
Maono: Nimeona watu wanapita katika mazingira hatarishi
sana na wanahitaji Mungu awafiche ili wasipate madhara
Kuna wakati unagundua kwamba pamoja na juhudi zako katika
mambo mengi umepungukiwa na ulinzi wa Mungu. Tunahitaji ulinzi katika maeneo
yote ya maisha yetu – nyumbani, safarini, kazini, miradini, katika huduma nk
Zaburi 121:8 “Bwana atakulinda utokapo
na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.”
SASA TUFANYEJE?
1. Tujifunze kukaa chini ya mbawa za Bwana
Zaburi 91:1-4 “1 Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. 2 Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. 3 Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. 4 Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.”
Wakati mwingine ingawa tunalitaja jina la Bwana tukiimba, tukisifu na tukiomba, hatumtumaini kama tunavyowatumainia wanadamu au kazi zetu. Wakati mwingine tunapokuwa na uhitaji tunamuomba Mungu lakini kichwani tunawaza kwenda kumuomba mtu fulani atusaidie. Sio vibaya kuomba msaada wa mtu lakini tunapokuwa magotini katika MAOMBI mbele za Mungu tusahau kuwa OMBAOMBA. Kama Mungu anataka tukapate msaada kwa mtu fulani tusubiri aanzishe yeye lakini tusimuendee wakati tayari tumeshapanga majibu. Tujiandae na kumuacha apange yeye. Tuketi mahali pa siri pake Mwenyezi. Mithali 16:1 “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.”
Kama vifaranga vinavyotulia chini ya
mbawa za tai, Mungu wetu awe KIMBILIO – hakika hatutaaibika. Zaburi 37:19 “Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za
njaa watashiba.”
2. Tujifunze kumtaja Bwana kuliko shida zetu na nguvu zetu
Zaburi 23:1,4 “Bwana
ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Naam, nijapopita kati ya bonde la
uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na
fimbo yako vyanifariji.”
Tunakwama kwa vile tunachanganyikiwa tunapopita katika magumu
(bonde la uvuli wa mauti). Tutambue kwamba hakuna wakati Mungu anatuacha. Sisi
ndio kuna wakati tunamuacha Mungu. Mruhusu Mungu awe Mchungaji wako (uwe kondoo
na Yeye awe Mchungaji) ndipo utaona ukiwa salama kupitia ‘gongo lake na fimbo
yake.’
Acha tabia ya kukiri kwa kinywa chako kwamba hutaweza,
utafeli, hutafanikiwa nk. Shetani anapokusikia ukikiri kushindwa unampa nafasi
ya kufanyia kazi maneno yako ili yawe halisi. Mithali 6:2 “Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa
chako.”
Lakini pia acha kutumainia nguvu zako mwenyewe, cheo chako,
elimu yako, uzoefu wako au ujanja wako. Badala yake mtegemee Mungu akuwezeshe.
Zekaria 4:6 “Akajibu akaniambia,
akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si
kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.” Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye
nguvu.”
3.
Tambua thamani yako kwa Mungu na hazina alizokuandalia
Zekaria 2:8 “Kwa
maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa
wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.”
Ikiwa mtu anayekugusa wewe anagusa mboni ya jicho la Mungu, Unadhani uko salama
kiasi gani mikononi mwa Mungu? Hata kama mtu unamheshimu kiasi gani, unadhani
utamfanya nini unapomuona analeta kidole chake kiguse mboni ya jicho lako? Bila
shaka utamsukumia mbali bila kujali ana uhusiano gani na wewe! Zaburi
17:8 u7yhj“Unilinde kama mboni ya jicho,
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako.”
Mungu yuko tayari kukumulikia katika giza nene unalopitia. Isaya
9:2 “Watu wale waliokwenda katika giza
Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru
imewaangaza.” Lakini pia ziko baraka zako alizoficha kwa ajili yako. Isaya
45:3 “nami nitakupa hazina za gizani, na
mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana,
nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.” Ili uzijue baraka
alizokuandalia SIRINI jifunze kuomba maombi ya kuingia chumba cha ndani na
kujifungia – MUNGU AONAYE SIRINI ATAKUPA THAWABU AU MAJIBU YAKO. Mathayo 6:6 “Bali wewe usalipo, ingia katika chumba
chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye
sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”
USHUHUDA WANGU
Jambo la pekee linalonifanya niweke tumaini langu kwa Mungu
kuliko mwanadamu yeyote ni mambo haya matatu: 1. MUNGU HAFI 2. MUNGU HABADILI
NIA YAKE 3. MUNGU HAFILISIKI. Mojawapo katika haya matatu linaweza kumpata mtu yeyote
unayemtegemea na kujikuta pabaya. Kama hatakufa kabla ya kukufanyia
alilokuahidi, anaweza kubadilisha nia yake ya kukusaidia kwa sababu ya
vipaumbele vyake au changamoto fulani. Asipobadili nia yake, anaweza kutikisika
kiuchumi na kujikuta anashindwa kufanya aliyokuahidi.
MAOMBI
1. Ee Mungu naomba unifundishe kukaa chini ya mbawa zako
ili nisiogope hata uchumi wa dunia na wa familia unapotikisika.
2. Ee Mungu naomba uniondolee tabia ya kutaja changamoto
zangu na nguvu zangu kuliko UWEZO wako. Nitambue kwamba Wewe ndiwe chanzo cha
mafanikio na ushindi wangu wakati wote.
3. Ee Mungu naomba uwe JUU YA YOTE KATIKA YOTE NA NDANI YA
YOTE (Efe 4:6) maishani mwangu; Wewe uzidi na mimi nipungue kama alivyoomba
Yohana Mbatizaji (Yn 3:30).
NAKUOMBEA
WIKI HII UFUNIKWE NA MBAWA ZA BWANA KATIKA MAISHA YAKO!
Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania