Mungu ametuumba kwa namna ambayo hakuna mtu anaweza
kujitosheleza kwa kila kitu. Tangu mwanzo aliona kwamba mwanadamu ana upweke
hata kama amempa utajiri. Hivyo akamfanyia Adamu msaidizi wa kumkamilisha.
Mwanzo 2:18 “Bwana Mungu akasema, Si
vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.”
Wengi tukisoma andiko hili tunakuwa na mtazamo finyu wa
kulihusianisha na ndoa peke yake. Tunasahau kwamba Adamu hakuletwa duniani ili
tu aoe. Aliletwa kumiliki na kutawala. Hitaji la mke lilikuwa kumsaidia atimize
jukumu lake aliloitiwa. Adamu hawakilishi mume peke yake bali pia mtawala wa
dunia chini ya uongozi wa Mungu. Adamu na Hawa waliporuhusu ukaribu na nyoka mpaka
kumsikiliza maneno yake walianza kutilia mashaka upendo wa Mungu kwao.
Wakasahau wameletwa duniani kwa misheni maalum. Mwanzo 1:28 “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia,
Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini,
na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”
Kwa
namna gani unaweza kujizungushia watu sahihi kwa usalama wako:
1. Abudu na watu ambao wanakuulizia na kukufuatilia
unapokosekana ibadani
Waebrania 10:25 “wala
tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na
kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.”
Acha kuabudu na watu ambao hata usipokuwepo mwezi mzima
ibadani hakuna mtu anajali. Pengine unapenda hali hiyo lakini unahatarisha maisha
yako. Kanisani sio klabu wala mahali pa kutoa tu sadaka na kusubiri kuzikwa
vizuri bali ni pa kuchungwa ili usitoke nje ya mstari.
2. Acha ubinafsi katika maisha yako ya kiroho
Mhubiri 4:9 “Afadhali
kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.” Kuna
wakati maombi binafsi yanahitajika lakini usipende tabia ya kukwepa kuomba na
wenzako mara kwa mara. Kuna vita zingine zinahitaji nguvu kubwa zaidi ya kushirikiana
na wapendwa wenzako.
Kum 32:30 “Mmoja
angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi, Kama Mwamba wao
asingaliwauza, Kama Bwana asingaliwatoa?”
Kama Bwana Yesu alihitaji kampani alipokuwa katika maombi
Gethsemane, wewe utakuwa salama kujiombea kibinafsi? Wewe endelea kubadilisha
channel za TV hata kama ni za mafundisho wakati wenzako wako kanisani wanaomba,
utajuta siku moja. Kwenye TV unaweza kujengwa lakini huwezi kupata USHIRIKA wa
wapendwa. Mt 26:38 “Ndipo akawaambia,
Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.”
3. Tambua mapungufu yako na ni nani wanaweza kukukamilisha
1 Kor 12:21,22 “Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi.”
Pengine umefika mahali ambapo unadhani kwamba unatosha wewe mwenyewe. Kama wewe ni mguu na hutaki kumwambia mkono akuokotee funguo, utachukua muda mrefu sana na unaweza kushindwa kabisa. Kitakachotokea ni wewe kumlalamikia Mungu kwamba amekuacha na kumbe ni wewe umemuacha kwa kupuuzia watu aliowaweka duniani kukukamilisha.
Usisahau kwamba utoshelevu wetu unatoka kwa Mungu. Anajua nani atamtumia kwa ajili ya lile ambalo unahangaika nalo bila mafanikio. 2 Wakorintho 3:5 “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu.”
Maombi
ya wiki hii:
1. Ee Mungu naomba unipe watu sahihi wa kuwa na ushirika
nao ili nisije nikadanganyika na kupoteza roho yangu.
2. Ee Mungu naomba uondoe ubinafsi kwangu ili nitambue
neema waliyopewa wengine katika kunisaidia kukujua zaidi.
3. Ee Mungu naomba unisaidie kutambua mapungufu yangu na
nani wa kunikamilisha kwa vile mimi ni kiungo katika mwili wa Kristo.
Kumbuka ku-follow kurasa zetu na kujiunga na makundi yetu ili
uendelee kupata mafundisho ya kukua katika neema ya Mungu na kushinda
changamoto za maisha.
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (ushauri na maombezi kwa njia ya
mtandao)