Ticker

6/recent/ticker-posts

Muombee mtumishi anayekuongoza

MUOMBEE MTUMISHI ANAYEKUONGOZA

Kwa kipindi sasa nimekuwa nikiombea watumishi wa Mungu waijue kweli na kuisimamia katika makanisa yao na Mungu afungue milango ya kufanya semina ambazo hazina ubaguzi wa kimadhehebu kwa ajili yao.

Maono: Usiku wa kuamkia jana niliona yakitajwa matatizo matatu ya wachungaji. La kwanza, hawajui majukumu yao ya msingi. La pili, hawajui kugawa madaraka na la tatu, wameacha kazi zao na kufanya kazi za wengine. Niliona wengine wakifanya kazi za mashemasi.

Maono haya hayana maana kwamba wachungaji wote wana mapungufu hayo. Ila Mungu anatuonyesha maeneo ambayo yanahitaji msaada ili watumishi wafanye kazi waliyoitiwa itakayowafanya wapate thawabu na kuwa na matokeo chanya katika huduma zao.

Napenda kuzungumzia mapungufu hayo matatu. Mwongozo huu unaweza kuwasaidia hata wale ambao ni viongozi wanaosimamia familia na taasisi mbalimbali.

1. Hawajui majukumu yao ya msingi

Kuna watumishi ambao hawajui majukumu wala mipaka ya kazi zao. Anatumika kwa dharura kulingana na mahitaji yanayojitokeza. Hana ratiba kwamba leo atafanya kazi gani na kesho ataanza na kazi ipi. Anapohubiri au kutumika hana lengo wala shabaha. Anahubiri kwa kufurahia na kusisimka lakini hana lengo maalum. Haijulikani kama anahamasisha, anafurahisha, anatafuta mabadiliko fulani yatokee au anataka watu wafikie hatua fulani. Biblia imeonyesha kusudi na lengo la Mungu kuita watumishi wake.

Makusudi hayo ni kukamilisha watakatifu, kazi ya huduma itendeke na mwili wa Kristo ujengwe. Kiwango cha juu tunachotakiwa kulifikisha kanisa ni KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU NA KUFIKIA CHEO CHA KIMO CHA UTIMILIFU WA KRISTO. Efe 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”

Mungu alipoita watumishi wake aliwapa maelezo ya kazi (Job Description) na namna ya kujitathmini (self-evaluation). Mfano, mtume Paulo alijui vizuri ameitiwa nini na anatarajiwa kuleta matokeo gani. Mdo 26:18 “uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.” Mungu alichotaka kwake sio kupewa jina au wadhifa fulani bali aone watu wakifunguliwa na kumuacha shetani, wamgeukie Mungu na kupokea msamaha na urithi wao kutoka kwa Mungu. Mara ngapi tumejitathmini kwamba ni wangapi wamefanyiwa mambo hayo kupitia huduma zetu? Tunaendelea kuhubiri na kuimba lakini wengi tunaowahudumia bado wamechoka na kukata tamaa na hatujali wala kujihoji.

2. Hawajui kugawa madaraka

Kuna watumishi wanafanya kila kazi wenyewe. Wamehodhi madaraka. Ingawa mtumishi ameteua au ana viongozi wasaidizi chini yake, wapo kama mapambo au vivuli tu lakini hawaamini na kuwaachia majukumu. Bado watu wanamuendea kwa kila aina ya tatizo. Tena kiongozi mwingine anapoona watu wamepunguza kumuona kutokana na kazi nzuri ya wasaidizi wake, anakasirika na kuwasema vibaya hadharani. Kutokana na hofu hii anashindwa hata kusafiri na kuwaacha wasaidizi wakiendeleza huduma. Watumishi wa aina hii sio wa kwanza kutokea duniani. Kipindi cha Biblia Musa alipoitwa alikuwa pia na mtazamo huu ambao ungemdhoofisha na kukwamisha huduma yake nzuri. Kwa vile Mungu anatumia watu, Musa alishauriwa na mkwe wake achague watu wenye sifa ili washughulikie mambo madogo na yale makubwa ndiyo wamletee. Kutoka 18:17-22 “Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema.Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako….Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe.”

3. Wameacha majukumu yao na kufanya ya wengine  

Mtumishi wa Mungu anaweza kuitwa Mchungaji au Kasisi lakini kazi anazofanya ni za mashemasi. Jambo hili linaleta mgongano na manung’uniko mengi. Mitume walikutana na changamoto hii wakaanzisha ushemasi mara moja ili wasitoke kwenye lengo kuu la kitume ambalo ni MAOMBI na NENO. Mdo 6:3,4 “Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.” Watumishi wengine hawana nafasi hata ya kusifu na kuabudu ibadani wala hawawezi kushiriki vipindi vya maombi. Wanazurura tu muda wa ibada wakati wengine wakiendelea kumsifu Mungu. Tukifika hatua ya kutingwa na kazi za ofisini na kuacha NENO na MAOMBI tumeshatoka kwenye wito tulioitiwa. Tunatakiwa kuwaandaa watu wafanye kazi za ofisi ili tuendelee na wito wetu wa msingi. Sijui kazi zako ni zilezile za wito ulioitiwa au umeziacha na kufanya za watu wengine?

HITIMISHO

Katika mwili wa Kristo (Kanisa) mifupa (skeleton) ni uongozi na nyama (flesh) ni waumini. Ukuaji wa mwili wenye afya unahitaji maeneo yote (mifupa na nyama) yakue kwa uwiano sawa. Wengi tunasisitiza sana kanisa likue kiidadi na kusahau ukuaji wa uongozi. Matokeo yake tunakuwa na watu wengi makanisani lakini hawamjui Mungu, hawajui kuomba, hawafanyi huduma yoyote, wamechoka kiroho na wametawaliwa na dhambi. Kazi yao kubwa ni kutoa tu sadaka na zaka na kutarajia kuombewa na kutabiriwa. Watu wa aina hii hata kama ni wengi wanaitwa washirika/washarika na sio wanafunzi kama tulivyopewa Agizo Kuu. Washirika/washarika WANAJIUNGA NA KANISA lakini wanafunzi WANAFANYWA/WANATENGENEZWA. Sijui kama kwa vigezo hivi tuna wanafunzi wangapi mpaka sasa makanisani. Mathayo 28:19 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.”

Kiongozi pia anatakiwa kukua kama anataka kuwa na wanafunzi badala ya washirika/washarika. Kiongozi anapitia hatua kama za kwenye timu ya mpira (Mchezaji, nahodha, kocha, meneja). Huduma inapoanza mchungaji anafanya kazi zote pamoja na waumini kama MCHEZAJI. Baada ya muda anatakiwa kubadilika na kuwa NAHODHA WA TIMU. Hapa anaendelea kucheza lakini pia ni kiongozi. Ni kama monita anavyoongoza wenzake darasani wakati yeye pia ni mwanafunzi.  Hatua inayofuata ya kiongozi anakuwa KOCHA. Hachezi uwanjani lakini lazima awaandane wachezaji kwenye mazoezi na na kuwafuatilia uwanjani. Hatua ya juu kama kiongozi ni kuwa MENEJA WA TIMU. Anaweza kutokuwepo uwanjani kama alivyo kocha lakini mambo yanaenda kwa vile amewaandaa wengine. Kwa hiyo sasa anapanga mipango ya kuboresha timu, maslahi ya wacheza nk. Nimekutana na wachungaji wenye makanisa makubwa lakini kiuongozi hawajakua kabisa matokeo yake kazi wanazofanya haziendani na idadi ya watu wanaowasimamia. Mchungaji asipojua kuwaandaa vizuri waumini kwa ajili ya huduma atashangaa wakichangia tu sherehe na burdani zao na kusahau kabisa kazi ya Mungu. Mchungaji anaweza kulalamika lakini ukweli ni kwamba amepungukiwa ujuzi wa uongozi. Mfano, kanisa lina waumini wengi lakini mchungaji ndiye anaenda kuchukua barua za kanisa posta, kupanga viongozi wa sifa, kushauri baada ya ibada kwa masaa mengi na tena watu wanamuona kwa matatizo ambayo yangeshughulikiwa na wasaidizi wake nk

Maombi:

1. Ee Mungu naomba uwasaidie wachungaji watumike katika viwango vyako ili wafikie kusudi na malengo yako.

2. Ee Mungu naomba unisaidie nisimame katika nafasi yangu kama mwanafunzi wa Yesu na sio mshirika/msharika tu wa kanisa.

3. Ee Mungu naomba ufungue milango ili watumishi wako wapatiwe mafunzo ya mara kwa mara ya uongozi ili amani yako itawale katika huduma ulizowapa.

Lawi Mshana