki zako wanaweza kuwa kikomo cha fikra zako. Tambua watu wenye akili za mambo fulani na kuwa karibu nao badala ya kuwaonea wivu na kuwasema vibaya. Mithali 13:20 ‘Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia’. Mit 10:14 ‘Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu’. Epuka kupoteza muda na watu ambao hawaongezi kitu kwako bali wanapoteza tu mwelekeo wako. 

29.Fanya kazi kwa bidii. Usitosheke bali uridhike. Acha uvivu, uzembe na kuahirisha mambo. Hakuna mtu amewahi kuwa tajiri bila bidii na kujituma. Wengi waliofanikiwa wanawahi kuamka na kuchelewa kulala pale wanapokuwa na jambo nyeti lenye mafanikio. Mit 21:5 ‘Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji’. Hata hivyo unatakiwa kuridhika ili usije ukaiba. 1 Tim 6:6 ‘Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa’. Lakini usitosheke na maisha uliyo nayo vinginevyo hutaweza kubadili kiwango chako cha maisha. Unaweza kuongeza bidii kama kuna kiwango cha maisha unachotaka kukifikia. Swali la kujiuliza: Je hayo maisha uliyo nayo ndiyo kula mema ya nchi kama Mungu alivyosema? Isaya 1:19 ‘Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi’. Usijitetee kwamba utaishi kwa raha ukiingia mbinguni. Uzuri wa mbinguni tunaanza kuuonja hapahapa. Lazima tuone angalau kwa kioo tukiwa bado duniani. 1 Wakorintho 13:12 ‘Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.’ 

30.Uwe tayari kwa hasara na faida. Hazikwepeki. Usivunjike moyo. Mwa 31: 8-9. ‘Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia. Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi.’ Wakati mwingine Mungu anaweza kumuinua jirani yako zaidi yako. Usiwe na wivu bali utafute mpango wa Mungu kwa ajili yako. Pia ujikosoe kama kuna mahali umetetereka. Lakini pia kuna pandashuka (ups and downs) kwenye biashara. Jifunze kutambua uko kwenye msimu gani katika kalenda ya Mungu. Hata katika misimu ya kawaida kuna vipindi vya joto, baridi na mvua. Kama utaendelea na shughuli yako hiyohiyo moja katika misimu yote lazima ujiandae kwa hasara. Vinginevyo soma nyakati ili ufanye shughuli zinazoendana na mahitaji ya wateja wako. Lakini pia Mungu akileta neema msimu fulani usijisahau ukaongeza matumizi bali uweke akiba kwa ajili ya kipindi kigumu. Mwa 41:35,36 ‘Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.’ 

Ubarikiwe kwa mambo haya 30 muhimu katika mafanikio yako. Lolote likikusaidia usisahau kunipa ushuhuda ili tumshukuru Mungu pamoja kwa kukuvusha na kukuketisha na wakuu.

NB: Kwa sasa kuna Kitabupepe (Ebook) kilichoelezewa kwa kina katika mfumo wa Epub.

Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania