Ticker

6/recent/ticker-posts

Unajua kwa nini hakuna dhehebu zuri kuliko jingine?

UNAJUA KWA NINI HAKUNA DHEHEBU ZURI KULIKO JINGINE?

Tumekuwa katika kipindi ambacho tunashika zaidi ‘kivuli’ badala ya kumshika ‘KRISTO’ aliye tumaini letu. Kuna tofauti kubwa sana kati ya KANISA na DHEHEBU. Kimsingi, tunaposema tumesajili Kanisa tuna maana ya kusajili Dhehebu. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kusajili Kanisa. Maana ya Kanisa ni Ekklesia yaani, WALIOITWA (called out assembly or congregation) – waliokuwa wamepotea Mungu akawaita. Hivyo katika dhehebu kuna ‘walioitwa’ na ‘waliopotea’. Baada ya Adamu na Hawa kumkosea Mungu, Mungu alitengeneza mpango wa kumrejeza mwanadamu kwake ambao unaitwa KANISA. Kanisa hilo akalipa nguvu dhidi ya shetani kwa kusema milango ya kuzimu haitalishinda Kanisa (sio dhehebu). Mathayo 16:18 “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” YESU HAKULETA ‘DINI’ AMEITA WATU WAWE ‘KANISA.’

Pengine hujui kwamba dini ndiyo ilimuua Yesu. Mfalme (kiongozi wa serikali) alitamani kumuachia Yesu asisulubiwe lakini viongozi wa dini wakasema lazima asulubiwe. Yohana 19:4,6 “Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake. Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulibishe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.”

Bwana Yesu alipata upinzani sana kutoka kwa madhehebu ya wakati huo. Mathayo 16:1,6 “Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni. Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” 

Tuangalie haya madhehebu mawili ya kipindi cha Biblia yalivyopoteza mwelekeo wao (yalikuwepo mengine zaidi ya haya):

Ingawa Mafarisayo waliamini vitabu vya sheria, vya hekima na manabii pamoja na maisha yajayo, Masadukayo hawakuamini ufufuo wa wafu. Jambo kubwa lililowakwaza kuhusu Bwana Yesu ni huduma yake ya kuwapa watu wote njia ya kupata wokovu wa milele na uhusiano na Mungu.

Masadukayo:

Walijiona kuwa ni waumini wa zamani wenye msimamo mkali (conservative). Walikubali tu sheria ya Musa iliyoandikwa. Hawakukubali ufunuo. Hivyo walipinga mafundisho mengi ya Bwana Yesu kama vile ufufuo wa wafu, uwepo wa malaika na adhabu baada ya kifo. Walikuwa pia wako kisiasa zaidi na walitaka huduma za kidini zifanyike hekaluni tu. Baada ya kuharibiwa kwa hekalu mwaka 70 baada ya Kristo dhehebu hili halikuendelea. 

Mafarisayo:
Waliwakilisha kundi la watu wa kawaida. Zaidi ya kuamini torati ya Musa waliamini pia vitabu vingine ambavyo leo tunaviita Agano la Kale pamoja na ‘mapokeo ya wazee,’ kama vile kunawa mikono mpaka kiwiko nk. Mt 15:1-15; Mk 7:1-23.

1. Waliongeza sheria nyingi ambazo zilikuwa mzigo kwa watu na hata kwao wenyewe.

Waliongeza sheria 613 ambapo 365 ni za kukataza (hasi) na 248 za kutakiwa kufanya mambo fulani (chanya). Luka 11:46 “Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.”

2. Walikuwa wanapenda kujihesabia haki kuliko wengine.

Walijiona wako viwango vya juu kiroho kuliko watu wengine. Luka 18:11 “Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.”

3. Walipenda kuangalia dhambi za nje na kupuuza za ndani.

Walijali zaidi usafi wa nje wakati uhalisia wa maisha yao ulikuwa umejaa dhambi.

Mt 23:25-28 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.”

4. Walichukizwa na tabia ya Yesu ya kuwa karibu na wenye dhambi ili kuwavuta kwa Mungu.

Walipenda kuwahukumu wenye dhambi badala ya kuwasaidia. Mt 9:10-13 “Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

HEBU TUJIULIZE:

1. Je katika kipindi chetu hakuna viongozi wa dini na waumini wenye tabia hizi hata kama madhehebu yao yana majina tofauti? Hakuna walioweka sheria ambazo haziko katika Biblia na wamezipa nguvu kuliko Biblia yenyewe? Hakuna wanaosema mimi si kama yule wa dhehebu lile wakati wametawaliwa na dhambi? Hakuna wanaojali mahudhurio na utoaji wa waumini na kupuuza kabisa mabadiliko ya ndani katika mioyo yao? Hakuna waumini wanaowachukia WENYE DHAMBI badala ya kuichukia DHAMBI?

2. Je hatuna wanafiki wanaoona tu dhambi za wengine lakini za kwao wenyewe hawazioni?

Mathayo 7:3-5 “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”

MAMBO NILIYOIFUNZA KWA KUABUDU NA KUHUDUMU KATIKA MAKANISA YASIYO YA KIPENTEKOSTE, FELLOWSHIP NA KATIKA MAKANISA YA KIPENTEKOSTE TANGU NIMPOKEE BWANA YESU MWAKA 1989:

1. Zamani wokovu na kujazwa Roho Mtakatifu vilichukuliwa kama dini mpya, kero au uzushi hivyo viongozi wa dini hawakuwahitaji watu hao ibadani. Jambo hili lilipelekea madhehebu mapya kuanzishwa ili watu hao wapate uhuru wa kuabudu katika roho. Miaka kadhaa baadaye yalitengenezwa mazingira ya kuwapa uhuru wanaotaka kujiachia katika Roho Mtakatifu.

2. Baada ya madhehebu mapya kuanza yapo ambayo msisitizo wake haukuwa mabadiliko ya kiroho bali yalikuwa ni kupambana na madhehebu walikotoka. Hawakuona au hawaoni lolote zuri linalofanywa na madhehebu walikotoka. Hawakumbuki kwamba hata kuiamini Biblia kuwa ni Neno la Mungu na kuvijua vitabu vya Biblia walijifunza huko.

3. Baadhi ya madhehebu mapya yaliamua kuweka mkazo katika mabadiliko ya kiroho tu na kusahau kwamba bado tuko duniani na tunahitaji kula na kuishi. Kilichotokea au kinachoendelea kutokea ni watu kuwa tegemezi wa misaada na wengine kuikana imani kwa sababu ya changamoto za maisha. Haukuwepo mkakati wowote wa kijamii au kiuchumi zaidi ya kujenga nyumba za ibada na majukwaa ya mikutano ya Injili.

4. Baadhi ya madhehebu yalijikita katika mahitaji ya maisha ya hapa duniani na kusahau lengo kuu la kuwasaidia watu kumjua na kumuona Mungu na hatimaye kwenda mbinguni. Kinachotokea ni kujali utoaji wa mtu hata kama haonekani kanisani. Uhai wa muumini unapimwa kwa utoaji wa mali zake na sio kujihusisha kwake katika ushirika, ibada, maombi na kumtumikia Mungu.

5. Jambo jingine ni kwamba hakuna dhehebu ambalo moja ya mambo haya hayapo au hayatokei:

(a). Kuwa na waumini ambao hawana ishara zozote za waaminio kama maandiko yalivyosema. Kumbuka hizi sio ishara za wainjilisti wala wachungaji bali ni za waaminio. Angalau mtu anatakiwa kuwa na mojawapo ya ishara hizi. Labda tu kama ametosheka kuwa mshirika/msharika. Marko 16:17,18 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

(b). Kuwa na waumini wenye matendo ya mwili. Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Kama hakuna walevi, kuna waasherati. Kama hakuna wachawi kuna wenye wivu, wazushi na wenye fitina. Tuwe tu wakweli tusione vibanzi vya wengine wakati tuna boriti. Sijui mwenye boriti anaonaje kibanzi?

(c). Kuwa na watu ambao hawajaokoka pamoja ingawa wamekuwepo kanisani kwa muda mrefu. Tena baadhi yao ni watumishi. Siku moja kabla ya kuanza kubatiza nilihubiri Neno na kuuliza mmoja mmoja kama ameokoka. Binti mmoja ambaye nadhani tangu azaliwe tunaabudu naye, akasema mimi sijaokoka ila mama ameniambia leo nibatizwe. Unadhani kama singehoji vizuri ningekuwa nimembatiza kweli? Madhehebu yanatofautiana tu idadi ya waliookoka na wasiookoka. Lakini makundi yote yapo kwenye kila kusanyiko au dhehebu.

(d). Kuna watu wameongozwa sala ya toba lakini hawajaokoka bado. Unaweza usinielewe lakini kuna watu tumewang’ang’aniza mpaka wameamua kutukubalia ili wasitukwaze. Kumekuwa na mtindo siku hizi wa kuitwa wagonjwa na wenye mahitaji mbele mkutanoni ili waombewe halafu hapohapo tunawaongoza sala ya toba na kuwaambia wamfuate mtu fulani akawaandike majina. Huu ni ujanja ambao hautoki kwa Mungu. Ukimfuatilia huyo mtu aliyeongozwa sala ya toba anasema mimi sikupita kuokoka bali nilimleta ndugu yangu mgonjwa aombewe. Mimi mwenyewe niliwahi kung’ang’anizwa nikiwa mwanafunzi ili niokoke nikamkubalia huyo ndugu. Akashangaa kuniona mwaka uliofuata niliposikia mahubiri nikipita mbele kuokoka upya. ILE YA KWANZA NILIMUOKOKEA, HII YA PILI NIKAOKOLEWA NA BWANA YESU. Mtu akigundua kwamba kiingilio cha kanisani kwenu ni sala ya toba, atawaokokea ili apate mke au anachotafuta. Sijui kama unajua kwamba Bwana Yesu hakumuongoza Zakayo sala ya toba bali alitangaza tu kwamba wokovu umeingia humo kutokana na mabadiliko aliyoyaona (Lk 19:8-10). Sipingi sala ya toba ila nataka ujue kwamba sala ya toba ni mwongozo tu baada ya mtu mwenyewe kuamua kutubu na kumgeukia Mungu. Akiamua anaweza kutubu mwenyewe kwa kuongozwa na Zaburi 51.

Nimalizie tu kwa kusema kwamba tusiache kuhubiri kweli na kutekeleza maono tuliyopewa. Lakini tumuache Mungu mwenyewe ahukumu. Mungu ndiye anajua vigezo anavyotumia katika kuhukumu. Anaweza pia kumtangazia mtu msamaha ambaye kwa vigezo vyetu hastahili kabisa kama Rais anavyoamua kutangaza msamaha kwa wafungwa siku ya sherehe fulani. Hivi yule mwizi wa msalabani ilikuwaje? Bilashaka wengi walimsikitikia sana kwamba amekufa katika dhambi kwa sababu ni mwenye dhambi, hajaokoka, hajabatizwa wala hajabarikiwa. Lakini alitubu akiwa katika maumivu na Bwana Yesu akamuahidi kuwa naye siku hiyohiyo paradiso. Hata hivyo usitumie kigezo hiki kukataa kutimiza yote unayotakiwa kufanya kwa vile wewe hujapigiliwa misumari msalabani. Unaweza kupoteza roho yako milele usipokuwa mwangalifu.

Hata hivyo Yesu mwenyewe aliwahi kusema kwamba maono yakiwa mapya yanahitaji chombo kipya. Kwa hiyo tunatakiwa kuwa viriba vipya kwa ajili ya divai mpya. Mathayo 9:16, 17 ‘Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote’. Tusilazimishe maono mapya yakubalike kwa watu ambao ni viriba vya kale. Chombo cha Bwana ni watu aliowaita na sio vyama wanavyovitumikia. Mdo 9:15 “Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.”

Mungu atusaidie sana na kuturehemu. 

Maombi ya wiki hii:

1. Ee Mungu naomba uniondolee roho ya kujiamini kupita kiasi na kujihesabia haki ili nisije nikahukumiwa kama Farisayo.

2. Ee Mungu naomba uliponye kanisa lako ili tusishikilie tofauti zetu na kusahau kazi ya msalaba ambayo ilimgharimu uhai Mwanao mpendwa Yesu Kristo kwa ajili ya kutupatanisha na Wewe.

Lawi Mshana