JINSI YA KUHARAKISHA MAJIBU YA MAOMBI YAKO NA AHADI ULIZOAHIDIWA
Pengine umeomba maombi yako kwa muda mrefu na hupati majibu
dhahiri. Na wakati mwingine umeahidiwa na Mungu lakini ahadi haitimii. Napenda
ujue kwamba Mungu anajibu maombi kwa kuzingatia kanuni za Neno Lake. Zipo
kanuni nyingi lakini leo nitakupatia chache za msingi.
1.
Kirimu watu wenye funguo za majibu yako
Ibrahimu aliahidiwa na Mungu kwamba atapata mtoto katika
uzee wake. Mtihani aliotakiwa kuushinda ili apate mtoto ulikuwa ni kupokea wageni
ambao wana funguo za maombi yake. Kama angekuwa mchoyo, angeendelea kufunga na
kuomba bila majibu na pengine angemnung’unikia Mungu kwamba hajamjibu.
Mwa 18:2-4,10 “Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu….Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake.”
Hata Waebrania walisisitizwa kanuni hii ya kukirimu wageni (watu tusiojuana nao) kwamba inaweza kusababisha siku moja ukaribishe malaika (watumishi wa Mungu) wenye majibu yako. Waebrania 13:2 “Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.”
Angalizo: Tabia yako ya kukirimu watu mnaojuana tu inaweza kukunyima baraka zako. Kuna wakati Mungu anawaleta watu wenye funguo za mahitaji yako ili uwasaidie. Ndiyo sababu tunapenda kusaidia wahitaji bila kutarajia shukrani kutoka kwao. Tambua mtihani ambao ukiushinda, utapokea majibu yako dhahiri. Usifunge na kuomba tu na kusubiria majibu. Hata mjane wa Sarepta hakufa njaa kwa vile alishinda mtihani wa kutanguliza mahitaji ya nabii Eliya aliyekuwa mgeni wake. 1 Fal 17:13-16 “Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.”
2.
Tambua ishara za majibu yako na kuhakikisha umeziona
Hakuna kitu kinachotokea bila dalili au ishara, kiwe kizuri
au kibaya. Hata magonjwa yanaambatana na dalili fulani. Kabla Mungu hajatenda
jambo kunakuwa na dalili zinazotangulia. Eliya alijua kwamba mvua haiwezi
kunyesha wakati anga halina mawingu. Hata Waswahili wanasema, “Dalili ya mvua
ni mawingu”. Hivyo Eliya alihakikisha maombi yake yanatengeneza wingu ndipo
awahakikishie watu kwamba mvua itanyesha. Hakuridhika na tabia ya kuomba na
kisha kuamua tu kukiri kwamba Mungu atatenda bila ishara zozote kwamba Mungu amekubali.
1 Wafalme 18:43,44
“Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea,
akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba. Ikawa
mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama
mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.”
Angalizo:
Tambua dalili za kupata majibu yako na kuhakikisha unaomba mpaka unaziona. Acha
tabia ya kudhani tu kwamba kwa vile umefunga na kuomba siku kadhaa utapokea
majibu yako. Unaweza kufunga siku nyingi lakini umeshinda tu njaa na kuhesabu
masaa. Badala ya kupokea majibu ya maombi yako, unaweza kupokea vidonda vya
tumbo.
3.
Tambua vizuri haki yako na kuidai bila kuchoka
Lazima utambue HAKI YAKO au HITAJI LAKO na NI NANI ANA
MAMLAKA YA KULITATUA. Hata kama hataki unamkabili mpaka aidhinishe majibu yako.
Mwanamke mjane (asiye na mtetezi) aliamua kumsumbua bosi mkorofi mpaka huyo
bosi akamjibu bila kupenda. Hakuna siku shetani na mawakala wake watakuhurumia.
Wanahitaji kulazimishwa kwa mamlaka. Mungu pia anapenda umsumbue usiku na
mchana kwa hitaji hilohilo moja na sio kuomba hitaji jipya kila dakika.
Luka 18:1,4,5,7,8 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa… Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima…Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”
Angalizo: Epuka tabia ya kuombea mambo mengi mpaka unasahau uliombea nini juzi na jana. Maombi yenye maana kwako ni yale ambayo unashindwa kunyamaza kuyataja mara kwa mara (ni msiba kwako). Ni jambo lililokuchosha na linalokukera ambalo UNALILIA USIKU NA MCHANA. Mtu akifiwa hatafuti muda mzuri wa kulia wala hatafuti kulia kistaarabu. Choshwa na tatizo lako kiasi hicho, utapokea kutoka kwa Bwana.
Maombi
ya wiki hii:
1. Ee Mungu naomba uniwezeshe kukirimu watu hata nisiowajua
na unipe macho ya kuwatambua matapeli wanaojifanya wana mahitaji kumbe sivyo.
2. Ee Mungu naomba unipe macho ya kutambua ishara za majibu
yangu ili nisije nikapishana na muujiza wangu
3. Ee Mungu naomba unisaidie kutambua haki zangu na jinsi ya kuzipata kwa kuwa na maombi endelevu ambayo sio ya msimu.
Lawi Mshana, 0712-924234 (ushauri na maombezi kwa njia ya
mtandao)

