Jinsi ya kutofautisha watumishi wa kweli na wa uongo
NB: Ni ujumbe mrefu lakini utakusaidia. Umekuwa ujumbe mrefu kwa vile nimekuwekea baadhi ya Maandiko wewe uliye mbali na Biblia
Tumekuwa tukilalamika sana kuhusu kuwepo kwa manabii na walimu wa uongo. Ni vizuri kutambua tabia zao ili kujua jinsi ya kuwaepuka. Neno la Mungu limeonya kwamba njia pekee ya kuepuka udanganyifu wao ni Kanisa kuwa na HUDUMA TANO ZILIZOTOLEWA NA BWANA YESU (NA SIO ZILIZOTOLEWA NA VYUO WALA KWA MSUKUMO BINAFSI). Huduma hizo ni kwa ajili ya kusaidia watu KUKUA KATIKA KRISTO. Kazi ya vyuo vya Biblia ni ‘kunoa huduma’ na sio ‘kutoa huduma’. Kukataza waumini kushiriki mikutano ya hawa watumishi hakutoshi kwa vile sasa kuna mitandao ya jamii. Tunatakiwa kuwasaidia wajue jinsi ya kupambanua jema na baya. Efe 4:14 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.”
1. Watumishi wa uongo wanataka wengine wawatumikie; watumishi wa kweli wana shauku ya kuwatumikia wengine.
Mt 20:25-28 “Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Yn 13:14 “Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.”
Kinyume chake, watumishi wa uongo wanatumia vibaya mamlaka kwa kuwanyonya wengine kwa manufaa yao wenyewe. Yuda 12a,16 “Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu. Watu hawa ni wenye kunung'unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.” Wanajijali wenyewe. Eze 34:2-4 “Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala.”
Watumishi wa kweli ni wanyenyekevu na wanajali wengine kuliko wao wenyewe hasa hasa wanajali masikini, wanaoishi mazingira hatarishi na wanaoonewa. Mchungaji mwema anatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo (Yn 10:11).
2. Shabaha ya watumishi wa uongo ni pesa; wakati shabaha ya watumishi wa kweli ni huduma
1 Tim 6:5-10 “na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”
Yer 6:13 “Kwa maana, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa miongoni mwao, kila mmoja ni mtamanifu; na, tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu.” Mik 3:11 “Wakuu wake huhukumu ili wapate rushwa, na makuhani wake hufundisha ili wapate ijara, na manabii wake hubashiri ili wapate fedha; ila hata hivyo watamtegemea Bwana, na kusema, Je! Hayupo Bwana katikati yetu? Hapana neno baya lo lote litakalotufikia.” Lk 12:15 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” 2 Pet 2:3 ‘Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.”
Tabia za watumishi wa kweli. Mdo 20:33-35 “Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.” 1 Tim 3:3 “si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha.” 1 Tim 6:8 “ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.”
3. Watumishi wa uongo wanapamba na kupuuza dhambi; watumishi wa kweli wanahubiri toba
Msingi mkuu wa ujumbe wa mtumishi aliyetumwa na Mungu ni kuita watu watubu na kumrudia Mungu. Mik 3:8 “Bali mimi, hakika nimejaa nguvu kwa roho ya Bwana; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubiri Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake.” Mungu aliwatuma manabii wa Agano la Kale kwa ajili ya kuhubiri toba. Yer 35:15 “Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza.”
Toba ilikuwa pia ni shabaha kuu katika mahubiri na mafundisho ya Agano Jipya. Yohana Mbatizaji alihubiri toba (Mt 3:1,2), Yesu alihubiri toba (Mt 4:17), Petro na Paulo walihubiri toba (Mdo 2:;38; 3:19; 26:20), na katika nyaraka za makanisa saba, Yesu aliendelea kusisitiza ulazima wa toba (Ufu 2:5,16,21,22; 3:3,19).
Watumishi wa uongo wanapuuza ujumbe kuhusu toba. Yer 23:14,17 “Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.Daima huwaambia wao wanaonidharau, Bwana amesema, Mtakuwa na amani; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.” Watumishi wa uongo hawachukulii dhambi kwa uzito wake na hawaikemei. Wanaahidi kibali na mafanikio bila toba na utii kwa Mungu.
4. Watumishi wa uongo wanatumia vibaya Neno la Mungu; watumishi wa kweli wanahubiri kusudi lote la Mungu
Watumishi wa kweli hawahubiri tu kuhusu toba, wanahubiri pia mausia yote ya Mungu. Mdo 20:27 “Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.” Hawapuuzii andiko lolote kwa vile wanatambua kwamba Maandiko yote yana pumzi ya Mungu. 2 Tim 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”
Wanajitahidi kuhubiri kweli ya Mungu. 2 Tim 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.”
Watumishi wa uongo wao ni tofauti. Wanapindisha ukweli. 2 Pet 2:2 “Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa.” Wanachagua kifungu kinachosaidia malengo yao na kupindisha maana yake kwa faida yao (Yer 23:36; Gal 1:7; 2 Pet 3:16).
5. Watumishi wa uongo wana theolojia ya Kristo iliyopinda; shabaha ya watumishi wa kweli ni kwa Kristo
Msingi wa ujumbe wa watumishi wa uongo ni theolojia iliyopinda kuhusu Yesu Kristo. Mitume walionya kuhusu hili. 2 Pet 2:1 “Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.” Yud 4 “Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.” Kol 2:8,9 “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.” Roho ya mpinga Kristo inatenda kazi duniani (1 Yoh 4:3).
Msingi mkuu wa watumishi wa kweli ni Kristo. 2 Kor 4:5 “Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.” Soma pia 1 Kor 1:23 “bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi”; Kol 1:28 “ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo”.
6. Watumishi wa uongo wana tabia za makafiri; watumishi wa kweli wana tabia ya utauwa wakati wote (tabia njema wakiwa mahali popote)
Yer 23:13,14 “Nami nimeona upumbavu katika manabii wa Samaria; walitabiri kwa Baali, wakawakosesha watu wangu Israeli. Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.”
Sef 3:4 “Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu.” Yud 8 “Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu.” 2 pet 2:118 “wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.” Hawatendei kazi mahubiri yao. Mt 23:3 “basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.”
Watumishi wa kweli wako tofauti kabisa. Mfano mtume Paulo. 1 The 2:3-6,10 “Kwa maana maonyo yetu siyo ya ukosefu, wala ya uchafu, wala ya hila; bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu. Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wo wote, kama mjuavyo, wala maneno ya juujuu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi. Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine tulipokuwa tukiweza kuwalemea kama mitume wa Kristo. Ninyi ni mashahidi, na Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa.” Mtume Paulo pia alimuonya Timotheo awe mfano wa kuigwa. 1 Tim 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”
7. Watumishi wa uongo wanazaa matunda mabaya; watumishi wa kweli wanazaa matunda mema
Bwana Yesu alitoa mwongozo kuhusu hili. Kwa nje wanaweza kuonekana wanyenyekevu na wacha Mungu lakini maisha yao halisi ni tofauti kabisa. Mt 7:15,16 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?” Ni watu wanaoleta matengano badala ya kuunganisha watu. Yud 19 “Watu hao ndio waletao matengano, watu wa dunia hii tu, wasio na Roho.” Wanawavuta wanafunzi wawaandamie wao badala ya kuwaelekeza kwa Bwana. Mdo 20:29,30 “Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.” Rum 16: 17,18 “Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao. Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.”
Kinyume chake, watumishi wa kweli aliowatoa Kristo kwa ajili ya Kanisa wanawaimarisha katika imani (Efe 4:13). Wanatumia mamlaka kwa kipimo walichopewa na Bwana. 2 Kor 13:10 “Kwa sababu hiyo, naandika haya nisipokuwapo, ili, nikiwapo, nisiutumie ukali kwa kadiri ya uwezo ule niliopewa na Bwana, kwa kujenga wala si kwa kubomoa.” Huduma yao inakuwa na matunda mema. Kol 1:6-7 “iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mjoli wetu mpenzi, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu.”
Nukuu zimetoka kwenye Herald of His Coming katika makala ya Rich Carmicheal (Beware of false prohets and false teachers Nov/Dec 2022)
HABARI YA KUSIKITISHA KUTOKA NCHINI KWETU
1. Binti alizoea kwamba wakienda kufanya usafi nyumbani kwa mchungaji wao kwa zamu wanatoa huduma zote ikiwa ni pamoja na kuzini naye. Alipohamia katika mji wetu na kuabudu kanisa tofauti na lile alilokuwa anaabu awali akashangaa hilo halitokei. Ikabidi aulize wenzake mbona hawatoi huduma hiyo. Ilibidi aongozwe katika toba kwa vile alidhani ni maisha ya kawaida kwa waumini kutoa huduma hiyo kwa mchungaji wao.
2. Mwanamke alienda kanisa fulani kuombewa na mhubiri ofisini. Alipowekewa mkono akalala usingizi na kisha akaingiliwa kingono. Alipoamka alihisi hali fulani asiyoielewa. Alipouliza akaambiwa ni operesheni tu inaendelea kufanya kazi katika mwili wake hivyo asiwe na wasiwasi.
Tunahitaji kuwa macho sana katika nyakati hizi za mwisho.
Dr. Lawi Mshana, +255712924234; Tanzania