Ticker

6/recent/ticker-posts

Ee Mungu nisaidie niione njia iendayo uzimani

EE MUNGU NISAIDIE NIIONE NJIA IENDAYO UZIMANI

Maono: Niliona tukipita kwenye kamlango kadogo sana ambako mtu hawezi kupita kwa njia ya kawaida isipokuwa kwa kuburuzika kwa tumbo. Hakuna aliyeweza kupita akiwa amebeba kitu au akisaidiana na mwenzake.

Naamini Roho wa Mungu anatukumbusha tu kwamba safari ya mbinguni inahitaji kujikana na sio rahisi kama wengine wanavyorahisisha.

Lk 13:23,24 “Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.” Lk 18:26,27 “Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Akasema, Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu.”

Ukifuatilia sana jibu la Yesu kuhusu wokovu utagundua mambo kadhaa. 1. Sio kazi rahisi kwa mwanadamu (jitahidini) 2. Wengi watataka lakini hawataweza kufikia viwango (masharti) 3. Kwa kuwezeshwa na Mungu inawezekana (neema).

Nimekuwa nikitafakari kwa nini ni vigumu kwa wengi kujiandaa na safari ya mbinguni. Jibu ni rahisi tu. Kuna watu wanataka kuingia mbinguni kwa matendo yao mema bila kujali kumpokea Yesu Kristo ambaye ni NJIA, KWELI na UZIMA. Lakini pia kuna watu wanajali tu uraia wao wa duniani na hawajali kabisa kwamba kuna maisha mengine baada ya hapa ambayo ni ya uhakika zaidi.

Nitatumia Mathayo 7:13-27 kutuandaa kwa ajili ya maombi ya wiki hii.

1. Unaweza kuwa muumini kwenye dini yako na usione ‘njia iendayo uzimani’

Mst wa 13,14 “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.

Dini ni juhudi za mwanadamu za kumtafuta Mungu wakati wokovu ni mpango wa Mungu wa kumtafuta na kumuokoa mwanadamu. Yesu Kristo hakuleta dini duniani bali wokovu wa roho zetu. Wala sio Wakristo waliojiita hivyo bali walipewa jina hilo na watu ambao hawakuwa Wakristo (Mdo 11:26). Kabla ya Antiokia waliitwa watu wa Njia ile (Mdo 19:23). Jina la Wakristo limekuwa likibadilika kadiri wahusika wanavyojichanganya. Kwa sasa unaweza kusema u mkristo na bado una michanganyo. Hivyo kuna majina mengine yamejitokeza kama vile, Mkristo aliyeokoka, mlokole, Mkristo jina, mlokole feki nk ili tu jina liendane na tabia halisi ya mtu.

Maandiko yanatuambia WENGI wanapitia mlango mpana (maisha ya kidini yenye uhuru usio na mipaka) na WACHACHE wanapitia mlango mwembamba (maisha ya kujikana nafsi na kutambua kwamba uraia wetu uko mbinguni na hapa tu wapitaji tu). Ukiona tu kwamba huwazi kwamba utawezaje kukaa na Bwana baada ya maisha haya ya duniani, bado hujaona njia iendayo uzimani. USIPENDE KUCHAGUA NENO UNALOTAKA KUSIKIA. SIFA ZA NENO LA MUNGU NI KUCHOMA NA KUKATA KOTEKOTE KULIKO SIME. Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.” Kuna siku utakumbuka mafundisho magumu uliyokwepa kuyasikiliza ukiwa tayari umehukumiwa. Hatukuja duniani kwa ajili yetu wenyewe. Tumeitwa kwa kusudi la Mungu (Rum 8:28).

2. Tambua watumishi wa kweli kwa tabia (character) na sio vipawa (charisma)

Mst 15-20 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.”

Huwezi kuwagundua watumishi wa uongo kwa kushiriki tu ibada peke yake. Mara nyingi wakiwa wanahudumu ibadani wanavaa ngozi ya kondoo (wanaigiza utakatifu). Wanakuwa mbwa mwitu kabla na baada ya kuhudumu ibadani. Maisha yao nje ya ibada yako tofauti sana. Hutashangaa ukiwaona kwenye baa na wanawake wenye mizigo ya dhambi, wakiwarubuni waumini, wakitapeli watu, wakizini na wanawake ndipo wasimame mimbarini, wakijitajirisha huku waumini wakifilisika nk. 2 Timotheo 3:6 “Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi.”

Kipindi hiki shetani amekusudia kuwavamia watumishi kwa roho ya zinaa na kupenda umaarufu (popularity). Tuwe macho na kulinda moyo kuliko yote tulindayo (Mit 4:23).

3. Karama alizo nazo mtumishi zisikupofushe macho, chunguza mwenendo wake

Mst 21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

Kuna watumishi wanaigiza karama za Roho na wengine wanapewa na shetani uwezo wa kutambua shida za watu kupitia pepo wa uaguzi. Pepo huyu alitaka kumdanganya mtume Paulo lakini akamgundua. Huyo pepo anaanza kukuambia ukweli ili umuamini kisha badae anapindisha ukweli. Kama una Roho wa Mungu hutaangalia tu UKWELI WA TAARIFA bali pia CHANZO CHA TAARIFA HIYO. Mdo 16:16-18 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.”

Unaweza kudhani umeponywa na Mungu na kumbe ni uponyaji wa kiina macho kutoka kwa shetani. Kinachotokea ni tatizo lako kuhamia tu upande mwingine. Unaingiziwa pepo lenye nguvu ya kudhibiti lile lililokupa ugonjwa (mapepo yanatofautiana mamlaka) halafu unajikuta tatizo limehamia kwenye ugumu wa maisha, zinaa au mahusiano kuvunjika. Shetani anachotaka ni wewe kuendelea kuwa mtumwa wake.

4. Kujua kwako mambo mengi bila kuyafanyia kazi hakutakusaidia wakati wa vita

Mst 24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

Shetani haogopi kujua kwako mambo mengi ikiwa hufanyii kazi unayoyajua. Ndiyo maana tuna watumishi wengi waliosomea mambo mengi ya Mungu lakini wanaanguka kila uchwao. Shetani pia anajua mengi sana kuhusu Mungu maana amekaa na kutumika mbinguni lakini hatendi mapenzi ya Mungu. Yak 2:19,20 “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?” Kama unajua mambo mengi kuhusu Mungu lakini hutendi mapenzi ya Mungu, HUNA TOFAUTI NA SHETANI. Tofauti yako na shetani itakuja pale utakapoacha kazi zake na kufanya mapenzi ya Mungu.

Majaribu yanakuangusha kwa vile nyumba yako haina msingi imara. Jifunze kuwa mtendaji wa Neno la Mungu ndipo utakuwa salama. Usitafute dini bali mtafute Mungu maadamu anapatikana (Isa 55:6).

MAOMBI

1. Ee Mungu naomba unisaidie niione njia ya uzima ili nisipoteze muda wangu kuabudu na kutoa sadaka wakati hunijui.

2. Ee Mungu naomba unipe macho ya kutambua watumishi wa kweli uliowaita ili nisiangukie kwa mbwamwitu.

3. Ee Mungu nisaidie nisipofushwe macho na miujiza kiasi cha kuuamini uongo na mwisho kuhukumiwa milele.

4. Ee Mungu naomba unisaidie niweze kutendea kazi mambo mengi niliyojifunza ili nisiendelee kuanguka kiroho na kimaisha.