Mara nyingi
tunatumia nguvu kubwa kujaribu kubadilisha watu wengine na mazingira yetu na
kujisahau sisi wenyewe. HUWEZI KULETA TOFAUTI KAMA KAMA WEWE MWENYEWE HUTAKUWA
MTU WA TOFAUTI. WEKEZA KWAKO MWENYEWE! Hatuhitaji tu MABADILIKO bali MAGEUZI
katika maisha yetu.
Mifano ya mageuzi katika Biblia
1. Sauli alihitaji kupata mageuzi kabla
ya kuwa mfalme wa Israeli
Moja ya matokeo
ya upako wa Sauli ilikuwa kugeuzwa awe mtu mwingine. Huwezi kupakwa mafuta kwa
kusudi fulani, halafu uendelee kuonekana vilevile.
1 Sam 10:6 “na roho ya Bwana itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao,
nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine.”
2. Unahitaji mageuzi katika fikra zako
na sio kiroho peke yake
Kuna watu
wengine wamempokea Bwana Yesu moyoni lakini hawajamruhusu awafanye upya katika
fikra zao. Matokeo yake mipango yao haipangiki na haitekelezeki.
Rum 12: 2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa
upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza,
na ukamilifu.”
3. Unahitaji kujua kwamba kuokoka sio
kumaliza safari bali ni mwanzo wa safari ya mageuzi
Kuna baadhi ya watu
waliookoka ambao wanadhani kuokoka ni kukiri tu bila kuwa na matokeo dhahiri. Wanatafsiri
vibaya maandiko matakatifu. Hawajui kwamba kuokoka ni MWANZO WA SAFARI na sio
MWISHO WA SAFARI. Wanasahau kwamba wana wa Israeli waliokoka na mikono ya Farao
Misri wakiwa wanaume laki 6 (sawa na milioni 3 tukihesabu pia wanawake na
watoto) na wakafika Kanani WAWILI TU miongoni mwao. Wengine wote waliofika walizaliwa
wakiwa safarini. Maana ya ‘YAMEKUWA MAPYA’ ni MAISHA MAPYA YAMEANZA yaani
kuanza safari mpya ya kiroho hadi ufikie hatima uliyopangiwa na Mungu na sio
kuhudhuria tu ibada ukihesabu miaka ya umri wako.
2 Kor 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya
kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”
4. Ukiwa kiriba cha kale huwezi kubeba
divai mpya – utapasuka
Maono mapya yanahitaji kukuta mbeba maono mpya. Kama mbeba maono uko kizamani, maono mapya yatakuletea madhara na yatapotea. Unaweza kuwa na maono mazuri lakini wewe mwenyewe hufai kuyabeba maono hayo. Bwana Yesu anasema maono mapya yatakupasua kama hujaandaliwa kuyabeba.
Lk 5:37,38 “Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama akitia, ile divai mpya itavipasua vile viriba, divai yenyewe itamwagika, na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya.”
Maombi
1. Ee Mungu naomba unigeuze niwe mtu tofauti anayeweza kuleta
tofauti katika jamii inayohitaji msaada wa Mungu.
2. Ee Mungu naomba unigeuze kifikra ili niweze kuhakiki
mapenzi yako na mpango wako kuhusu maisha yangu.
3. Ee Mungu nisaidie nisiwe na wokovu wa kuigiza usio na
matokeo chanya bali niwe mtu aliyebadilishwa.
4. Ee Mungu naomba unifanye kiriba kipya ili maono mapya unayonipa yasinipe madhara bali yanipe hatua nyingine.
Unaweza kujiunga na makundi yetu ya maombi Facebook ili upate miongozo mbalimbali kuhusu maombi na maombezi.
Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania