FUNGA
MILANGO YA SHETANI KATIKA MAISHA YAKO
Jana mchana nilipokuwa nikiomba mwongozo wa maombi ya wiki
hii nilipata maono haya: “Niliona mwanamke anataka akafue kaunda suti ya mume
wake. Akashangaa kwenye mkunjo wa shati kwa ndani pameandikwa, ‘Nitahakikisha
ananioa.’ Mume akashangaa maana amekuwa akiivaa mara nyingi. Hivyo akawa
anataka pengine aendelee tu kuvaa suruali na kuacha kuvaa shati lake.”
Maneno kama hayo hata kama hutaki kukubali yanaweza
kukuingiza kwenye agano baya la kishetani kiasi cha kuyumbisha ndoa yako.
Lazima mapando ya shetani yang’olewe! Mt 15:13 “Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni
litang'olewa”
Tangu kipindi cha Biblia mpinga Kristo amekuwa akitenda kazi kwa siri. 2 The 2:7 “Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.” Hata hivyo hataweza kutenda kazi kikamilifu hadi kanisa la Mungu litakaponyakuliwa. Kama mpinga Kristo alitenda kazi kwa siri kipindi cha mtume Paulo hata sasa anaendelea na kazi hiyo. Anahakikisha kwamba anapata milango ya kumuwezesha kunasa na kudanganya hata wateule wa Mungu. Mt 24:24 “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.” Waumini wengi wanaojali tu matokeo kupitia maombezi (miujiza) bila kujali kwamba chanzo cha huduma hiyo ni shetani wameshanaswa na kusajiliwa kuzimu. Lolote utakalowaambia hawataweza kukuelewa.
Ili mtu aweze kuepuka kuwa na chapa ya shetani katika mwili wake anatakiwa kuwa na hekima na ufahamu kutoka kwa Mungu. Ufu 13:18 “Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.” Ingawa shetani atatumia mifumo ya kibinadamu, tunahitaji hekima na ufahamu kutoka kwa Mungu. Mtu ambaye hajampa Yesu maisha yake (hajaokoka) hataweza kuepuka kupigwa chapa hiyo hata kama anajua maandiko matakatifu au amesoma Theolojia. Hii hekima wamepewa watu waliosajiliwa mbinguni tu. Ufu 13:8-9 “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia. Mtu akiwa na sikio na asikie.” Ijapokuwa watu waliookoka wanaoishi maisha ya kujikana wanadharaulika hapa duniani, kuna siku watu watajua kwamba mbele za Mungu ni watu muhimu sana. Isaya 35:8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.”
Mambo ya msingi kufahamu
1. Shetani hajali dini yako wala cheo chako. Anajali vitu vyake ulivyo navyo
Hata kama unamjua na kumuabudu Mungu kama una alama ya shetani katika maisha yako, unakuwa umempa uwezo wa kukuona (kuku-access) na kukushughulikia. Pengine u mwombaji mzuri sana lakini nguo zako unazovaa zina maneno ambayo yanamkaribisha shetani, hutaweza kupokea majibu yako. Unamtukuza shetani bila kujua. Alama za shetani ulizo nazo zinamfanya ajue kila kitu unachotaka kufanya kabla hujakifanya kwa sababu anakuona hata akiwa mbali. Chunguza vizuri nguo zako, mikanda unayovaa, saa unayovaa, vitabu unavyosoma, nyimbo unazosikiliza, video unazotazama. Vingine vina uhusiano wa moja kwa moja na matatizo uliyo nayo. Usijidanganye kwamba unaweza kutakasa vitu vilivyotengenezwa kuzimu.
Kuna mtu alipata shida nyumbani kwake mpaka alipogundua kwamba kalenda aliyo nayo, ina picha ya jinni. Unaweza kufuga majini bila kujua na kujikuta mambo hayaendi katika nyumba yako. Hata Waswahili wanasema, Kikulacho ki nguoni mwako. Unadhani ndoto za mahaba zitakoma na ndoa yako kupona, wakati unavaa nguo za ndani zenye alama za wachawi na wapinga-Kristo? Usipuuzie alama na maneno ya nguo unazovaa. Kama yana maana mbaya, yatamkaribisha shetani katika maisha yako na nyumba yako. Alama hizo hazitakuzuia kuzama katika maombi au kutumiwa na Mungu. Zitakuzuia kumuona Mungu. Hakuna mtu atakaingia katika ufalme wa Mungu wakati ana chapa za shetani.
2. Damu ya Yesu haitakasi kila aina ya uchafu. Usiitumie vibaya.
Kuna watu wana mazoea ya kutakasa kila kitu kwa damu ya Yesu. Kazi ya damu ya Yesu ni kusafisha uchafu au uvuvio wa shetani ambao umezunguka kitu ambacho ni cha halali. Kuna vitu havitakasiki bali vinatakiwa kutupwa au kuchomwa moto. Mtu anaweza kuosha embe lakini hakuna mtu anaweza kuosha takataka. Kama damu ya Yesu ingekuwa inatakasa kila kitu Mungu hangesema tokeni kati yao mkatengwe nao. Angesema jitakaseni tu hata kama mmejichanganya na wachafu. Kuna watu unatakiwa kuwaepuka katika maisha yako hata kama baadhi yao wanakuchekea sana. Wanakuibia ndoto na hatima yako. 2 Wakorintho 6:17 “Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.” Wengine kati ya maadui zako ni watu ambao wako karibu sana na wewe kiasi kwamba huwezi kuamini kama ndio chanzo cha kufeli kwako. Zab 55:12-14 “Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.”
Watu walipookoka walichoma vitabu vya
uganga bila kujali thamani yake na wala hawakuvitakasa. Mdo 19:18,19 “Na wengi wa wale walioamini wakaja
wakaungama, wakidhihirisha matendo yao.Na watu wengi katika wale waliotumia
mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote;
wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.”
Mtu akiokoka anatakiwa ‘kukimbia machafu ya dunia na sio kujichanganya na matendo maovu.’ 2 Petro 2:20 “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.”
Hata kama una vitu vya thamani kama ni vitu vya shetani, vichome au uvitupe ndipo utakuwa salama. Vinginevyo, shetani ataendelea kupeleka mashitaka kwa Mungu kwamba huna sifa za kupokea majibu yako na siku ya mwisho atadai roho yako.
Hivi karibuni nilitoa kisa fulani cha mama aliyekuwa na mgahawa wenye mvuto wa watu sana. Alipopata kichaa, akawa anatembea barabarani na kutoa siri ya mvuto huo. Akasema amefanikiwa kuvuta wengi kwa vile alikuwa anachanganya chakula na damu ya hedhi pamoja na maji ya kuoshea maiti. Hivi chakula kama hiki kinafaa kutakaswa na kisha kuliwa? Hapa tunahitaji macho ya kiroho na kuepuka kula chakula kama hiki ili tusipate madhara. Mungu hakukusudia kwamba kazi yetu iwe ni kushiriki ibada na kuimba na kupiga pambio peke yake bali kuwa na ufahamu wa roho na kupambanua mambo – kujua jema na baya na kumsikiliza Roho Mtakatifu. Tambua kwamba hata kama u mtu wa Mungu, kama unashiriki dhambi za mtu, utashiriki pia mapigo yake. Ufu 18:4 “Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.” Mungu atusaidie sana.
MAOMBI YA WIKI HII
1. Ee Mungu naomba unifunulie milango ya shetani ambayo iko
katika maisha yangu ili niifunge na kuhakikisha simpi ibilisi nafasi.
2. Ee Mungu nifungue macho yangu nisiwaambie siri zangu
wajumbe wa shetani hata kama wengine wanajiita watumishi wa Mungu.
3. Ee Mungu nipe macho yanayoona bidhaa za shetani ili
niepuke kuzinunua na kuzivaa au kuzitumia kwa ajili ya usalama wangu wa sasa na
baada ya kuondoka duniani.
4. Ee Mungu naomba unitapishe vitu vya shetani nilivyokula
ambavyo vimeharibu maisha yangu katika maeneo mengi
