
Maono:
Mungu anataka kukurudishia muda na vitu ulivyopoteza kama unaamini na kuchukua
hatua ya imani.
Nitatumia Yoeli 2:12-27 kukupa mwongozo wa kukusaidia
1.
Mrudie Mungu kwa moyo wako wote (kwa toba ya kweli)
Mst wa 12-14 “12 Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; 13 rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya.14 N'nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu?”
Inawezekana umekuwa ukimkemea shetani kwa muda mrefu na huoni matokeo chanya. Wakati mwingine vita yako haitoki moja kwa moja kwa shetani, bali umepishana na Mungu. Una tatizo na Mungu. Jitiishe kwanza kwa Mungu ndipo ukimpinga shetani atakimbia. Shetani anamuogopa mtu mwenye uhusiano wa karibu na Yesu. Yakobo 4:7 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.” Lakini pia inawezekana unafanya maombi mengi ya mazoea. Safari hii unahitaji KUFUNGA, KULIA NA KUOMBOLEZA. Kufunga ni kuacha vitu vya kujifurahisha kwa ajili ya Mungu, kulia ni kuthibitisha kwamba hali hiyo inakuumiza na kuomboleza ni kuelezea msiba wako kwa Mungu. Maombi ya kufunga sio kushinda njaa na kuhesabu masaa. Ukifanya hivyo unaweza kupata vidonda vya tumbo. Usikae katika mabaraza ya wenye mizaha. Kama umechoshwa na hali yako lazima utapata machozi. Hutaomba maombi ya ukame. Tatizo lako likifikia hatua ya kuliona ni MSIBA, utaomboleza na kuweka kando heshima yako na ustaarabu wako. Hutaangalia na wala hutajali nani anakutazama ukiomboleza. Ukifanya hivyo, Mungu atageuka na kujibu haja ya moyo wako.
2. Watu wa karibu na wewe wahusike pia (asiwepo mtazamaji katika vita)
Mstari wa 15-16 “Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake.”
Kuna watu wanapenda sana kuombewa halafu wao wenyewe wanastarehe. Sio mpango wa Mungu kwamba wewe uwe mtazamaji katika vita vya kiroho. Unahatarisha maisha yako. Lakini pia unakuwa mzigo kwa wengine. Lazima familia au watu wa karibu na wewe wahusike pia katika maombi kwa kadiri wanavyojaliwa na Mungu. Andiko hili linaonyesha kwamba Mungu hataki mtu ajitetee kwamba yeye ni mzee, mtoto, bwana arusi au bibi arusi. Kutokana na uzito wa tatizo hata maharusi waache starehe waende kumlilia Mungu. Tusimtafute Mungu kwa dharura bali kwa makusudi ndipo tutamuona akitenda makuu. Dan 11:32b “lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.”
3. Hakikisha uko chini ya kuhani sahihi wa Mungu ili atamke KUACHILIWA
Mstari wa 17-18 “Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao? Hapo ndipo Bwana alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.”
Hapa sizungumzii mtumishi anayejiita
kuhani bali mtumishi aliyeitwa na Mungu anayeweza kusimama kati yako na Mungu
ili ALIE KATI YA PATAKATIFU NA MADHABAHU KWA AJILI YA KUACHILIWA KWAKO.
Kuna watumishi wanatimiza tu wajibu wao siku na saa za ibada lakini baada ya hapo hawana muda wowote wa maombi. Mtu anaweza kuwa kiongozi wa ibada na asiwe na machozi wala mzigo kwa ajili ya mapito yako.
Biblia inatambua kwamba kuna matatizo ambayo yanazidi uwezo wa muumini hivyo anahitaji kuwapelekea makuhani (kama mtu wa kwenu hawezi). Hata hivyo yale ambayo yako ndani ya uwezo wake ayafanyie kazi mwenyewe (kama amepatikana na mabaya). Yak 5:13,14 “Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.”
Nini kitatokea hatua hizi zikichukuliwa?
1. Bwana ataona wivu na maisha yako na
kukuhurumia (Mst 18 “Hapo ndipo Bwana
alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.”)
2. Bwana atakulisha na kukushibisha na
hutadhalilika tena (Mst 19 “…Tazameni,
nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala
sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa.”)
3. Bwana atawafukuza mbali aduiu7 zako
na kuondoa kibali chao/watanuka (Mst 20 “lakini
jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka
nchi ya ukame na ukiwa;… na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya
itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.”)
4. Miradi na kazi zako zitakuwa na faida
tele (Mst 21-24 “….na huo mti unazaa
matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake.…Na sakafu za kupepetea
zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.”)
5. Bwana atakurudishia muda uliopotea
(Mst 25 “Nami nitawarudishia hiyo miaka
iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa
nililotuma kati yenu.”)
6. Utakula na kushiba (Mst 26 “Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na
kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu
wangu hawatatahayari kamwe.”)
7. Utamjua Mungu na kumuabudu Yeye peke Yake (Mst 27 “Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe.”)
MAOMBI
1. Ee Mungu nipe moyo wa nyama na hofu
yako ili nitetemeke mbele zako na kuwa na toba ya kweli.
2. Ee Mungu tusaidie familia nzima
tukupende na kukuabudu katika roho na kweli.
3. Ee Mungu nifungue macho nimtambue
kuhani mwenye funguo za vifungo vyangu ili niwe huru.
4. Ee Mungu naomba unirudishie muda
niliopoteza na fedha nilizopoteza
5. Ee Mungu naomba nile na kushiba na kukuabudu Wewe peke yako, na nisitahayarike tena.
Mungu akujibu maombi yako kupitia Jina
la Uweza la Yesu Kristo.
Lawi Mshana