TAMBUA KWAMBA KUWEKWA HURU SIO KUWA HOLELA
Tangu tupate uhuru mwaka 1961 katika nchi yetu tunakiri
kwamba tuko huru. Lakini ukifuatilia sana utagundua kwamba uhuru huo una
mipaka. Ingawa tuko huru katika nchi yetu huwezi kuchukua tu pori fulani na
kuanza kulima bila kibali, nyumba uliyojenga mwenyewe unailipia kodi, ukigundua
madini kwenye ardhi ya shamba lako sio ya kwako, ukitaka kujiua unachukuliwa
hatua wakati mwili ni wa kwako mwenyewe. Hii ni mifano tu ya kutufundisha
kwamba UHURU sio UHOLELA.
Lazima tujue kwamba hakuna mtu aliomba (ali-apply) kwamba
azaliwe kupitia familia fulani. Tumejikuta tu tumezaliwa na tuko duniani. Kwa
hiyo yupo aliyepanga kutuleta duniani bila kutuuliza wala kutushirikisha.
Sidhani kama hakuwa na mpango wowote wakati anatuleta duniani. Hata wewe
sidhani una vifaa nyumbani kwako visivyo na faida kwako. Unapoona kifaa hakina
faida kwako unakitupa au kukiuza kama bado kina faida kwa mwingine.
Jambo la kusikitisha ni kwamba ingawa tumejikuta tu tuko
duniani na tunaona kwa macho yetu masikini kwa matajiri wakifa, hatujiulizi
kwamba tumemfanyia nini huyo aliyetuleta duniani kwa miaka kadhaa aliyotupa.
Tunaendelea kufanya ya kwetu wenyewe bila kujihoji wala kujiuliza tutampa
ripoti gani tutakaposimama mbele zake. Ingawa Mungu anataka tufurahie maisha,
HILO SIO LENGO LAKE KUU. Kuna kitu anataka umfanyie. Na ili umfanyie kazi
fulani unatakiwa ule ili uweze kuishi. Lakini hakukuleta duniani ili tu ule na
kunywa halafu baadaye akuchukue. Mungu hawezi kufanya biashara ya hasara kiasi
hicho. Hata wewe hujawahi kufanya biashara ya aina hiyo. Kulisha mtu au mnyama
fulani bila malengo yoyote ya mbeleni.
Kwa minajili hii, hatuna uhuru wa kula wala kunywa kila
tunachotaka, hatuna uhuru wa kuvaa kila tunachotaka, hatuna uhuru wa kusikiliza
kila tunachotaka, hatuna uhuru wa kusema kila tunachotaka, hatuna uhuru wa
kufanya kila tunachotaka nk. Na kama hutaki kukubali ukweli huu, ukimaliza
mwendo wako wa maisha ya hapa duniani ndipo utaelewa ingawa utakuwa umeshachelewa.
LAZIMA TUISHI KWA AJILI YAKE (TUMUISHIE MUNGU) KWA
KUZINGATIA MIPAKA YA UHURU ALIOTUPA, KAMA TUNATAKA KUEPUKA JEHANAMU YA MOTO
Yak 2:9-26
1.
Mungu hataki upendelee/ubague watu
Mst 9: “Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na
kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.”
Mungu hapendi tabia ya kubagua matajiri kwa masikini,
wasomi kwa wasiosoma, wafupi kwa warefu, weupe kwa weusi, dini hii na dini ile
nk
2.
Usijifariji kwamba uko salama kwa kutii sheria zote na kuasi moja
Mst 10,11: “Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote,
ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. Kwa maana yeye aliyesema,
Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa
mvunja sheria.”
Usipuuzie baadhi ya makosa yako. Hata katika sheria za nchi
yetu ndivyo ilivyo. Hebu jiulize kama utatii sheria zote na kutoa misaada mingi
kwa jamii halafu ukavunja sheria moja inayozuia kuozesha watoto ili waendelee
na masomo yao. Kitakachokukuta hutajitetea kwamba sheria zingine zote
ulizishika vizuri. Hakuna mtu atakumbuka utekelezaji wako mzuri wa sheria
zingine. Kwa hiyo hakikisha unamtii Mungu katika maeneo yote ya maisha yako.
Usiwe na maisha ya kanisani na ya nyumbani au ofisini (double life).
3. Sheria
ya uhuru ni ngumu kwa vile umepewa uhuru wa kuamua. Haina miongozo na adhabu za
papo kwa papo’
Mst 12,13 “Semeni ninyi, na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ya uhuru. Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu.”
Kipindi chetu hatushuhudii watu wakipigwa papo kwa papo hivyo ni rahisi zaidi kuzembea. Mungu ni wa upendo lakini pia ni Mungu wa haki. Tusipothamini upendo anaotuonyesha sasa kama Mwokozi, kuna siku tutakutana naye kama Mhukumu wa Haki. Wakati huo hakutakuwa na rehema tena. Unatakiwa kupatana na mshitaki wako njiani mkielekea polisi au mahakamani na sio ukitoka mahakamani ukielekea gerezani. Mt 5:25,26 “Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.”
4. Imani
ya maneno tu bila kuthibitishwa kwa vitendo itakupoteza
Mst 14-17 “Ndugu zangu, yafaa nini, mtu
akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza
kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na
riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na
kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa
ina matendo, imekufa nafsini mwake.”
Mifano: Ibrahimu mst 21-22,24 na Rahabu Mst 25,26
Ni kweli kwamba matendo yetu mema hayawezi kutupatia wokovu. Tunapata wokovu kupitia kazi ya Yesu msalabani. Hata hivyo matendo yetu ni muhimu sana tukishamuamini Yesu ili kuthibitisha toba yetu kama ni ya kweli. Mdo 26:20 “bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.”
5.
Kama matendo yako hayaendani na imani yako huna tofauti na shetani
Mst 18,19 “Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.”
Kama imani yako ni ya maneno tu, shetani anakuzidi maana anatetemeka kabisa akisikia Jina la Yesu. Anajua mengi na anaongea mengi kuhusu Mungu. Shida yake kubwa ni kwamba hatekelezi anayosema. Anafanya kinyume na Mungu na lengo lake ni kuumiza moyo wa Mungu kwa kuhakikisha anaenda na wengi Jehanamu.
MAOMBI
1. Ee Mungu naomba uniondolee tabia ya kudharau, kubagua na
kuhukumu watu ambao uliwaumba kwa mfano wako hata kama hawana imani kama ya
kwangu.
2. Ee Mungu naomba uniondolee tabia ya kujifariji kwamba
ninakupenda wakati nikiwa peke yangu nakukosea kwa mawazo yangu na matendo
yangu. Siwezi kukuficha tabia yangu Wewe Mungu wangu wala mshitaki wangu
shetani.
3. Ee Mungu naomba unisaidie nisiutumie uhuru ulionipa
vibaya kwa kuwa na maisha holela yasiyo na mipaka katika Neno Lako
4. Ee Mungu naomba unisaidie matendo yangu yaendane na
imani yangu ili nisiwe kikwazo kwa watu wanaotaka kukuamini
5. Ee Mungu naomba uondoe tabia za shetani katika maisha
yangu. Nisiwe msemaji na msimuliaji tu wa imani yangu wakati katika vitendo na
uhalisia wa maisha ninakukwaza.
Karibu
sana wewe unayehitaji kumpa Bwana Yesu maisha yako. Omba sala hii kwa imani
moyoni mwako:
“Ee Mungu Baba wa mbinguni, nimekukosea kwa mengi na
ninastahili hukumu yako. Lakini natambua kwamba ulimtuma Mwanao wa pekee, Yesu
Kristo afe msalabani kwa ajili yangu. Najua Yesu hakuleta dini bali alileta
wokovu wa roho yangu. Naomba unirehemu na kunisamehe dhambi zangu na kunipa
maisha mapya. Nipe Roho Mtakatifu aniongoze ili niweze kushinda majaribu na
kukuishia kwa uaminifu ili hatimaye baada ya maisha haya nikakae na Wewe
milele. Nakushukuru kwa kuniokoa katika Jina la Yesu Kristo aliye hai. Amina.”
Lawi Mshana