
Ufufuo wa Yesu ni tukio muhimu sana katika maisha yetu.
Kama Bwana Yesu hangefufuka, Ukristo wetu haungekuwa na maana. Na kama tunaitwa
Wakristo kwa ajili ya maisha ya hapa duniani peke yake kuna mambo mawili ya
kutafakari:
(1). Sisi ni maskini kuliko watu wote. 1 Kor 15:19 “Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu
maskini kuliko watu wote.”
(2). Maana ya kuabudu na kujitakasa itakuwa haipo. 1 Kor 15:32 “…..Wasipofufuliwa wafu, na
tule, na tunywe, maana kesho tutakufa.”
Sasa basi, kama tunaamini kuna maisha mengine tena halisi
kuliko haya, tunahitaji kutakaswa na damu ya Yesu. 1 Yohana 1:9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki
hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” Kuungama ni
kukiri au kukubali kwamba umemkosea Mungu na sio kukariri maneno na kuyarudia mara
kwa mara.
Hata hivyo wengi bado hatujanufaika na nguvu ya damu ya
Yesu kwa vile hatujui kama tumechafuka na wala hatujui kama kuna uwezekano wa
kusafika. Lazima uwe na tafsiri sahihi kuhusu uchafu wa mwili, nafsi na roho na
namna uchafu huo unavyoweza kuondolewa. 2 Kor 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi
zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha
Mungu.”
Ayubu
anaomba kwamba Mungu amjulishe dhambi yake:
Ayubu 13:23 “Maovu
yangu na dhambi zangu ni ngapi? Nijulishe kosa langu na dhambi yangu.”
Bila kumruhusu Roho Mtakatifu atusaidie hatutaweza kutambua
dhambi zetu. Kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kutufanya tujisikie hatia
tunapokuwa tumetenda dhambi (convict). Yohana 16:8 “Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi,
na haki.” Bila Roho Mtakatifu tutaendelea kutetea dhambi na mwisho
zitatupeleka pabaya.
Lakini pia Neno la Mungu lililo hai linachoma na kumfanya
mwenye dhambi ajitambue na kuchukua hatua. Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko
upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na
viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na
makusudi ya moyo.”
Neno la Mungu linachoma kuliko sime na kuweka wazi mawazo
na makusudi ya moyo. La kusikitisha wengine wanapochomwa na Neno wanatafuta
mapungufu ya mhubiri ili waweze kujitetea. Wakati huohuo wengine wakichomwa na
Neno wanaanguka mbele za Mungu kwa machozi na kuchukua hatua za mabadiliko.
Sishangai kwa vile hata kipindi cha Biblia watu ‘walipochomwa
mioyo’ waliitikia kwa namna mbili tofauti:
1. Kundi la kwanza ni la wale ambao walihitaji msaada zaidi
ili wapone
Mdo 2:37 “Walipoyasikia
haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje,
ndugu zetu?”
2. Kundi la pili ni la wale ambao walipinga na kuamua
kumuua mhubiri
Mdo 7:54,58 “Basi
waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi
wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.”
TAHADHARI
1. Usipende kujifariji wakati njia zako hazikubaliki mbele
za Mungu. Usisahau kwamba hata wanaokufariji kwamba uko sawa hawajawahi kwenda
mbinguni. Usichague maneno ya kusikiliza kwa vile tu unayapenda. Mungu
atahukumu kwa kutumia Biblia na sio utashi binafsi wa wahubiri.
Mithali 16:25 “Iko
njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”
2. Usipoangalia utakuwa kibao cha kuongoza wengine wakati
wewe mwenyewe huendi mbinguni. Hakuna kibao kinakwenda kule kinakoelekeza watu
ingawa kimesaidia wengi kufika. 1 Kor 9:27 “bali
nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine,
mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”
3. Usidhani kila mahali panafaa kujitakasa. Fanya uchaguzi
mzuri wa kanisa la kuabudia. Huwezi kujitakasa wakati uko na watu ambao uchafu
ni kawaida ya maisha kwao. Wanatenda dhambi kwa makusudi kabisa.
2 Wakorintho 6:17,18 “Kwa
hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho
kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu
wanangu wa kiume na wa kike.”
Uwe makini usilishwe matango mwitu badala ya Neno la Mungu. Usiwaze kuwasaidia wengine wakati wewe mwenyewe huko salama. Jali kwanza usalama wa roho yako. 2 Fal 4: 39,40 “Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtango-mwitu, akayachuma matango-mwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasua-pasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua. Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula.”
Linda sana moyo wako kuliko yote ulindayo. Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo;
Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.”
Lakini pia uwe na kiasi katika sikukuu hii ukizingatia
kwamba katika Agano Jipya hatukuagizwa kuikumbuka siku ya Pasaka bali
kumkumbuka Bwana Yesu ambaye ndiye Pasaka wetu. Bwana Yesu mwenyewe ametuagiza
kwamba tumkumbuke kwa kushiriki meza ya Bwana. Hivyo Bwana Yesu awe kipaumbele
chetu kuliko siku yenyewe ingawa hatukatazwi kusherehekea.
1 Kor 5:7 “Basi,
jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile
mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka,
yaani, Kristo.”
1 Wakorintho 11:23,24 “Kwa
maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule
aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio
mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
Maombi:
1. Ee Mungu naomba unijulishe dhambi yangu ili nisijifariji kumbe nakukosea.
2. Ee Mungu naomba unipe hofu yako
ninaposikiliza Neno lako. Nisichague neno ninalotaka kusikia kwa sababu ya
kiburi.
3. Ee Mungu naomba unifunulie watu
ninaotakiwa kujitenga nao na nisiguse vitu vichafu ili niwe mwanao.
Lawi Mshana