Kuna watu wanatafuta sana mafanikio lakini wameshindwa kutokana na kuingia au kuingizwa katika maagano ya kishetani kwa kujua au kutokujua. Agano lina nguvu ya kisheria ya kumfunga mtu (legally binding). Hivyo haliwezi kuvunjika kienyeji. Kumbuka AGANO (COVENANT) ni tofauti na MKATABA (CONTRACT). Mfano, ndoa ya Kikristo ni Agano kati ya Mungu na wanandoa ambalo haliwezi kuvunjwa na mwanadamu. Lakini mkataba uliosainiwa na watu wawili unaweza kuvunjwa. Ndiyo sababu Biblia inasema hivi: Mathayo 19:6 “Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”
Usalama wetu uko katika Agano la Mungu alilofanya na sisi au baba zetu. Kutoka 6:5 “Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu.” Mambo ya Walawi 26:42 “ndipo nitakapokumbuka agano langu pamoja na Yakobo, tena agano langu na Isaka, tena agano langu na Ibrahimu nitalikumbuka; nami nitaikumbuka nchi hiyo.
Kama mwenye
nyumba ni mchawi na anataka usiondoke kwa vile unamlipa kodi kwa wakati,
anaweza kukufunga usijenge nyumba. Hata kama unapata pesa anahakikisha
zinaishia kwenye kodi yake, kula, kuvaa na kuchangia sherehe za watu. Na kama
mwenye nyumba amezindika nyumba uliyopanga na kufanya maagano fulani, unaweza
kujikuta wewe ni sehemu ya maagano hayo. Ndiyo maana wakati mwingine unaota
ukiwa unakaa nyumba hiyo wakati miaka mingi imepita tangu uhame nyumba hiyo.
Maswali ya msingi kujiuliza.
1. Wewe una agano gani na Mungu wako ambalo unaweza
kulisimamia ili ufanikiwe? Malaki 2:5 “Agano langu naye lilikuwa agano la uhai na
amani; nami nikampa ili aogope, naye akaniogopa, akalicha jina langu.”
2. Maagano gani yamefanywa na baba zako au wewe mwenyewe
ambayo yanaongoza maisha yako? Umeyasimamia (kama ni mazuri) au kuyavunja (kama
ni mabaya)?
Isaya 28:18 “Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo.”
NJIA ZA KUINGIZWA KWENYE MAAGANO YA KISHETANI
1. Waganga wa kienyeji
Unapowaendea waganga wa kienyeji wanakuingiza katika agano kwa kukuchanja chale, kukunywesha na kukuapiza. Kama uliwaendea zamani lakini hujatumia damu ya Yesu kufuta kumbukumbu hizo, wanaweza kuendelea kukuathiri kimaisha hata kama kiroho hawawezi.
Law19:31 “Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
2. Zinaa
Unapozini
na mtu mnakuwa mwili mmoja na yeye na kuambukizana roho mbalimbali kv magonjwa,
umasikini nk. Kuna mama tajiri aliibiwa utajiri wake na mtu masikini alipoanza
mahusiano naye kwa ngono. Wapo wengine wanaingizwa katika maagano hayo kwa njia
ya ndoto za ngono mpaka ndoa zao zinavunjika na wanakuwa masikini kabisa.
Wengine wakiwa wapenzi wanaapishana kwa agano na kujikuta wakiteseka baadaye.
Mfano, mmoja anamwambia mwenzake nisipoolewa na wewe sitaolewa tena au bila
wewe siwezi kuishi nk.
1
Wakorintho 6:16 “Au hamjui ya kuwa yeye
aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa
mwili mmoja.”
3. Ushirika na mawakala wa shetani
Usifanye kazi ya ubia na mtu mwenye maagano na shetani. Tunahitaji macho ya kiroho ya kutambua watu tunaofanya nao kazi au biashara. Kama mtu mnayeshirikiana biashara anatumia sehemu ya faida yenu kutafuta zindiko, anakuingiza katika maagano. Wengi tunadhani andiko linalosema MSIFUNGWE NIRA NA WASIOAMINI KWA JINSI ISIVYO SAWASAWA ni katika eneo la ndoa au imani tu. Sivyo! Unaweza kufungwa nira na wakala wa shetani katika shughuli zako pia.
2 Kor 6:14,15 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?”
4. Kutumia jina lenye agano na shetani
Jina lako likiwa na maana mbaya au kama umerithishwa na mtu
mwenye tabia mbaya au matatizo, unafungua mlango wa kufanana naye. Agano
linapata nguvu zaidi pale yule aliyelifanya anapofariki. Hivyo kataa jina
ambalo linafungua milango ya kumilikiwa na mapepo.
1 Nya. 4: 9-10 “Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”
Mungu alibadilisha watu majina ili waweze kufikia malengo ya Mungu na hatima aliyowapangia. Abramu akawa Ibrahimu na Simoni akawa Petro. Mwanzo 17:5 “wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Mt 16:16-18 “Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”
5. Ibada ya kishetani
Unapoabudu katika imani fulani na kujiunganisha na madhabahu yake kwa kutoa sadaka, hakikisha umejiridhisha kwamba inatoka kwa Mungu aliye hai. Shetani akipokea sadaka kutoka kwako anakuingiza katika madhabahu yake na kuwa kuhani wa maisha yako.
Kum 12:13,14 “Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo; bali katika mahali atakapopachagua Bwana katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo.”
6. Sherehe za kipagani
Kuna watu
wanaweza kukuingiza katika maagano mabaya kwa njia ya sherehe na chakula
wanachokukaribisha. Unatakiwa kuepuka sherehe za kishetani. Mtu anaweza kuandaa
sadaka ya kukufanya uwe tegemezi kwake kiuchumi na kuhakikisha unaila. Ila yeye
ukimkaribisha katika sherehe yako hawezi kufika.
Kut 34:15 “Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi,
watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu
mmoja akakuita, ukaila sadaka yake.”
Maombi
1. Nafuta kumbukumbu zote kwa mawakala wa shetani niliohusiana
nao, waganga walioniagua na madaktari na manesi waovu walionitibu, katika Jina
la Yesu.
2. Navunja maagano yote niliyofanya kwa
ndoto, na wapenzi wa zamani na marafiki waliokuwa na nia mbaya na mimi katika Jina la Yesu.
3. Nafuta maneno mabaya yaliyotamkwa juu
yangu na watu
wanaonichukia katika Jina la Yesu.
4. Naharibu madhara yote niliyopata kwa kupokea huduma mbali mbali zenye uvuvio wa kishetani kama kunywa damu, migahawa ya wachawi, mafundi walionishonea, vitu na zawadi nilizopewa nk (Taja kila unachokumbuka na kukazia pale unapoona unapata msisimko wa kuwepo kwa nguvu za giza).
Lawi Mshana, +255712-924234, Tanzania


