Ticker

6/recent/ticker-posts

Tuwe watu wa rohoni na tuongozwe na Roho Mtakatifu

TUWE WATU WA ROHONI NA TUONGOZWE NA ROHO MTAKATIFU

Maono: Nimeona mtu akitaka kutumia camera yake ila akatakiwa kutambua sensor ya camera iko wapi na sio kupiga tu. (Mungu hataki tupige hewa wala kubahatisha katika maombi na huduma zetu).

Ulimwengu wa roho ni halisi kuliko huu wa mwili tunaouona kwa macho. Hivyo tusisinzie, tusiwe wajinga na tujazwe Roho. Waefeso 5:14-18 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza. Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;”.

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”

Lk 1:80 “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.

Yohana Mbatizaji aliongezeka nguvu rohoni akaweza kuishi jangwani bila shida na akatimiza huduma yake – watu wakamfuata jangwani kumsikiliza (Mt 3:4-6 “Naye Yohana mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao.”)

1 Kor 2:10-16 “10 Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.11 Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.12 Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.13 Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.14 Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.15 Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.16 Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.

Faida za kuwa mtu wa rohoni

1. Kujua siri za Mungu (mafumbo ya Mungu)

2. Kujua karama ulizopewa na Mungu

3. Kutafsiri mambo ya rohoni

4. Kuwa na nia ya Kristo (hata kama dunia haitakuelewa)

1 Kor 3:1-3 “1 Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. 2 Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,3 kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?

Kuna aina 3 za waumini makanisani. Nao ni watu wa tabia ya asili (wasiookoka), watu wa mwilini (waliookoka lakini wanaishi kimwili/kidunia) na watu wa rohoni (waliookoka na kumuishia Bwana Yesu). Ukiona mtu ameokoka lakini ana wivu na fitina, bado anaishi kimwili na sio kiroho.

Rum 8:12-14 “12 Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, 13 kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.

Mtu anayeongozwa na Roho Mtakatifu anakuwa MWANA na sio MTOTO (wakati unapookoka ndipo unakuwa mtoto). Hutaendelea kuishi kama mtoto bali utakuwa mwana (kijana mkubwa) anayeweza kujitegemea na kupewa majukumu na Mungu.

Mathayo 3:17 “na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Yesu hakuambiwa maneno haya akiwa mtoto bali Kijana Mkubwa aliyepewa majukumu na Baba Yake. 

MAOMBI

1. Ee Mungu naomba unifanye kuwa mtu wa rohoni ili nikujue zaidi kwa kuwa Wewe ni Roho. Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

2. Ee Mungu naomba unisaidie kujua nini kinaendelea katika maisha yangu. Nijue mipango uliyonipangia ili niisimamie na nijue mipango aliyopanga shetani juu yangu ili niipinge. Yakobo 4:7 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.”

3. Ee Mungu naomba unijulishe karama ulizonipa ili nisikutumikie kwa kubahatisha na kutokuwa na matokeo mazuri. Najua kila mtu umempa karama fulani.  Warumi 12:6 “Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya Imani.”
4. Ee Mungu naomba niongezeke na kukua kama Wewe ulivyokua katika maeneo yote ili nipokee mambo makubwa. Luka 2:52 “Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.” (Yesu alikua kimwili, kiakili, kiroho na kijamii).

1 Wakorintho 14:20 “Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu; lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, bali katika akili zenu mkawe watu wazima.

NB: Jitahidi kutenga muda kila siku kwa ajili ya maombi haya. Maombi haya yanakuandaa kupokea majibu ya mahitaji yako binafsi pia. Hutapokea majibu yako kama hujafikia viwango vya kustahili kupokea.

Unapokuwa na ushuhuda, swali na hitaji binafsi usisite kuniuliza au kunipigia. Sio mambo yote yanahitaji kuombewa. Mengine yanahitaji kupewa ushauri au mwongozo.

Lawi Mshana