
Maono: Nimeona
mtu akionyeshwa mipaka ya shamba lililokuwa la baba yake na kutakiwa kufika
mpaka juu mwisho ili akapate maelekezo zaidi. (Hii ina maana kwamba unatakiwa
kujua vizuri mipaka ya urithi wako lakini pia ufike mahali ambapo unapata
maelekezo ya kina).
Lazima kila mmoja wetu atambue kwamba urithi hauwi wa kwake
kwa sababu tu mzazi wake ameondoka duniani. Kuna mambo muhimu ya kufanya.
Vinginevyo hatanufaika na urithi huo.
1.
Lazima utafute kukua ili uwe na sifa za kupewa urithi
Wagalatia 4:1,2 “Lakini
nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa
ni bwana wa yote; bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati
uliokwisha kuamriwa na baba.”
Hata Bwana Yesu aliitwa MWANA alipofikia umri unaofaa.
Hakuambiwa hivyo akiwa MTOTO MDOGO. Mathayo 3:17 “na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa
wangu, ninayependezwa naye.”
2.
Tambua aina ya urithi wako (wewe sio mrithi wa kila eneo)
Urithi wa wana wa Lawi ulikuwa zaka kwa vile walikuwa
wanafanya huduma ya madhabahuni. Lakini nao hawakupewa urithi wa mashamba.
Kama mtu yuko katika mchepuo
wake wa utumishi ataziona baraka za Mungu. Akiacha wito wake na kufanya
kazi ambazo hakuitiwa, anaweza kuwa na maisha magumu hata kama wengine
wanafanikiwa katika eneo hilo.
Hesabu 18:21,23 “Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania. Lakini Walawi watatumika utumishi wa hema ya kukutania, nao watauchukua uovu wao; hii itakuwa amri ya milele katika vizazi vyenu vyote, na kati ya wana wa Israeli hawatakuwa na urithi.”
3. Usijione kwamba umechelewa au hustahili urithi wako
Kalebu aliahidiwa urithi wake akiwa na miaka 45, akadai haki yake na kuipata akiwa na miaka 85. Hujachelewa wala hujazeeka. Dai kilicho chako.
Yos 14:10-13 “Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu. Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani. Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena. Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.”
4. Utarithi kulingana na juhudi yako katika kumiliki
Kuendelea kusema mimi ni mtoto wa Mfalme wakati hutumii nguvu na vipawa ulivyopewa kutakufanya uendelee kuwa msimuliaji wa maono lakini kamwe hayatakuwa na matokeo halisi.
Yos 17:14-18 “Kisha wana wa Yusufu wakanena na Yoshua, wakasema, Kwa nini umenipa
mimi kura moja tu na fungu moja kuwa ni urithi wangu, kwa kuwa mimi ni taifa
kubwa la watu, kwa sababu Bwana amenibarikia hata hivi sasa? Yoshua akawaambia,
Kwamba wewe u taifa kubwa la watu, haya, kwea uende mwituni, ujikatie mahali
hapo kwa ajili ya nafsi yako katika nchi ya Waperizi, na ya hao Warefai; ikiwa
hiyo nchi ya vilima ya Efraimu ni nyembamba, haikutoshi. Wana wa Yusufu
wakasema, Hiyo nchi ya vilima haitutoshi sisi; lakini Wakanaani wote wakaao
katika nchi ya bondeni wana magari ya chuma, hao walio katika Bethsheani na
miji yake, na hao walio katika bonde la Yezreeli pia. Kisha Yoshua alinena na
nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa
la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata kura moja tu; lakini hiyo nchi ya
vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa ni mwitu, wewe utaukata, na matokeo
yake yatakuwa ni yako; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, wajapokuwa wana
magari ya chuma, wajapokuwa ni wenye uwezo”
MAOMBI
1. Ee Mungu naomba uniwezeshe kukua
nifikie kiwango ambacho nina sifa za kumiliki milki zangu.
2. Ee Mungu naomba unijulishe urithi
wangu ili nising’ang’anie urithi wa watu wengine.
3. Ee Mungu naomba unipe nguvu na
ujasiri wa kudai na kumiliki urithi ulionipangia.
Lawi Mshana