PONGEZI KWA BWANA NA BIBI ERNEST MSHANA KWA KUDHIBITI VILEO NA MIZIKI YA MATUSI
Napenda kuwapongeza wazazi wa Bwana arusi kwa kudhibiti vileo na miziki ya matusi katika arusi ya kijana wao ingawa hawasali dhehebu moja na kijana wao.
Shetani ametumia hila kuwafanya watu wa Mungu ambao hawawezi kumnunulia mtu pombe sasa wanawanunulia watu pombe kwenye arusi. Biblia imetuonya kwamba tuonyeshe tofauti baada ya kuokoka kwa kuepuka karamu za ulafi na vileo. Na imesema wazi kwamba hatutaeleweka kwa kuwa na msimamo huo. Na ikaongeza kusema kwamba wasiotuelewa watahukumiwa kwa kufanya hivyo. Soma mwenyewe andiko hili ujionee mwenyewe. 1 Petro 4:2-5 “Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani.Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali; mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana. Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.” Baadhi yetu tumeomba rehema kwa kuchangia sherehe ambazo tunajua wazi kwamba kuna bajeti ya kununulia pombe.
Mkakati wa kanisa letu:
1. Tunatambua ndoa
ni mpango wa Mungu kwa wanadamu bila kujali imani yao. Ili mradi wanaooana
wamefuata kanuni za msingi kv wazazi wao kuhusika, mahari kulipwa, maadili
sahihi kufuatwa nk (na sio kufungwa kanisani peke yake). Kuna ndoa zina
migogoro mikubwa ingawa zilifungwa kanisani kwa vile wahusika hawana uhalali
wala baraka zozote kutoka kwa wazazi wao. Yesu pia alishiriki arusi ya Kana
kama mwanajamii. Hata hivyo Yesu alipewa nafasi akatenda muujiza.
2. Kama sherehe ina
pombe, miziki ya matusi nk tunakuwepo tu wakati ndoa ikifungwa kanisani na
hatutoi michango wala kwenda ukumbini isipokuwa tunaweza kutoa zawadi kwa
maharusi au wazazi.
3. Ndoa ikifungwa kanisani
kwetu tunafanya sherehe kanisani ili hata washirika wasio na uwezo wa kuchangia
michango mikubwa washiriki. Baadhi yao ndio wameombea maharusi mpaka wakakutanishwa
na Bwana. Kisha ukumbini wataendelea wazazi ambao hatuwezi kuwadhibiti kwa vile
sio washirika wetu ila hatutashiriki labda tu kama tumehakikishiwa kwamba maadili
ya msingi yatakuwepo. Kama hatukai meza moja na walevi kwenye baa hatuwezi
kukaa meza moja na walevi kwenye harusi.
4. Tunashirikisha watu wachangie ambao wako tayari kwa harusi isiyo na vileo nk. Lakini pia tunapenda sherehe zetu ziwatambue hata wasio na uwezo ili nao washiriki maana tumeagizwa hivyo ili tupate thawabu. Luka 14:13,14 “Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.”
Ushuhuda
Tulipofanya maadhimisho ya miaka 25 ya huduma niliyopewa na Mungu, tuliamua kuchangia wenyewe na kuwashirikisha marafiki halafu tukawaalika watu wengi ambao hawakuchangia wakiwemo majirani zetu. Kwa mara ya kwanza majirani wa dini zote walishirikiana na sisi na sherehe ikafana sana. Tulishinda mfumo wa ‘aliyechangia ndiye ana haki ya kula.’ Uzuri wa mfumo wetu wa kualika hata wasiochangia ni kwamba mtu hawezi kulaumu kwamba hakula aina 4 za vyakula kwa vile hakuchangia. Kama anahitaji vyakula hivyo akitoka kwenye sherehe yetu anaweza kupitia hotelini aongezee kile kilichopungua kwetu.
Mwisho
Hatumhukumu mtu yeyote ila tunajitahidi kuepuka yale tunayoweza kadiri iwezekanavyo ili tusionekane kama tunaotenda dhambi kwa kukusudia. Kumbuka hakuna dhabihu ya dhambi kwa ajili ya watu wanaotenda dhambi wanazojua wakijifariji kwamba watatubu badae. Waebrania 10:26 “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi.”