NB:
Soma mpaka mwisho uijue roho ya ‘fantasia’ inavyotenda kazi leo.
Juzi Ijumaa: Nimeona mtu yuko katika uhatarishi ambao
akiendelea kuupuuza atapata madhara makubwa
Jana Jumamosi: Nimeona watumishi wanaoombea watu na
kuwashika shika sehemu za mwili isivyofaa, wakichukuliwa hatua za kiroho na
kisheria.
Utangulizi
Bwana Yesu aliwahi kutoa mfano kuhusu mjenzi mwenye busara
na mpumbavu na namna ambavyo nyumba ya yule mpumbavu ilianguka vibaya. Sababu
kuu ilikuwa ni msingi mbovu ambao haukuweza kustahimili mafuriko na upepo
mkali. Mt 7:27 “mvua ikanyesha, mafuriko
yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa
kubwa.” Usipuuze mazingira ya huduma, kazi, biashara, marafiki, majirani,
ndoa nk. Yana mchango mkubwa katika mafanikio yako au anguko lako.
Kwa
namna gani uko katika mazingira hatarishi?
1. Una
kiburi hivyo hutaki kujifunza kwa wengine
Mithali 16:25 “Iko
njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”
Kujiamini ni jambo jema sana lakini uwe makini usijiamini
kupata kiasi. Wengi waliosema sio rahisi kuanguka walianguka kwa vile
walitegemea nguvu zao wenyewe. Usipende kujiona kwamba unajua kila kitu/kuwa
mjuaji (know-it-all) – tunategemeana. Biblia inasema hakuna mtu anaanguka bila
kutanguliwa na roho ya kiburi. Mithali 16:18 “Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia
maanguko.” Ukimuuliza kila mtu aliyeanguka iwe kiroho, kimaisha, kihuduma
nk atakuambia kwamba kuna mahali hakutii jambo fulani kv ushauri, sauti ya
moyoni nk. Kuna wakati unakatazwa kumkopesha mtu au kufanya kazi na mtu fulani
halafu wewe unapuuzia sauti hiyo. Halafu unagundua kosa lako baadaye. 1
Wakorintho 10:12 “Kwa hiyo anayejidhania
kuwa amesimama na aangalie asianguke.”
2.
Unakaa karibu na dhambi iliyowahi kukutesa sana
Waebrania 12:1 “Basi
na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na
tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige
mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu.”
Fahamu vizuri tabia za aina ya watu unaoshirikiana nao.
Kama hufanani nao itakuwa umekubali kuathiriwa na tabia zao. Mara nyingi
shetani anapenda kuleta vishawishi vinavyoendana na aina ya dhambi uliyowahi
kufanya. Anazo kumbukumbu za maisha yako. Anapojua kwamba kwa umri huo kuanza
upya kukushawishi uvute sigara inaweza kuchukua muda, anafuatilia maeneo ambayo
una udhaifu na kuelekeza nguvu zake zote hapo. Hivyo epuka maeneo ambayo ni rahisi
zaidi kushawishika. Kumbuka miili yetu haiokoki bali inatiishwa na kusulubiwa. Wagalatia 5:24 “Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake
mabaya na tamaa zake.”
3.
Hupigani vita vya kiroho – unakiri ushindi bila kupigana vita
Waefeso 6:13 “Kwa
sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu,
na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.”
Katika hivi vita vya kiroho lazima tuzingatie mambo kadhaa.
La kwanza, lazima tuvae SILAHA ZOTE ZA MUNGU (sio baadhi). La pili, lazima
tushindane au tupambane (kumiliki bunduki bila kuitumia au kujua kuitumia ni
hatari sana), La tatu, lazima tuwe macho muda wote kwa vile shetani hafi
(tusiwe na maombi ya msimu). Moja ya silaha ambayo hatuitumii sana ni KUOMBA
KATIKA ROHO MTAKATIFU. Maombi yetu mengi ni ya akili hivyo hatugundui adui ni
yupi, yuko upande gani, anatumia silaha gani na sisi wenyewe tuna nguvu kiasi
gani. Matokeo yake tunaaibika bila kutegemea. Yuda 1:20 “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana,
na kuomba katika Roho Mtakatifu.”
Hivyo lazima tujue chanzo cha vita kabla ya kuanza
kupigana. Yakobo 4:1 “Vita vyatoka wapi,
na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu
zifanyazo vita katika viungo vyenu?”
4.
Hutaki kupima roho uliyo nayo
1 Yohana 4:1 “Wapenzi,
msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa
sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.”
Unaweza kumpenda Mungu na kupenda kumtumikia na wakati huohuo una roho nyingine inayotenda kazi ndani yako. Utaijua kwa kupima hisia zako, nia yako na kama unakosa amani moyoni. 2 Kor 10:4,5 “(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo.
Tumepewa silaha zenye uwezo wa kuangusha ngome za shetani ambazo ni “MAWAZO NA FIKRA POTOFU.”
Napenda
ujue kidogo shetani anavyotumia ya roho ya fantasia ndani na nje ya kanisa:
1. Kuamsha hisia za mapenzi kwa mtu ambaye sio mwenzi wako.
Mf kumpapasa, kumkonyeza nk
2. Kuvaa nguo ambazo unalenga kuwatamanisha watu tofauti na
mwenzi wako-unawakosesha na kuzini nao katika ulimwengu wa roho. Unakaribisha
kuolewa na majini na kisha kuota ndoto za mahaba.
3. Kufurahia na kutojizuia kuangalia watu ambao wako uchi
au nusu uchi kv kuwachungulia wakiwa nyumba za kulala wageni, wakiwa wanaoga,
kuwatazama kwenye TV, simu nk
4. Kumfikiria kimapenzi mtu ambaye sio mwenzi wako wa maisha.
Hata kama hajui, shetani anajua kwamba unazini naye kwa mawazo na anakusubiria
tu ufe ili ukateseke milele.
5. Kutumia vitu vya kusisimua na kuamsha hisia za ngono.
Mfano siku hizi kuna ongezeko la midoli ya kike iliyovalishwa nguo za ndani,
wengine hawajui shampeni inatoa ujumbe wa matusi inapofunguliwa. Wanachoangalia
ni kama ni pombe au la. Shetani amejipanga kufanya kazi kwa hila. Mungu atupe
macho ya kiroho. 2 Wakorintho 11:3 “Lakini
nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu
fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.”
Wiki chache zilizopita niliona perfume kwenye duka moja
imeandikwa ‘fantasy’. Juzi tena nikakutana na mtu amevaa fulana ambayo kifuani
imeandikwa ‘fantasia’. Fantasia ni kuwaza mambo ambayo hayawezi kutokea na mara
nyingi mtu anakuwa mtumwa wa mawazo ya ngono nje ya mwenzi wake wa ndoa. Maneno
kama haya yanapokuwa yameandikwa kwenye nguo zako za ndani au perfume,
usitegemee kushinda utumwa wa ngono. Hata kama hutaki, utajikuta unafuatiliwa
mpaka utakubali vishawishi na kama uko katika ndoa utavutiwa na wengine kuliko
mwenzi wako wa maisha. Pengine unaweza kujipa moyo kwamba unamuwaza mwenzi wako
tu. Mungu hakukusudia wanandoa waishi kwa kuwaziana kwa tamaa mbaya (lustful
desire/fantasize) bali kwa kupendana (love). Fantasia ni dhana isiyo halisi
inayoweza kuweka matarajio yasiyofikika na kusababisha majuto na kumlinganisha
mwenzi wako na wengine. Lakini upendo ni kitu halisi kinachokuwezesha kumpenda
na kumkubali mtu kama alivyoumbwa na Mungu.
Maombi
ya wiki hii:
1. Ee Mungu naomba uondoe roho ya kiburi na kunipa roho ya
unyenyekevu ili nipokee neema yako na msaada wako.
2. Ee Mungu naomba unipe uwezo wa kutambua na kuepuka
mazingira hatarishi na watu hatarishi kwa maisha yangu.
3. Ee Mungu naomba unifundishe jinsi ya kupigana vita
vizuri vya kiroho ili nisishindwe na kuaibika.
4. Ee Mungu naomba unipe ushindi dhidi ya roho ya
‘fantasia’ ili nisije nikapoteza roho yangu milele. Marko 9:47 “Na jicho lako likikukosesha, ling'oe,
ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na
macho mawili, na kutupwa katika jehanum”
Kumbuka ku-follow kurasa zetu na kujiunga na makundi yetu ili
uendelee kupata mafundisho ya kukua katika neema ya Mungu na kushinda
changamoto za maisha.
Lawi Mshana, 0712-924234 (ushauri na maombezi kwa simu au
whatsap)