
Maono: Nimeona nikimwambia mtu fulani kwamba baada ya Mungu
kumuondoa Uzia sasa kazi itaendelea vizuri
Upende usipende maisha yako yanaathiriwa na aina ya mamlaka iliyo juu yako. Kwa kawaida upako na baraka zinatoka juu kushuka chini (Zab 133). Hivyo unapokuwa chini ya mamlaka isiyo sahihi, inaathiri maisha yako.
Nitatumia Isa 6:1-8 kukupa mwongozo wa maombi ya wiki hii:
1. Hutaona utukufu wa Mungu wakati uko chini ya mtu anayejikweza
Mst 1-4 “Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi …”
Isaya hakuona utukufu wa Mungu mpaka alipokufa mfalme Uzia. Mfalme Uzia alikuwaje? Ukisoma 2 Nya 26:16-21 utagundua kwamba ufalme wake ulipokuwa na nguvu alijikweza mpaka akaingilia kazi za makuhani ambazo Mungu hajamtia mafuta kuzifanya. Makuhani wakamzuia lakini akalazimisha kwa hasira. Matokeo yake akapigwa ukoma katika paji la uso. Hivyo akatolewa nje ya hekalu na nje ya mamlaka yake hadi kufa kwake. Mwanawe akatawala badala yake.
Wakati mwingine tunaongozwa na watu wa aina hii hata makanisani. Mtu ambaye hana wito ndiye anakuwa kiongozi wetu. Kibaya zaidi tunaongozwa hata na mtu ambaye amepigwa ukoma kwa kutojali mipaka yake. Katika mazingira hayo hata tufunge na kuomba hatuwezi kuuona utukufu wa Mungu.
2. Ukimuona Mungu utajikosoa zaidi kuliko kukosoa wengine
Mst 5 “Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni
mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na
macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.”
Kabla Isaya hajauona utukufu wa Mungu alikuwa na jumbe za wengine zaidi kuliko ujumbe wake mwenyewe. Ili ujue hujaona utukufu wa Mungu, utagundua kwamba unasoma tu Biblia kwa ajili ya kuandaa mahubiri ya wengine na sio kwa ajili ya kuilisha roho yako. Ukisoma Isaya 5 (sura iliyotangulia) utagundua Isaya alikuwa na jumbe za wengine tu. Isaya 5 alitoa jumbe nyingi za OLE WAO lakini katika Isaya 6 alipouona utukufu wa Mungu akasema OLE WANGU. Sio vibaya kuwaonya na kuwahubiri wengine. Lakini unaweza kuwa kibao cha kuonyesha wengine njia wakati wewe mwenyewe unaenda upotevuni. Unafika mahali unajisahau kwamba hata wewe pia hujafika bali uko safarini. 1 Wakorintho 9:27 “bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”
3. Ukishatambua umechafuka wapi na ukakiri mbele za Mungu ndipo unatakaswa
Mst 6-7 “Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.”
Najiuliza ilikuwaje huyu mtumishi wa Mungu aendelee kupata maonyo ya wengine wakati midomo yake ni michafu? Hii inatufundisha kwamba UTUMISHI na UTAKATIFU ni vitu viwili tofauti kabisa. Kama unajali kumtumikia Mungu, ataendelea kukutumia na kama unajali kujitakasa, Mungu atakutakasa. Utaenda mbinguni kwa utakatifu na sio kwa utumishi. Na kama utaingia mbinguni, utapata taji au heshima kwa utumishi wako. Ila kama unajali tu kutumika bila utakatifu utapata hasara ya kukosa mbingu na kutaabika bure. Mungu alimsubiri Isaya atambue amecahfuka wapi na kuhitaji msaada wake.
4. Ukishatakaswa na Bwana unaitwa kiupya
Mst 8 “Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani
atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.”
Hapa tunaona Isaya akipokea wito kiupya. Hatumiki kwa mazoea tena. Nakumbuka miaka ya karibuni nilipoamua kumtafuta Mungu kwamba sichagui tu neno fulani la kuhubiri kwa sababu nalijua kwamba liko kwenye Biblia. Nauliza kwanza ni ujumbe gani ambao utatatua changamoto za wasikilizaji wangu. Sio kila andiko linafaa kwa mafundisho bali ni kila ANDIKO LENYE PUMZI YA MUNGU. 2 Timotheo 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.” Unaweza kutumia andiko vibaya na kuwaumiza watu badala ya kuwajenga. 2 Wakorintho 3:6 “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.”
Usisahau kwamba wapotoshaji wanatumia Biblia hiihii ambayo ina maneno yenye pumzi ya Mungu.
MAOMBI
1. Ee Mungu nisaidie kutambua mtu au
roho inayonizuia kuuona utukufu wako na kuchukua hatua stahiki.
2. Ee Mungu nipo roho iliyopondeka ili
nijikosoe badala ya kuwahukumu wengine
3. Ee Mungu nisaidie kutambua udhaifu
wangu kwa msaada wa Roho wako ili nitubu na kupokea msamaha wako
4. Ee Mungu niite upya kwa vile
nakutumikia kwa mazoea kiasi kwamba wakati mwingine najali wengine na kusahau
kuilisha roho yangu mwenyewe
Mungu akutane na wewe kipekee katika wiki hii na kukupa nguvu na muda wa maombi ili uweze kuugusa moyo wake kwa vile amesema tusijisumbue bali tumjulishe haja zetu.
Wafilipi 4:6,7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na
kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya
Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo
Yesu.”
Lawi Mshana