
Maono: Nimeona
mtu akipewa kitu fulani ambacho alidhani ni dawa ya kumsaidia. Alipoichanganya
na chakula, pakatokea wadudu wengi wakala chakula karibia chote. Akawa hana
namna. Akajaribu kutafuta dawa ya kupuliza ili kuwaua hao wadudu, akashindwa
kuitumia kwa vile dawa hiyo itakuwa ni sumu kwenye chakula chake. Wadudu hao
walikula chakula mpaka wakaondoka wenyewe ghafla.
Maana
ya maono haya:
1. Kuna watu wa karibu na wewe ambao ni chanzo cha matatizo
yako ingawa wanajifanya kama wanataka kukusaidia,
2. Una haraka ya kutumia vitu unavyopewa bila kumuomba
Mungu kwanza,
3. Matatizo uliyo nayo yako juu ya uwezo wako hivyo lazima
utafute msaada kwa watumishi wenye mamlaka (uchawi unahusika katika vita zako).
Utangulizi
Mungu wetu anataka tuwe na ushirika wa karibu lakini katika
ushirika huo kuna uwezekano mkubwa wa kusalitiwa na baadhi ya marafiki. Huwezi
kusalitiwa na mtu ambaye hakujui vizuri na hajui njia zako. Lazima msaliti awe
mtu ambaye akizusha jambo kuhusu wewe anaaminika kwa vile watu wanajua yuko
karibu na wewe. Hata Bwana Yesu alisalitiwa na mwanafunzi wake wa karibu sana.
Mathayo 26:25 “Yuda, yule mwenye
kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.”
Nitatumia Zaburi 55:1-23 katika kukuandaa kwa ajili ya
maombi ya wiki hii. Omba kwa kumaanisha.
1. Mwite
Mungu kwa maombi
Mst 1,2,16,17 “Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema. Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga nikilalama na kuugua. Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa; Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti yangu.”
Usitumie silaha za kimwili kupambana na adui yako. Kimbilia kwa Bwana. Usiwe na maombi ya msimu na wala usiombe kwa kukata tamaa. Luka 18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.”
2.
Tambulisha vizuri tatizo lako
Mst 3,20,21 “Kwa sababu ya sauti ya adui, Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu. Kwa maana wananitupia uovu, Na kwa ghadhabu wananiudhi. Amenyosha mkono awadhuru waliopatana naye, Amelihalifu agano lake. Kinywa chake ni laini kuliko siagi, Bali moyo wake ni vita. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, Bali hayo ni panga wazi.”
Tambua vizuri ukubwa wa tatizo lako ili uwe na hoja zenye nguvu. Isaya 41:21 “Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.” Usijikanyage wala kupayuka katika maombi yako mbele za Mungu.
3. Eleza vizuri tatizo hilo lilivyokuathiri
Mst 4,5 “Moyo wangu unaumia ndani yangu, Na hofu za mauti zimeniangukia. Hofu
na tetemeko limenijia, Na hofu kubwa imenifunikiza.”
Acha unafiki wa kujifanya huna tatizo mbele za Mungu. Jianike na kujiweka uchi mbele za Mungu ili akusaidie. Yesu ni wakili (mwombezi) katika kesi yako. Mueleze umeathiriwa kiasi gani. 1 Yohana 2:1 “….. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki”
4. Eleza
hatua mbayya unazotamani kuzichukua
Mst
6-8 “Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama
njiwa, Ningerukia mbali na kustarehe. Ningekwenda zangu mbali, Ningetua
jangwani. Ningefanya haraka kuzikimbia Dhoruba na tufani.”
Kama unatamani kufa au kujiua, mueleze Mungu ili akurehemu na kukusaidia. Pengine unatamani kuachana naye, kuacha kazi, kutoroka nk. Usikimbie tu bali mueleze Mungu atakupa mlango wa kutokea katika jaribu lako hata kama unadhani tatizo lako ni kubwa sana. Ayubu 34:6 “Nijapokuwa mwenye haki, nimehesabiwa kuwa mwongo; Jeraha yangu haiponyeki, nijapokuwa sina makosa.”
5. Muombe
Mungu aharibu mipango ya maadui
Mst 9-11,15 “Ee Bwana, uwaangamize, uzichafue ndimi zao, Maana nimeona dhuluma na
fitina katika mji. Mchana na usiku huzunguka kutani mwake; Uovu na taabu zimo
ndani yake; Tamaa mbaya zimo ndani yake; Dhuluma na hila haziondoki mitaani
mwake. Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu
u makaoni mwao na katikati yao.”
Hii sala aliiomba kabla ya kipindi cha neema ya Yesu Kristo. Hivyo usimuombee afe au aende kuzimu. Omba kwamba afundishwe kwa namna ambayo atajua yuko Mungu na wewe ni mtu wa Mungu. 1 Timotheo 1:20 “Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.”
6. Kubali kwamba rafiki wa leo anaweza kuwa adui wa kesho
Mst 12-14 “Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia.
Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione.
Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana
shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.”
Kubali kwamba wewe sio wa kwanza kusalitiwa na mtu ambaye ulimuamini sana na mlishirikishana mambo mengi tena mpaka mambo ya kiroho. Usiruhusu kukata tamaa. Mara nyingi adui za mtu ni watu wa karibu na yeye. Mathayo 10:36 “na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.”
7. Weka tumaini lako kwa Mungu
Mst 18-23 “Ameiokoa nafsi yangu iwe salama, asinikaribie mtu, Maana walioshindana nami walikuwa wengi. Mungu atasikia na kuwajibu; Ndiye Yeye akaaye tangu milele. Mageuzi ya mambo hayawapati hao, Kwa hiyo hawamchi Mungu. Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele. Nawe, Ee Mungu, utawatelemsha, Walifikilie shimo la uharibifu; Watu wa damu na hila hawataishi nusu ya siku zao, Bali mimi nitakutumaini Wewe”
Mungu hatakuacha kama u mwenye haki. Jipeleleze kama kuna maeneo na wewe umedhulumu watu ili shetani asipeleke mashitaka yanayozuia maombi yako. Lipa watu haki zao kv mshahara wa msichana wa kazi, ahadi zako kanisani, fungu la kumi nk. USIPELEKE MASHITAKA POLISI AU MAHAKAMANI WAKATI WEWE MWENYEWE UNATAFUTWA KWA MAKOSA YAKO MENGINE ULIYOFANYA!
Maombi
Tumia vipengele maombi haya nilivyokupatia katika kumuomba Mungu akupe ushindi katika hali yako ngumu unayopitia.
Hata hivyo kungaliko tumaini katika hili
tatizo lako. Ezra 10:2 “… Sisi tumemkosa
Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko
tumaini kwa Israeli katika jambo hili.”
Lawi Mshana