Ticker

6/recent/ticker-posts

Tambua kalenda ya Mungu kuhusu maisha yako ili usije ukakufuru na kukosa shukrani


 TAMBUA KALENDA YA MUNGU KUHUSU MAISHA YAKO ILI USIJE UKAKUFURU NA KUKOSA SHUKRANI

Kama tunavyoona misimu ikibadilika kila mwaka, ndivyo ilivyo kwa maisha yako binafsi. Mungu ana kalenda maalum kwa ajili yako tangu uzaliwe. Unatakiwa kuigundua na kutoilinganisha na ya mtu mwingine. Mungu ana mpango maalum kwa ajili ya maisha yako ya leo na kesho. Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” Maneno ya andiko hili yanayosema “kuwapa tumaini siku zenu za mwisho”, ni tafsiri ya “to give you a future and a hope.” Nadhani umewahi kusikia watu wakisema, “Huyu fulani hana ‘future’.” Mungu anataka ujue mpango wake kwa ajili ya leo na kesho yako na kisha uufuatilie na kuusimamia.

1. Mungu ameweka majira maalum kwa ajili ya maisha yako

Muulize Mungu ujue kusudi lake kwa ajili ya hali unayopitia leo. Mhubiri 3:1,8 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.”

Mungu habadilishi mioyo ya watu peke yake. Ndiye anayebadilisha pia majira au misimu. Danieli 2:21 “Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa.”

2. Jifunze kukubaliana na mpango wa Mungu katika hali zote

Sisi tuliomwamini na kumuishia Bwana Yesu, uraia wetu uko mbinguni na sio hapa duniani. Wafilipi 3:20 “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo.” Hivyo hapa ugenini au safarini tunatakiwa kuwa tayari na hali zozote. Mtume Paulo alijifunza maisha ya aina zote. Wafilipi 4:12 “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.”

Kuna jambo lilikuwa linamsumbua sana mtume Paulo. Akamuomba Mungu amuondolee. Kinyume chake Bwana akamwambia, NEEMA ALIYOMPA INATOSHA KUISHI NALO NA FAIDA YA KUISHI NALO NI KUTEMBEA KATIKA UWEZA WA MUNGU. MTAZAMO WA PAULO UKABADILIKA KABISA. AKAACHA KULALAMA. 2 Kor 12:7-10 “Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”

3. Tambua kinachoendelea sasa katika maisha yako – usiishi kwa kubahatisha

Bwana Yesu aliulilia mji kutokana na madhara ambayo aliona yataupata kwa sababu ya kushindwa kutambua kalenda ya Mungu kwao. Lk 19:41-44 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.”

MWISHO

Kama ambavyo mvua hazinyeshi mwaka mzima na kiangazi sio mwaka mzima, unatakiwa kujua uko msimu gani na kujua baraka zake ni za aina gani. Kama sio wakati wako wa kuvuna pengine ni wakati wako wa kupanda au kupalilia. Usilazimishe kupata mavuno wakati ni kipindi cha kutafuta mbegu za kupanda.

Umeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Wewe si wa kawaida. Hivyo usijidharau. Zaburi 139:14 “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana.”

Maombi

1. Ee Mungu naomba uniwezeshe kutambua niko katika msimu gani kulingana na kalenda yako ili nisilazimishe maisha ambayo hujanipangia.

2. Ee Mungu naomba unifundishe kuishi kama MGENI wa duniani na MWENYEJI au RAIA wa Mbinguni.

3. Ee Mungu naomba unisaidie kujua sababu ya mapito yangu ili nisije nikakukufuru na kushindwa kukushukuru.

Unaweza kujiunga na kundi letu la maombi ili upate miongozo mbalimbali kuhusu maombi na maombezi.

Kiungo cha Kliniki ya Uponyaji ni https://www.facebook.com/groups/2358596387744616

Lawi Mshana, 0712-924234.