
Maono: Tukiwa
katika maombi Ijumaa nilipata ujumbe kwamba kuna mtu anajitahidi kudai vitu
ambavyo hujaahidiwa na Mungu. Kila ahadi ina kanuni na masharti yake. Mfano,
huwezi kudai ahadi ya kujazwa Roho Mtakatifu wakati bado hujampokea Yesu kama
Mwokozi wako.
Utangulizi
Watu wengi tunapenda kudai ahadi za Ibrahimu lakini
hatujiulizi kama tunafanana na utii wake kama watoto wake. Tutaangalia maandiko
ili tujifunze maisha ya Ibrahimu yalivyokuwa ili tufanyie kazi mapungufu yetu
na kupokea ahadi zetu kwa wakati.
Mwa 18:16-24, 32-33
1. Ibrahimu alikuwa mkarimu kwa watu asiowajua
Ukarimu huu ulisababisha aalike malaika wenye majibu ya maombi yake ya muda mrefu. Hakuwa na tabia ya wengi ya kujali watu wanaowajua tu.
Mwa 18:2-4 “Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu.”
Watu hawa ambao walikuwa ni malaika walitoa tamko la majibu yake. Mst wa 10 “Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume.”
Neno la Mungu linatukumbusha umuhimu wa kukaribisha wageni kwa vile wengine ni malaika wenye majibu yetu. Kuna mahitaji hayahitaji kuwekewa mikono na watumishi bali yanahitaji ukarimu wa wageni ili watoe tamko la mafanikio. Waebrania 13:2 “Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.” Tuache tabia ya kupuuza watu maofisini na nyumbani. Hata kama tuna shida, tusikwepe kupokea wageni. Tukiwajali kazi zetu zitabarikiwa.
2. Ibrahimu aliwasindikiza wageni akapata siri za Mungu
Mst 16-23 “Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize. Bwana akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana, wafanye haki na hukumu, ili kwamba Bwana naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake. Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo?
Nimejifunza
mambo kadhaa kwa Ibrahimu:
1. Ukarimu wake haukuishia nyumbani bali
aliwasindikiza wale wageni (alijenga mahusiano nao)
2. Aliipata siri kubwa akiwa njiani na hao
wageni (hawakuguswa kumwambia siri hiyo wakiwa nyumbani)
3. Wale malaika walitoa sababu ya
kumjulisha Ibrahimu kuhusu hukumu wanayoipeleka Sodoma na Gomora. (1).
Anatarajiwa kuwa taifa kuu, hodari, (2) Atakuwa baraka kwa mataifa yote ya
dunia (3) Atawaamuru wanawe na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana,
wafanye haki na hukumu, (4) Ibrahimu akitimiza hizi sababu walizotoa, BWANA
NAYE ATAMTIMIZIA AHADI ZAKE.
4. Alikuwa mwombezi – alisimama mahali palipobomoka kwa ajili ya wengine ili wasiangamizwe. Alimsihi Mungu mpaka akahakikishiwa kwamba kama Mungu atapata wenye haki 10 hatawaangamiza wanadamu.
Swali la kujihoji: Unamfanania Ibrahimu ili upokee ahadi zake kama mwanae, mjukuu, kitukuu, kilembwe nk?
3. Ahadi
za Mungu zikoje?
2 Kor 1:19-20 “Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, yaani, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika yeye ni Ndiyo. Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi.”
Yak 1:17 “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”
MAOMBI
1. Ee Mungu nipe roho ya ukarimu kwa wageni na kuniletea
wageni sahihi wenye baraka zangu ili nipokee ahadi zangu.
2. Ee Mungu niwezeshe kujenga mahusiano yenye tija na
wageni na marafiki ili ninufaike na siri walizo nazo za kunisaidia maishani.
3. Ee Mungu nijulishe ahadi ulizonipangia ili nisije
nikapoteza muda kuomba ahadi za watu wengine ambazo hujanipangia.
Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania