
HUTAPOKEA MAJIBU YAKO KWA KUFUNGA (SAUMU) PEKE YAKE
Ni ukweli usiopingika kwamba kufunga na kuomba ni mojawapo ya nguzo kuu za muumini wa kweli. Hata mtumishi wa Mungu aliyewahi kuwa muabudu shetani (satanist) alisema kwamba moja ya vitu ambavyo walipovikuta kwa Mkristo walikwama kumdhuru ni uaminifu katika maombi ya kufunga. Neno la Mungu linatuagiza kufunga na kuomba.
Hata hivyo napenda kukupa angalizo. Bwana Yesu hakumkomboa mwanadamu kwa kufunga peke yake bali ALITOA UHAI WAKE KUFA KWA NIABA YETU ILI KUTUPATANISHA NA MUNGU (substitutionary atonement). Ingawa alijitoa kufa kwa ajili yetu bado aliagiza kwamba na sisi tuishi maisha ya KUJITOA KISADAKA kwa ajili Yake.
1. Kila mtu achukue msalaba wake na kumfuata ndipo ataweza kuwa mwanafunzi wa Yesu. Kinyume na hapo, atakuwa ni mshirika/msharika tu ambaye anategemea kuzikwa vizuri siku akifa hata kama roho yake inakwenda kuzimu.
Luka 14:27 “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”
2. Toa mwili wako uwe dhabihu iliyo hai (kafara) takatifu ndipo utakuwa umefanya ibada yenye maana.
Ibada ya kweli ni kujitoa kisadaka kwa Mungu mpaka usikie maumivu. Mnyama anapotolewa kafara anasikia maumivu ya moto. Leo hatutoi kafara za wanyama tena kwa vile Yesu amefanyika kafara kwa ajili yetu MARA MOJA TU. Lakini anataka tuwe na maisha ya KUJIKANA NA KUTESEKA KWA AJILI YAKE.
Rum 12: 1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.”
KWA NINI WATU WENGINE WANAFUNGA NA KUOMBA LAKINI MAISHA YANAKUWA MAGUMU ZAIDI?
1. Hawajali kutoa msaada kwa masikini
Gal 2:10 “ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya.”
2 Kor 9:8,9 “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele.”
Baraka za watu wa Mungu hazitegemei kuomba na kufunga peke yake wala kufanya kazi peke yake. Lazima tutii maagizo tuliyopewa na Mungu. Hata Mtume Paulo alipoenda Yerusalemu (makao makuu) kutambulisha huduma yake, aliambiwa asiwasahau masikini. Pamoja na upako wa kuhubiri, kufundisha, kuombea, kuimba, kuponya magonjwa; LAZIMA UWE NA BIDII YA KUWASAIDIA MASIKINI.
2. Wanapenda kutembelea wahitaji wakiwa mikono mitupu
Ni jambo la kawaida kwa waombaji wengi kutembelea watu na kuwaombea bila kuwapa chochote hata kama uwezo wanao. Agizo la Mungu ni kwamba usiende mbele zake mikono mitupu (toa sadaka kanisani), usitembelee mkweo mikono mitupu na usiwasahau wahitaji na maskini.
Kutoka 34:20 “….. Wala hapana atakayehudhuria mbele zangu mikono mitupu.”
Ruthu 3:17 “Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana akaniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu.”
Kum 15:11 “Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako.”
KWANINI KIPINDI CHA MAANDALIZI YA SIKUKUU NIMESHIRIKISHA FURSA YA KUGUSA WASICHANA MASKINI WASIOWEZA KUPATA TAULO ZA KIKE?
Nimefanya hivyo ili tushiriki mateso ya Kristo kwa kujitoa kwa ajili ya wahitaji kuliko kusherehekea kwa mazoea. Wengi katika sikukuu tunavaa vikali, tunaandaa chakula cha gharama nk lakini tunatoa sadaka ndogo sana. Lakini pia sadaka hii tunayotoa inagusa makanisa yetu tu na huenda matumizi yake yakaishia kwenye mahitaji ya makanisa yetu. Tunapomsaidia msichana maskini anayedhalilika ambaye sio ndugu yetu na wala sio muumini mwenzetu katika kipindi hiki kigumu, tunapata thawabu kubwa kwa Mungu.
Kum 16:16 “Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu.”
Hata Bwana Yesu alikuwa na mfuko wa sikukuu na kusaidia maskini. Hii inaonyesha jinsi alivyojali mahitaji ya kimwili ya watu na sio ya kiroho tu.
Yohana 13:29 “Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu.”
Hata Hana alipoona amedhalilika kwa muda mrefu, aliamua kuweka nadhiri ya utoaji ndipo akajibiwa. 1 Sam 1:11 “Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.”
NB: Lakini pia tusisahau kwamba mtu ambaye hasaidii masikini na wahitaji ataenda motoni hata kama anatoa vizuri huduma za kiroho. Kwa mujibu wa Biblia mtu wa aina hii ni mbuzi ambaye yuko mkono wa kushoto na sio kondoo aliyeko mkono wa kuume.
Mt 25:41-46 “41 Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; 42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; 43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. 44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? 45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. 46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.”
Mungu atusaidie tujue wajibu wetu kwa Bwana na kwa jamii inayotuzunguka hasa katika kipindi hiki tunapokumbuka kufa na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Lawi Mshana