Ticker

6/recent/ticker-posts

Uanafunzi (sehemu ya kwanza)

2 Tim 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine”. Ukweli wa andiko hili ni kwamba si mambo yote yanafaa kufundisha watu wote ibadani au mkutanoni. Lazima tutambue hadhira. Somo hili sio kwa ajili ya wabinafsi wanaotaka kujifunza ili tu wapone magonjwa, wabarikiwe, wainuliwe, wajulikane nk. Yaani mimi mimi mimi (me-ism). Kinyume chake ni kwa ajili ya WATU WAAMINIFU WATAKAOFAA KUWAFUNDISHA WENGINE. I. KANUNI ZA UANAFUNZI Mt 28:19-20 ’Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari’. Maneno haya yanaitwa ‘Agizo Kuu’. Biblia imejaa maagizo mengi lakini hili ni agizo kuu. Kama una shauku kuu ya moyo wa Yesu tambua kwamba agizo hapa ni ‘fanya wanafunzi’ na sio fanya washirika/washarika. Hebu tujiulize kwamba tutalifanyia kazi vipi? Hatua ya kwanza ni kuwaleta kwa Yesu na sio kuwabadilisha tu dini. Kisha lazima tuwasaidie wakue na kuwa wanafunzi wanaomjua Mungu kweli ili nao wawalete wengine kwa Yesu. Kila mkristo anatakiwa ajiwekee utaratibu angalau wa kumleta kwa Yesu mtu mmoja kwa mwaka. Swali ni je tangu umpokee Yesu una miaka mingapi, na wangapi umewaleta kwa Yesu na kuhakikisha wanakua na kuweza pia kuwaleta wengine kwa Yesu? Tumepewa kazi muhimu ya kuwasaidia waamini wengine wakue Efe 4:11-12 ‘Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe. Tukijua kweli ya Neno la Mungu, tunawekwa huru. Yn 8:32 ‘Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru’. Yesu ndiye ukweli huo. Yn 14:6 ‘Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi’. Mtoto mchanga haachwi peke yake ajilishe. Akiachwa peke yake atakufa. Ni kosa kubwa kuzaa watoto hospitalini na kutojali kuwapeleka mahali pa kupata malezi yanayoendana na umri wao. Kwa nini kukua kiroho ni muhimu? Ebr 5:14 ‘Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya’. Tunakua ili tuweze kubeba majukumu makubwa. Umebeba majukumu gani makubwa ili tuseme umekua kiroho? Kama bado kuna mtu umeshindwa kumsamehe, hutoi zaka, humleti mtu kwa Yesu, unachelewa ibada kila wakati, hujishughulishi na huduma yoyote kanisani; unastahili mafundisho ya watoto wachanga. 1 Petro 2:2 Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu. 1.Uanafunzi ni nini? Uanafunzi ni mkristo mmoja kumsaidia mkristo mwingine kukua kiroho na kukua katika uhusiano wake na Yesu Kristo. Uanafunzi ni sawa na stuli ya miguu mitatu. Miguu hiyo ni maombi, uhusiano na mafundisho. Hakuna usalama kama mguu mmoja ni dhaifu. a) Maombi. Yesu anasema kwamba pasipo Yeye hatuwezi kufanya lolote. Yn 15:5 ‘Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote’. Lazima tutumie muda wa kutosha katika maombi tukitafuta msaada wa Mungu na kuombea waamini wapya. Tujifunze kuweka tumaini letu kwa Mungu kuliko kwenye dini au kwa wanadamu. b) Uhusiano. Waamini wapya wanahitaji upendo na urafiki. Wanahitaji mfano mwema wa kuufuata. Fil 3:17 ’Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi’. Lazima maisha yetu yawaonyeshe kile Mungu anachotarajia. Paulo alimwonyesha Timotheo jinsi ya kuishi. Tunahitaji kujifurahisha pamoja nao, kufanya kazi pamoja, kutembea pamoja, kucheka pamoja na kulia pamoja. 2 Tim 3:10,11 ‘Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote’. c) Mafundisho. Waamini wapya wanahitaji mafundisho. Sehemu mojawapo katika ‘Agizo Kuu’ ni mafundisho. Wakristo wapya hawawezi kukua bila mafundisho yenye uzima. Mt 28:20 ‘na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari’. 2.Mwanafunzi ni nani? Mwanafunzi ni mtu anayejifunza zaidi kwa Bwana wake na anayependa kufuata nyayo za Bwana wake na kubadilika akifanana naye. Mwanafunzi ni mtu anayejifunza, anayefuata na anayekua. Rum 12:2 ‘Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu’. Mwanafunzi wa kweli anatafuta kufanana na Yesu kuliko kufanana na dunia. Hebu jiulize kama uvaaji wako, mahusiano yako, matumizi yako na mapato yako yanaakisi (reflect) tabia ya Yesu Kristo. Kanisa la kianafunzi ni kanisa ambalo linawaleta watu kwa Yesu Kristo, na kuwajenga katika imani yao na kuwaandaa wawalete wengine kwa Yesu na kuwajenga katika imani yao. Tusijali sana namba ya waumini tu wakati kati yao hakuna wanafunzi. Watumishi wa kipindi cha Biblia walitofautisha kati ya wanafunzi na makutano ya watu. Somo hili litaendelea…..