Usiku wa kuamkia jana niliona watumishi ambao walikuwa wamejishusha na
kuishi maisha ya kawaida wakitumiwa na Mungu kusaidia wengi wenye uhitaji
kimaisha.
Angalizo:
Tuko katika kipindi ambacho
watumishi wengi wa uongo wanacheza na akili za watu na kutumia umasikini wao
kujitajirisha. Waumini wengi wako foleni wakisubiri ahadi ambazo hazitimii kwa
sababu wamewaendea watumishi ambao wana maagano na shetani. Kwa tafsiri
nyingine wamewaendea watu ambao ni ‘kopela’ hivyo wanafilisika zaidi. Hata
hivyo tunatakiwa kuwatambua watumishi wenye sifa za kibiblia. Watumishi hawa wako
tayari kuishi maisha ya kawaida ili wawaokoe wengine katika moto kwa kutumia
kanuni za Biblia Takatifu.
Tabia za watumishi wa kweli
wanaoweza kuinua maisha ya watu wanaowahudumia:
1.
Hawapendi kutumikiwa bali kutumikia
Hawatafuti kutetemekewa, kusujudiwa,
kupigiwa magoti wala kuitwa majina yanayochukua nafasi ya Bwana Yesu. Wana
tabia ileile ya Bwana wao wanayemtumikia yaani, YESU KRISTO – ambaye hakupenda
kujionyesha kwamba ametoka mbinguni na alipenda kuwatumikia wanadamu. Fil 2:4-7
“Kila mtu
asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni
na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya
Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;
bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa
wanadamu.”
Mathayo 20:28 “kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja
kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
Badala ya Bwana Yesu kuwaagiza
wanafunzi wake wamtawadhe miguu, Yeye ndiye aliwatawadha. Hii ni roho ya
kutumikia (servant spirit). Yn 13:4-8 “aliondoka
chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni.
Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na
kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo
akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia,
Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe
hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika
nami.”
2.
Hawachanganyi wito na mali
Kuna Mungu wa mbinguni na
mungu-mali (mammon). Mtumishi anaweza kuwa msomi wa Theolojia na kumtaja Mungu
kwa maneno lakini moyoni mwake ametanguliza mungu-pesa. Huyu Mungu-pesa katika
Biblia anaitwa ‘mammon.’ Huyu mungu-pesa anamfanya mtumishi athamini wale tu
wenye pesa, ajilimbikizie mali bila kujali anaowaongoza, apime mafanikio ya
huduma yake kwa kumiliki pesa na mali badala ya utendaji wa Roho Mtakatifu
(dalili za Roho na nguvu). Huyu mungu-pesa
ndiye anasababisha baadhi ya watumishi kutoza watu walipie huduma ambazo Bwana
alizitoa bure.
Luka 16:13 “Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana
wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na
huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.”
3.
Hawana tabia ya kupenda fedha
Hawatafuti kuitwa matajiri
bali kutimiza mahitaji katika kiwango walichopangiwa na Mungu. Wanajua kiwango
cha maisha walichokusudiwa na Mungu na hawatafuti njia za mkato katika
kufanikiwa.
Waebrania 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi
na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa,
wala sitakuacha kabisa.”
Ukitafuta kuwa tajiri kwa
haraka bila uaminifu utaadhibiwa na Mungu. Mithali 28:20 “Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa
tajiri hakosi ataadhibiwa.”
4.
Hawatumainii utajiri wa dunia bali Mungu
Shauku yake ni kuona Mungu
anainuliwa na watu wanakutana na Mungu. Baraka anazopata anazitumia kwa utukufu
wa Mungu na sio kwa kujinufaisha mwenyewe. Utajiri wake unatoka kwa Mungu na
sio katika maagano ya kishetani yenye masharti yanayowagharimu wafuasi wake. Waumini
wanaojiunganisha na watumishi wa kishetani wanatolewa kafara au kuingizwa (kuwa
initiated) katika maagano yanayowatesa hata wanapotoka katika imani hizo. Wakifunguka
macho na kuamua kuachana na imani hizo potofu wanatakiwa kuombewa na watumishi wa
kweli wenye mamlaka katika kuvunja hayo magano ya kishetani. Vinginevyo
wataishi maisha magumu sana kwa vile walikula kiapo kwa hiari yao wenyewe.
1 Timotheo 6:17 “Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa
uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini
Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.”
Shuhuda za watumishi wa kweli
zinahusu ukuu wa Mungu na sio mali wanazomiliki hapa duniani. Zaburi 20:7 “Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali
sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.”
5.
Shauku yao ni kutajirisha wengi na sio kujitajirisha wao wenyewe
Hawawezi kufurahia
kujilimbikizia mali na kujionyesha kwa watu wakati waumini wao wanaomcha Mungu
wamechoka kimaisha, ni tegemezi, ombaomba na wanalala njaa. Wanakuwa na juhudi
za kuwasaidia waumini na jamii ijue mbinu za kupata upenyo wa kimaisha na sio
kuhamasisha utoaji peke yake. 2 Wakorintho 6:10 “kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali
tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.”
Kuna waumini wamefikia hatua
ya kuchenji pesa ili wamudu kutoa sadaka nyingi ambazo zinatolewa kila siku ya ibada
na mara nyingi hakuna uwajibikaji wala mrejesho wa wazi wa matumizi yake. Mungu
ametuagiza kumtolea lakini hapendi waumini wapangiwe kiasi cha kutoa. 2 Wakorintho
9:7 “Kila mtu
na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima;
maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.” Tuwe wabunifu
wa njia zingine za kupata kipato kwa vile Neno la Mungu limetuagiza pia kufanya
kazi kwa bidii. Asiyefanya kazi hatakiwi kula chakula. Ndiyo maana wengine
tunashona hema kama mtume Paulo ili tusiwalemee waumini wetu wala kuweka tozo
katika huduma tulizopewa bure. 1 Wathesalonike 2:9 “Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana
na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu.” 2
Wathesalonike 3:10 “Kwa kuwa hata wakati
ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya
kazi, basi, asile chakula.”
MAONO
YA USIKU WA KUAMKIA LEO
1. Nimeona waumini wanaomba
wakiwa katika ukame wa kiroho bila bubujiko na mhubiri ameishiwa maneno kiasi
kwamba mahubiri yake hayana mvuto. (Nimemuomba Mungu akuhuishe wewe ambaye
umeibiwa bubujiko la Roho ili usitumike kwa kujilazimisha).
2. Nimeona wanafunzi watano
wanarubuniwa kufanya mapenzi shuleni. (Hii ni roho inayoharibu watoto wetu
mashuleni. Tukemee na kubomoa madhabahu za uasherati mashuleni badala ya
kulalamika na kulaumu tu. Wanaofanya vitendo hivi wengine wamepagawa na mapepo
hayo na wanajuta kwa kufanya vitendo hivyo lakini wanashindwa kuacha.)
Maombi ya wiki hii:
1.
Ee Mungu naomba unipe macho ya kuwatambua watumishi wa kweli ili nisije
nikatolewa kafara.
2.
Ee Mungu naomba uniwezeshe kukuabudu Wewe peke yako badala ya kukuchanganya na
mungu-pesa (mammon).
3.
Ee Mungu naomba unipe uwezo wa kuwatajirisha wengi badala ya kutawaliwa na
ubinafsi na uchoyo.
4.
Ee Mungu naomba unipe bubujiko la Roho wako ili nisijilazimishe kukutumikia
bali nitumike kwa shangwe na furaha ya moyo.
5.
Tumia mamlaka ya Jina la Yesu kuharibu maagano na madhabahu za shetani
zinazotesa wanafunzi. Shetani anajua ni rahisi kuwaharibu wanafunzi kwa vile
wametoka mikononi mwa wazazi ambao ndio walimu wakuu wa malezi.
Kumbuka
ku-follow kurasa zetu na kujiunga na makundi yetu ili uendelee kupata mafundisho
ya kukua katika neema ya Mungu na kushinda changamoto za maisha.
Dr. Lawi
Mshana, 0712-924234, Tanzania