TAMBUA VISABABISHI VYA MKWAMO WA MAISHA YAKO NA KUVIFANYIA KAZI
Watu wengi
wanashindwa kupata ushindi kwa vile wanaishi kwa dhana (assumption) badala ya
kuhakiki na kuthibitisha chanzo cha matatizo yao. Kabla ya madaktari kukupa
dawa wanafanya kwanza uchunguzi kutokana na dalili fulani (diagnosis). Lakini
pia wanapima madhara yanayoweza kutokea mbeleni (prognosis). Hata wanaofanya
biashara au huduma makini wanahakikisha wana mpango uliochanganuliwa vizuri (business
plan).
Mambo haya ni
ya muhimu pia katika masuala ya kiroho na kimaisha kwa ujumla wake.
Hutashughulikia tatizo vizuri kama unashughulika na majani badala ya mizizi ya
tatizo lako.
Napenda kukupa
mifano kadhaa ya visababishi vikuu vya mkwamo wa maisha yako:
1. Wewe mwenyewe
Kutomsikiliza
wala kumtii Mungu anaposema na wewe . Yona alikataa wito wa kwenda kuwahubiri
toba watu wa taifa jingine. Inavyoonekana hakutaka maadui zake watubu na
kusamehewa na Mungu.
Yona 1:1-4 “Basi
neno la Bwana lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,
Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa Bwana; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa Bwana. Lakini Bwana alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.”
Yona alipokimbia wito wa Mungu alisababisha matatizo kwa wengine. Ilipobidi atupwe baharini Mungu akatuma samaki ammeze. Mungu alitaka Yona atubu akiwa ndani ya tumbo la samaki. Nani ajuaye kama na wewe hupo ndani ya tumbo la samaki kipindi hiki? Ukikubali kosa lako na kutubu kwa moyo wako wote, Mungu atasema na samaki aliyekumeza ili akutapike kule unapotakiwa kwenda – ili mradi uaminike kwamba utakwenda kutekeleza maagizo uliyokuwa umeyakataa awali. Yona 2:10 “Bwana akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.”
Lakini pia unaweza kusababisha ugumu wa maisha yako kwa kukataa kujifunza ujuzi mpya, kuwa na matumizi mabaya ya fedha zako, kuwa mvivu, kuchagua kazi wakati huna ujuzi rasmi, kutojali au kutodumisha mahusiano mazuri na watu wenye baraka zako na wenye fursa mbalimbali, kutopata ushauri kwa watu sahihi nk
2. Shetani
Shetani anapeleka mashitaka kwa Mungu kuhusu maisha yako. Hoja zake zikiwa na mashiko kutokana na tabia yako mbaya, anaweza kuzuia majibu yako. 1 Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”
Ayu 2:3,4 “Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu. Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake.”
Paulo alipozuiwa na shetani hakuogopa kusema wazi ingawa alikuwa na huduma kubwa. Alijua tunapaswa kuweka wazi kazi za shetani ili ziharibiwe. Kuna wakati shetani anaweza kuzuia majibu ya maombi yako. Usipende kuwa na visingizio ili tu uonekane hujakwamishwa. Wengi tukishindwa tunapenda kusema mambo yameingiliana, ratiba imebana nk. Lakini ukweli ni kwamba tulishindwa kwa vile shetani alituzuia hivyo tumpinge tukiwa thabiti katika imani. 1 The 2:18 “Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.”
3. Wanadamu (marafiki, familia, wapendwa nk)
(i). Rafiki zake Ayubu walimhukumu badala ya kumtia moyo.
Ayubu 32:3 “Tena hasira zake ziliwaka juu ya hao rafiki zake watatu kwa sababu hawakupata jawabu, lakini wamemhukumia Ayubu makosa.”
(ii). Mke wake Ayubu alimshauri amkufuru Mungu afe badala
ya kuwa faraja kwake
Ayubu 2:9 “Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe.”
(iii). Wapendwa au waumini wenzako walioikana imani
wanaweza kukukwamisha
1 Timotheo 1:19,20 “uwe mwenye imani na dhamiri njema, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia kwa habari ya Imani.Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.”
Mungu anachukulia kwa uzito sana wapendwa waliokana imani.
1. Anasema wala msimpe salamu 2 Yohana 1:10 “Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.”
2. Anasema msikubali kula naye 1 Wakorintho 5:11 “Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.”
Maombi
1. Ee Mungu naomba unijulishe dhambi yangu inayosababisha nipate
matatizo ili niitubie na kuiacha.
2. Ee Mungu naomba usinitie majaribuni bali uniokoe na yule
mwovu.
3. Ee Mungu naomba unipe macho ya kuwatambua watu wenye nia
mbaya na mimi na jinsi ya kuwaepuka
4. Ee Mungu naomba unisaidie nijue jinsi ya kuepuka waovu wasinajisi maisha yangu ya kiroho ili nisije nikapata mapigo yao. Ufu 18:4 “Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.”
Unaweza kujiunga na makundi yetu ya maombi ili upate miongozo mbalimbali ya muda mrefu kuhusu maombi na maombezi.
Kiungo cha Kliniki ya
Uponyaji ni https://www.facebook.com/groups/2358596387744616
na Maombezi ni https://www.facebook.com/groups/347180092411556